Taasisi za kifedha za Kanda ya Kati na mashariki zikiwemo Benki zimeshauriwa kupunguza riba katika mikopo ya Kilimo kufikia asilimia tisa (9) au chini ya hapo ili kuendelea kuwasaidia wakulima waweze kufaidika na mikopo ya Kilimo na shughuli za kilimo kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, wakati akifungua Mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya kujadili namna ya utunzaji wa mazingira (Kijanisha Maisha) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa Katoliki uliopo mjini Singida chini ya Shirika la Kilimo la PASS.
RC Serukamba ameeleza kwamba kwa kupunguza riba katika mikopo ya kilimo ni kuunga mkono maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan hadi asilimia tisa hivyo akatumia fursa hiyo kuzipongeza benki ambazo zimefuata agizo hilo.
Aidha Serukamba amewaomba wadau wa kilimo kuendelea kufanya shughuli za uzalishaji kwa kuzingatia kanuni za ukuaji wa kijani shirikishi kama ambavyo PASS Trust wanavyoshauri lengo likiwa ni kuongeza utunzaji wa mazingira na kuzalisha kwa tija.
Hata hivyo RC amelipongeza Shirika la Pass Trust kwa ubunifu ambao wameendelea kuchukua katika kukabiliana na changamoto za wakulima katika mnyororo wa thamani.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Shirika hilo Herimani Bashiri amesema Shirika limepata mafanikio makubwa kupitia udhamini wanaoufanya katika miradi ya kilimo ufugaji na misitu pamoja na biashara kupitia mnyororo wa thamani katika kilimo.
Bashiri amesema kwamba Shirika la PASS limetoa ajira kwa watu Milioni 2.7 kati yao wanawake wakiwa ni zaidi ya laki 3.4 na wengi wao wakiwa ni vijana.
Aidha ameeleza kwamba Shirika kwa sasa lina vituo atamizi katika eneo la Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) Morogoro na Dodoma ambapo vijana wanajifunza mambo mbalimbali ya kilimo ufugaji na misitu.
No comments:
Post a Comment