Wakizungumza na mwanahabari wa habari hizi leo tarehe 28 Septemba, 2023, muda mfupi baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, Abdalla Shaib Kaim kukagua jengo la Zahanati hiyo na nyaraka mbalimbali na uwekaji wa jiwe la msingi wamesema kuwa kitawapunguzia adha ya kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma ya matibabu.
Moja wa wananchi aliyeeleza furaha yake kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Bi. Agnes Mnyambeyu amesema kuwa kitendo cha Serikali ya awamu ya sita kutekeleza mradi wa ujenzi wa Zahanati katika eneo hilo ni kuwarahisishia huduma za afya hususani kwa akina mama wajawazito na watoto.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Jomson Mhagama, akitoa taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa amesema kuwa mradi wa Zahanati hiyo itasaidia kusogeza huduma ya afya kwa akina mama na watoto pamoja na wananchi wote wa kijiji hicho na jirani.
Amesema kuwa mradi huo lengo lake kubwa ni kusogeza huduma ya mama na mtoto pamoja na wananchi wa kijiji hicho wapatao 2526 na kupunguza idadi ya vifo kutokana na ajari zinazotokea mara kwa mara katika mlima salanda.
Aidha amesema kuwa mradi huo mpaka ukamilike utatumia kiasi cha shilingi Milioni 77.6 ambazo zimetokana na nguvu ya wananchi, mfuko wa Jimbo, Serikali Kuu na Halmashauri.
Katika hatua nyingine Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru imeweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Manyoni-Masigati-Hika kwa kiwango cha lami nyepesi yenye urefu wa mita 700.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mhandisi Stephen Nyanda akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaib Kaim, amesema kuwa lengo kubwa ni kuboresha hali ya usafiri na usafirishaji katika mji wa Manyoni pamoja na kukuza uchumi wa wananchi kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji ndani ya Wilaya hiyo.
Aidha, amesema kuwa hadi mradi huo muhimu kukamilika utagharimu zaidi ya kiasi cha Shilingi Milioni 489 ambazo zinatoka Serikali Kuu.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Utunzaji wa Mazingira (RUWASA) katika Halmashauri hiyo, Gabriel Ngongi amefafanua kuwa mradi wa chanzo cha maji Kaloleni kinalenga kuwahudumia wakazi wapatao 5271 waliopo katika mtaa mitaa ya Ujasiriamali, Mwanzi, Mitoo ya chini, Kaloleni na Samaria.
Amesema kuwa mradi huo utasaidia kuwapatia wananchi wa mitaa hiyo maji safi na salama na kuwawezesha kuwa na afya bora kutokana na utumiaji wa maji yenye uhakika ambayo yatakuwa yanaviwango vya ubora badala ya kutumia maji ambayo hayana ubora na viwango ambayo uweza kusababisha magonjwa ya tumbo.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim amewataka wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuhakikisha inatunza miradi hiyo na kuitumia kwa makusudi yaliyopendekezwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Kemirembe Lwota, akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye shamrashara za Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 amewasihi wananchi hao kuiunga mkono Serikali ya awamu ya Sita kwa kuitunza miradi hiyo kwa manufaa ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Aidha, katika Halmashauri ya Manyoni jumla ya miradi 7 imetembelewa, imekaguliwa na kuwekwa jiwe la Msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 1.7 zimetumika katika kutekeleza miradi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida anatarajia kukabidhi Mwenge wa Uhuru 2023 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kesho tarehe 29.9.2023 hafla itakayofanyika katika Kijiji cha Bahi Wilaya ya Bahi kuanzia saa 12.00 asubuhi.
No comments:
Post a Comment