Thursday, May 11, 2017

TASAF YATUMIA ZAIDI YA MILIONI 400 KUJENGA ZAHANATI MKOANI SINGIDA.



Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akipata maelezo katika chumba cha kujifungulia akina mama wajawazito katika zahanati ya kijiji cha Mwahango iliyojengwa kupitia TASAF 111 na ushiriki wa wananchi wa kijiji hicho mara baada ya kuizindua.
 
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akipima uzito katika zahanati ya kijiji cha Mwahango iliyojengwa kupitia TASAF 111 na ushiriki wa wananchi wa kijiji hicho mara baada ya kuizindua.




Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) Mkoa wa Singida umetumia zaidi ya shilingi milioni 430.3 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa zahanati nne katika halmashauri za wilaya ya Ikungi, Mkalama, Singida vijijini na Manispaa ya Singida.

Fedha hizo pia zimegharamia ujenzi wa nyumba mbili (two in one) za kuishi walimu katika shule ya msingi Chikombo wilaya ya Manyoni na shule ya Msansao iliyopo wilaya ya Iramba.

Ujenzi wa miundombinu hiyo kupitia TASAF 111 kipengele cha ujenzi wa miundombinu maalumu umefanyika kati ya Septemba 2014 na machi mwaka huu.

Hayo yamesemwa jana na mratibu wa TASAF mkoa wa Singida Patrick Kasango wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mwahango kata ya Ilongero halmashauri ya wilaya ya Singida.

Amesema wananchi wa vijiji ambapo miradi hiyo inatekelezwa wamechangia zaidi ya shilingi milioni 61.6 kwa kuchangia nguvu zao kwa kusomba michanga, maji na kuchimba msingi wa majengo hayo.

Kasango amesema kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo kulifanyika tathimini na uhakiki ili kubaini hali halisi ya uhitaji wa huduma halisi.

“Pia lengo ni kujiridhisha kwamba miradi hiyo kama itaweza kusaidia walengwa kutimiza masharti ya elimu bora na afya katika mpango wa kunusuru kaya maskini, katika halmashauri sita mkoani kwetu”, amesema.

Kasango ameongeza kuwa kati ya septemba 2014 hadi machi mwaka huu TASAF 111 Mkoa wa Singida imetumia fedha zingine zaidi ya shilingi bilioni 23.1 kugharamia utekelezaji wa kipengele cha uhawilisha fedha (conditional cash Transfer) ambapo kaya 38,984 za vijiji 277 kutoka halmashauri sita zimenufaika na fedha hizo.

Aidha amesema katika programu ya kutoa ajira za muda kwa kaya maskini, zaidi ya shilingi bilioni 2.7 zimelipwa kwa kaya zilizofanya kazi za muda, ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya maji, na upandaji miti.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa Zahanati ya Mwahango Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametumia fursa hiyo kuuomba uongozi wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) makao makuu kusaidia ujenzi wa nyumba kubwa (two in one) katika zahanati hiyo.

“Binafsi na kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Singida  naishukru sana TASAF 111 kwa kufanya mambo makubwa na umekuwa mkombozi  kwa wananchi kiuchumi. Mkurungezi TASAF makao mkuu usichoke kutusaidia, wananchi wa kijiji cha Mwahango wapo tayari kushiriki ujenzi wa nyumba ya watumishi, na wewe nakuomba uwaunge mkono kadri uwezo utakapokuruhusu”, amesema Dkt. Nchimbi.

Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa wananchi wa Mwahando wanapaswa kuitunza zahanati hiyo kwa kutumia huduma zinazopatikana hapo ili manufaa yake yaonekane pia waitunze kwa kupanda miti eneo la zahanati ili kutunza mazingira.

Aidha ameahidi pikipiki itakayosaidia utoaji wa huduma katika zahanati hiyo huku akitoa shilingi laki tano ili ujenzi wa nyumba ya watumishi wa zahanati uanze mara moja na kuwezesha zahanati hiyo kutoa huduma kwa masaa 24.

Awali Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mwahango Leonard Muna amesema jumla ya wakazi 2,776 wa kijiji hicho watanufaika na huduma za afya zitakazotolewa kwenye zahanati hiyo mpya.

“Kukamilika kwa zahanati kutasaidia wanakijiji kupata huduma za kiafya kwa karibu zaidi na hasa akina mama na watoto. Pia mradi utasaidia kuinua uchumi/kipato cha wanajamii kwa vile kupunguza muda wa kufuata huduma za afya na kupata muda mrefu wa kuzalisha huku afya zikiimarika ”, amesema Muna.

Amesema hapo awali wananchi wamekuwa wakifuata huduma za afya katika zahanati ya Ilongero zaidi ya kilomita tano ambapo shida kubwa walikuwa wakiipata hasa kwa kuwapeleka wajawazito kwa kuwabeba kwenye vitanda na mikokoteni kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika kijijini hapo.


Mratibu TASAF Mkoa wa Singida Patrick Girigo Kasango akito taarifa ya Mkoa ya Miradi ya TASAF katika hafla ya uzinduzi wa zahanati hiyo iliyojengwa kwa msaada wa TASAF 111 na wananchi wa kijiji hicho.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizindua jengo la zahanati ya kijiji cha Mwahango iliyojengwa na TASAF 111 na ushiriki wa wananchi wa kijiji hicho kilichopo wilaya ya Singida, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Singida Eliya Digha.

Jengo la zahanati ya Mwahango lililopo halmasahuri ya wilaya ya Singida iliyojengwa kwa msaada wa TASAF 111 na wananchi wa kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment