KWA mara ya kwanza tangu kuanzishwa
kwa Kampasi za Singida na Mwanza chini ya Taasisi mahiri na kongwe ya uhasibu
nchini (TIA) hapakuwepo na kozi ya Shahada ndani ya kampasi zake za Singida na
Mwanza. Hivyo wahitimu wa kozi ya shahada kwa mwaka wa masomo 2018/2019 ndio
wanaofanikiwa kuandika historia ya kuhitimu kozi hiyo kwa mara ya kwanza.
Katika mahafali ya 17 ya (TIA) kwa
kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma, na mahafali ya nane kwa kampasi ya
Singida, jumla ya wahitimu 209 wamehitimu kozi ya Shahada, huku wengine 328
wakihitimu kozi ya Stashahada, Astashahada 504 na ngazi ya cheti 647 wote
wakihitimu katika kozi za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Uongozi wa Rasilimali Watu
na Usimamizi wa Biashara.
Akizungumza kwenye mahafali hayo,
kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt Philip Mpango mkoani hapa jana, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema
Nchimbi, mbali ya kupongeza juhudi lukuki zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuboresha
ubora wa taaluma na wanataaluma, aliwasihi wahitimu hususan wale wa shahada na
uongozi mzima wa TIA kuanza kutumia sifa na ubora wa kitaaluma walionao katika
kuongeza thamani kwa wananchi walio mitaani hususan vijana.
Dkt Nchimbi aliwatakafarisha na
kuwataka wahitimu kujiuliza je sura ya kampasi hiyo huko nje ikoje? Kampasi hii
inavyosifika kwa ubora je na akina mama lishe na waendesha bodaboda na bajaji wanaoizunguka na kuihudumia kila kukicha nao
wamepata fursa ya kuambukizwa ubora huo? Je kampasi hizi zinaonekanaje huko nje
katika kubadili na kuongeza thamani hususan kwa vijana ili kuchagiza na kuleta
chachu ya mabadiliko ya fikra kufikia maendeleo stahiki na ya kiushindani.
“Je haiwezekani TIA kuwa na mafunzo
ya muda mfupi kwa vijana wetu, waendesha bodaboda, bajaji, mama lishe na
wajasiriamali angalau na wao wakawa na mahafali yao ya kila wiki itapendeza, na
itaongeza ubunifu tija na ufanisi ndani na nje ya kampasi zetu kwa maendeleo ya
taifa letu,” alisema Dkt Nchimbi
Alisema watumishi wa Singida
wamejiwekea kauli mbiu yao inayojulikana kama “ Mshahara wangu uko wapi”? huku akichekesha wahitimu kuwa kuna
watumishi ambao wameshapokea mshahara wa mwezi Novemba mwaka huu, lakini
ukimuuliza mpaka sasa hauoni Zaidi ya kulalamika mshahara hautoshi! Na kutoa
rai kwa wanajumuiya ya TIA kuangalia namna ya kuanzisha somo mahususi la matumizi
mazuri ya mshahara (fedha) akiamini ni taasisi hiyo pekee na wahitimu wake ndio
jawabu la kutamka kwanini hautoshi, uko wapi na kutupa maarifa na stadi stahiki
za siku zote kuiona mishahara yetu.
“Sisi wana Singida kwasasa tupo
vizuri, ukimuuliza mtu mshaara wake upo wapi atakuonye mashamba ya korosho,
nyumba nzuri, na n.k, hali inayopelekea kumpenda mwajiri wetu”. Dkt. Nchimbi
Aidha, akizungumzia kuhusu ubora wa
elimu ndani ya taasisi Dkt Nchimbi alisema fani zinazotolewa na TIA ni muhimu
sana katika kuendesha uchumi wa taifa, hususan katika kusimamia mapato na
matumizi ya fedha za umma, hivyo aliwataka kuzidisha kasi ya umahiri huo katika
kufanikisha azma ya sera iliyopo ya Tanzania ya Viwanda.
Alisema dunia ya sasa imetamalaki
teknolojia na utandawazi hivyo jukumu lililopo ni kuendelea kuboresha mitaala
ndani ya taasisi ili wakati wote ikidhi viwango vya kimataifa, na kuwasihi
kuzidisha kuzalisha wataalamu wenye weledi, maarifa na umahiri wa kutatua
changamoto na sio kuziongeza.
“Zingatieni kwa umakini suala la umahiri
katika mitaala yenu ili tuweze kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kulifikisha
taifa kwenye uchumi wa kipato cha kati kabla ya ishirini ishirini na tano (2025),”
alisema Dkt Nchimbi
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi
ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wakili Said Musendo Chiguma, alisema
jukumu la bodi ya ushauri, pamoja na mambo mengine ni kutoa ushauri kwa TIA kwa
nia ya kutekeleza na kuendeleza jitihada za serikali kulingana na malengo makuu
yaliyoianzisha.
Chiguma alisema lengo hasa la
taasisi hiyo ni kutayarisha wahitimu kwa
uboreshaji endelevu wa mitaala, azma ikiwa ni kuandaa wafanyakazi wenye weledi
na uwezo wa kujiajiri, sambamba na maboresho hayo kuzingatia juhudi za kujenga
uzalendo, uaminifu na maadili, huku akisisistiza kwamba mhitimu asiye na sifa
hizo siyo rasilimali kwa taifa.
Alisema kwa matokeo ya vigezo hivyo
taasisi imeendelea kupendwa na kuwa kivutio kikubwa, hali iliyopelekea ongezeko
kubwa la udahili wa wanafunzi kila mwaka licha ya kuwepo vyuo vingi vya
ushindani idadi inayofikia jumla ya wanafunzi 18,585 katika kampasi zake zote
sita ambazo zimesambaa kimkakati.
“TIA ni taasisi ya serikali,
imeweza pia kuchangia bilioni mbili na milioni mia tano (2,500,000,000) kama
ziada ya mapato yake serikalini,” alisema Wakili Chiguma
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA,
Luciana Hembe, alisema Taasisi hiyo kwa sasa ina kampasi 6 zilizopo katika
mikoa ya Dar es Salaam (Makao Makuu), Mbeya, Singida, Mtwara, Mwanza na Kigoma,
zote zikiwa na jumla ya wanachuo 18, 587, huku jumla ya kozi zinazotolewa
katika kampasi zote ni 20.
Hembe alibainisha kuwa, kwa mwaka
2019 katika kampasi zote kuna jumla ya wahitimu 8695 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 35.5 ikilinganishwa na wahitimu 6418 kwa mwaka 2018. Alisema mahafali
hayo ni kwa wahitimu wa TIA ngazi tofauti Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma
kwa mwaka wa masomo 2018/2019.
Alisema idadi ya wahitimu wote
waliohudhuria na wasiohudhuria mahafali hayo katika kozi ya Cheti cha Awali,
Astashahada na Shahada ni 1,688 wakiwemo wanawake 915 sawa na asilimia 54.21,
na wanaume 773 sawa na asilimia 45.79.
No comments:
Post a Comment