Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye kofia ya Tanzania) akiongoza wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa kimkoa Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCD) mkoani Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi amezindua kampeni ya Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti
magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCD) iliyofanyika kimkoa leo Novemba 9, 2019 katika
viwanja vya Bomberdia Manispaa ya Singida.
Dkt Nchimbi alisema, swala la
afya ni swala la kiusalama, hivyo jamii isiyo na afya bora usalama wake ni
mdogo, itakuwa ni jamii ya visasi na kero zisizoisha ndani ya jamii.
Alisema magonjwa yasiyo ya
kuambukiza yanawezekana kuondolewa na kuepukika katika mkoa wa Singida kwa asilimia
mia moja kwa njia ya mazoezi, kwani mazoezi ni kinga na ni tiba ya magonjwa
huku akiwasihi watumishi wa umma mkoani hapa kula mlo kikamilifu hasa wakati wa
asubuhi na mchana ili kulinda na kuimarisha afya itakayoboresha utendaji mzuri
wa kazi katika maeneo ya kazi.
Akizungumza kwa msisitizo Dkt.
Nchimbi alisema “Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanazeesha sana, unaonekana mzee
kuliko hata umri wako…Tuhakikishe tunajenga Singida yenye sifa ya kuwa na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa asilimia sifuri”.
“Singida yetu ni njema tena ni
njema sana… Tuhakikishe tunaijenga Singida yenye sifa ya kuwa na magonjwa yasiyo
ya kuambukiza kwa asilimia sifuri” Dkt. Nchimbi
Hata hivyo, amemwagiza mganga mkuu wa mkoa pamoja na watoa huduma za afya mkoani hapa kufanya ukaguzi wa mapishi kwenye hoteli zote, migahawa ya baba lishe na mama lishe juu ya mapishi bora, sambamba na kutoa elimu stahiki kuhusu afya ya mlo kamili ili kudhibiti magonjwa yanayotokana na vyakula vinavyopikwa kwa kutumia mafuta mengi yanayosababisha kuwa na ugonjwa wa shinikizo la damu (presha).
Mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi mkoani hapa kutokula kila chakula kinacholetwa mezani bali kula chakula bora chenye matokeo chanya ndani ya mwili ili kuwa mtu mwenye afya bora ya kimwili na kiakili.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa
Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi amewasisitiza watumishi wa umma na
wananchi wote wa Singida kufanya mazoezi ili kujenga miili yenye afya bora kwa
faida ya familia na Taifa kwa ujumla.
“Mpaka vijijini watu wanaumwa
magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Hii inaonyesha kuwa kadiri uchumi unavyokuwa
vizuri katika jamii zetu ndivyo magonjwa haya yanavyozidi kuongezaka. Hivyo
tusipoweka jitihada binafsi tutajikuta tunaugua magonjwa haya” alisema Dkt.
Lutambi
Akisisitiza zaidi Dkt. Lutambi amesema
moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni
mabadiliko ya taratibu za kimaisha zinazohusisha matendo yanayoweza kusababisha
ugonjwa.
“Matumizi ya nyenzo za kufanyia
kazi au kutofanya mazoezi ya mwili huwafanya watu kulimbikiza nishati lishe
mwilini ambazo husababisha ongezeko la uzito wa mwili ambao uchangia kuongeza
uwezekano wa kupata magonjwa hayo". Dkt. Lutambi
Naye, Mganga Mkuu wa mkoa wa
Singida Dkt. Victorina Ludovick alisema lengo la Serikali kufanya mpango huu ni kutokana
na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hasa vifo vinavyotokana na
magonjwa haya.
Ameyataja magonjwa hayo ni pamoja
na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, mishipa ya fahamu, figo, saratani,
kifua sugu, kisukari, meno, macho, magonjwa ya akili na magonjwa ya kurithi
kama vile ugonjwa wa selimundu.
Alisema wiki hii itaambatana na kufanya
mazoezi ya viungo, huduma mbalimbali za afya zitatolewa ikiwa ni pamoja na
upimaji wa shinikizo la damu (presha), huduma za macho na meno, upimaji uzito
na urefu ili kuangalia uwiano wa urefu na uzito kama uko sahihi katika mwili.
Dkt. Ludovick ametoa wito kwa
wananchi wa mkoa wa Singida kushiriki kikamilifu katika mazoezi na huduma
zinazoendelea kutolewa katika viwanja hivyo vya bombardier katika wiki hi ili kupata
elimu na huduma mbalimbali za kiafya zinazotolewa bila malipo yoyote.
Uzinduzi rasmi wa Mpango huu kitaifa utafanyika Novemba 14, 2019 katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa
kuwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na kuhutubia umma, Mgeni Rasmi atazindua Nembo na Jina la Mpango, atakabidhi vitendea kazi maalum vya Mpango kwa ngazi ya Kituo cha Afya.
Pamoja na kuhutubia umma, Mgeni Rasmi atazindua Nembo na Jina la Mpango, atakabidhi vitendea kazi maalum vya Mpango kwa ngazi ya Kituo cha Afya.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi (wa nne kutoka kulia), Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick (wa tatu kutoka kulia) wakiwa katika moja ya mazoezi ya viungo ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCD) iliyofanyika leo Novemba 9, 2019 katika viwanja vya Bomberdia Manispaa ya Singida.
No comments:
Post a Comment