Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amewagiza Watumishi wa Sekta ya Afya kujituma na kuongeza juhudi katika kazi bila kujali uchache walionao katika vituo vya Afya na Zahanati ili kuwapatia huduma stahiki wananchi wa Mkoa huo.
Hayo ameyasema jana tarehe 30/03/2023 wakati wa Kikao baina yake na watumishi pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe.
RAS amesema hategemei kusikia malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi kuhusu utoaji wa huduma za afya usioridhisha kwa kisingizio kwamba kuna uhaba wa watumishi kwa kuwa kazi ya utabibu ni wito.
Amewasihi kuwa na lugha nzuri kwa wateja wao wakati wanapotoa matibabu kwa kuwa lugha zisizo na staha ndizo zinazochangia kuharibu taswira ya sekta hiyo huku akisistiza watumishi hao kuacha kutumia vilevi wakati wa kazi.
Aidha amebainisha kwamba hategemei kusikia kwamba kuna kituo cha afya au Zahanati ambayo dawa zimeharibika au hazipo kwakuwa zipo taratibu za kufuata kuhakikisha madawa yanapaitikana kwa wakati na stahiki.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Maghembe amewataka wataalamu hao kutumia mafunzo wanayoyapata kutatua changamoto za kiafya za wananchi.
Amesema amewataka kufanya kazi kwa umoja na kuheshimiana huku akibainisha kila mtu kuhakikisha kwamba wanaendelea kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe akizungumza wakati wa kikao hicho.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick akizungumza wakati wa kikao hicho.
No comments:
Post a Comment