Wednesday, November 06, 2019

WAZIRI JAFFO APONGEZA MCHAKATO WA UCHAGUZI SINGIDA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Seleman Jaffo amewapongeza wakazi wa mkoa wa Singida kwa kuwa miongoni mwa mikoa mitano nchini iliyoonyesha hamasa na kujitokeza kwa wingi kitakwimu katika mchakato mzima wa zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la mpiga kura, ikiwa ni moja ya hatua muhimu kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea.
Jaffo aliyasema hayo Novemba 6, 2019 akiwa mkoani hapa, alipotembelea kukagua utekelezaji wa kanuni na taratibu za mchakato wa uchaguzi huo unavyoendelea hatua kwa hatua.
“Katika zoezi la uandikishaji Singida ni miongoni mwa mikoa mitano iliyofanya vizuri sana, na kwa wagombea tayari kwa mfululizo wa siku saba tumekamilisha zoezi la kuchukua na kurudisha fomu na hatimaye kufanya teuzi kwa wenyeviti na wajumbe wa kamati za rufaa,” alisema
Alisema, hali halisi iliyopo mpaka jana ni kwamba jumla ya kata 3956 zilizopo nchi nzima, kimantiki zoezi zima linakwenda vizuri, ingawa kuna baadhi ya maeneo machache zimejitokeza changamoto ikiwemo baadhi ya maeneo wagombea hawakupata fomu kwa wakati.
Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Songwe (Vwawa), Arusha (Arumeru), Mwanza na Kilimanjaro (Moshi), huku akizitaka kamati zote za rufaa nchi nzima kuhakikisha wakati wa maamuzi wanasimamia haki na usawa, kwa mujibu kanuni, taratibu na miongozo iliyopo bila ya kumuonea mtu yeyote.
“Azma yetu sote ni kuona uchaguzi huu unakwenda vizuri na unakamilika vizuri…kwa lengo mahususi la kuunda mamlaka za Serikali za mitaa ambazo zinakwenda kujibu matatizo makubwa ya wananchi,” alisema
Aidha, Jaffo alibainisha umuhimu wa zoezi linaloendelea kwa sasa kuwa, uchaguzi huo unakwenda kutengeneza Serikali za mitaa zilizo karibu zaidi na wananchi, ambazo taifa likitoka na ajenda zozote zile za maendeleo basi utekelezaji na msingi wa maendeleo utatoka chini.
Alisema, ifahamike kwa wananchi wote kuwa, kwa mujibu wa kanuni zilizopo, ‘Kamati ya Rufaa ya Wilaya’ inaundwa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ambaye ndiye mwenyekiti, akisaidiwa na wajumbe ambao ni watumishi 4 wa sekta za umma kutoka wilaya zote ndani ya mkoa, huku Katibu wa kamati naye atatoka ndani ya sekta ya umma lakini yeye tofauti na wenzake, ataruhusiwa kupiga kura.
“Mwenyekiti nendeni mkazingatie haki, sikilizeni rufaa na malalamiko yote yatakayoletwa mezani kutoka vyama vyote, na watu wote kwa uhuru na upana wake bila kuingiliwa na mtu yeyote,” alisisitiza Jaffo mbele ya wajumbe wa kamati ya rufaa mkoani hapa, na kuongeza;
“Mmepewa rungu lisilokuwa na mashaka…tendeni haki msiogope hakikisheni kila kitu kinanyooka, kama kuna mtu anastahili haki mpeni haki yake na kama kuna kasoro zozote rekebisheni.”
Zaidi, alilitaka Jeshi la Polisi kupitia Makamanda wa mikoa kuendelea kusimamia utaratibu uliowekwa kwa misingi ya Amani, na kamwe mtu yeyote asijitokeze kuchafua mchakato wa uchaguzi unaoendelea kwa maslahi yake binafsi.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya wilaya ya Singida DC mkoani hapa, Wilson Shimo, alisema kwamba wamejipanga vizuri kusikiliza malalamiko na rufaa zote kwa haki na kurekebisha kwa mujibu wa kanuni zinazowaongoza, huku akiweka wazi kuwa mpaka jana bado walikuwa hawajapokea malalamiko yoyote.
Aidha, Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Patrick Zamba, alisema watajitahidi kutoa maamuzi sahihi kwa muda mwafaka kwa mujibu wa sheria na kanuni, kulingana na kutoridhishwa kwao na maamuzi ambayo yamefanyika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, alisema siku zote ‘siku njema daima huonekana asubuhi’ na kwamba hatua ya mkoa huo kupokea hati ya ushindi na kuwa miongoni mwa mikoa 5 bora ni ishara njema.
“Singida ni njema…tena ni njema….na ni njema sana!…na asubuhi hii njema ndio itabeba mchana wote kuwa mwema zaidi, kwa hatua zote mpaka kukamilika kwa mchakato mzima wa uchaguzi huu muhimu,” alisema

MATUKIO KATIKA PICHA
  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe Seleman Jaffo, akisisitiza jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Rufaa ya Wilaya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Singida wakati alipotembelea kukagua utekelezaji wa kanuni na taratibu za mchakato wa uchaguzi unavyoendelea hatua kwa hatua hapa nchini.Mkutano ukiendelea.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe Seleman Jaffo, akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Rufaa ya Wilaya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Singida wakati alipotembelea kukagua utekelezaji wa kanuni na taratibu za mchakato wa uchaguzi unavyoendelea hatua kwa hatua hapa nchini.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akisikiliza kwa makini hotuba ya Waziri wa OR-TAMISEMI, Seleman Jaffo, wakati wa mkutano huo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike akisikiliza kwa makini hotuba ya Waziri wa OR-TAMISEMI, Seleman Jaffo, wakati wa mkutano huo.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza wakati wa mkutano huo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe Seleman Jaffo, akipokea shukrani za Serikali ya mkoa wa Singida kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Singida DKt. Rehema Nchimbi (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akifurahia jambo wakati wa mkutano huo.

Kwa habari zaidi tembelea tovuti: www.singida.go.tz

No comments:

Post a comment