Saturday, August 06, 2022

Waziri Mkuu Majaliwa aridhishwa na Utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi Jengo la Halmashauri ya Singida Vijijini.

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akiweka jiwe la msingi Mradi wa Ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Singida Vijijini

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa  ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Singida Vijijini lililopo Kata ya Ilongero  ambako limegharimu kiasi cha fedha Tsh. Bilioni 2.7 ambapo ameagiza jengo hilo kukamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma inayostahili.

Waziri Mkuu ameyasema hayo hivi karibuni baada ya kuweka jiwe la msingi katika jengo hilo na kufafanua kwamba Ujenzi huo unalingana na kiasi cha fedha kilichotumika ambapo aliwapongeza viongozi walioweza kulisimamia.

Amesema jengo hilo ni miongoni mwa majengo ambayo yamekuwa yakitolewa fedha nyingi na Serikali ili kuwasaidia wananchi kupata huduma.

Katika Ujenzi huo kiasi cha fedha Tsh.700 zilizobaki Waziri Mkuu ameahidi kwamba zitakuja ili zitumike katika umaliziaji na Ujenzi wa uzio kwa ajili ya usalama wa Ofisi hiyo.

Hata hivyo Waziri Mkuu amempongeza Mkurugenzi wa Singida DC Ester Chaula kwa usimamizi wake katika kazi za Serikali huku akimtaka kuendelea kuwasimamia wagavi katika kununua vifa vya ujenzi kama alivyofanya awali.

Hata hivyo amewataka Watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na kuwafuata wananchi vijijini ili kuwapa huduma na kuwaeleza fursa ambazo Serikali imekuwa ikizitoa.

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akizungumza na baadhi ya wananchi wa Singida Vijijini mara baada ya uwekaji jiwe la msingi Mradi wa Ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Singida Vijijini


Amesisitiza nidhamu katika kazi kwa Watumishi na viongozi wao kwa kuwa kufanya hivyo itakuwa ni chanzo cha mafanikio.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amesema Serikali imeleta miradi mingi Mkoani hapo ambayo inatumia kiasi kikubwa cha fedha hivyo ameahidi kuzisimamia na kuhakikisha thamani yake ina onekana.

Aidha amewataka wananchi wa Singida kuitunza miradi hiyo ikiwemo miradi ya maji elimu na Barabara ambazo fedha nyingi zimetolewa na Serikali na kwa kufanya hivyo utaweza kuwasaidia watu wengi zaidi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kulia) akizungumza na wananchi wa Singida vijijini wakati wa ziara ya uwekaji jiwe la msingi jengo la ofisi ya Halmashauri.


Serukamba ameendelea kuwaeleza wananchi wa Ilongero dhamira yake ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na Bima ya Afya ambayo itarahisisha kupata huduma za Afya kwa kila mwananchi.

Ziara ya Waziri Mkuu ililenga kukagua miradi mbalimbali ikiwemo jengo la ofisi ya Halmashauri ya Ilongero na upanuzi wa Hospitali ya rufaa ya Mandewa iliyopo Manispaa ya Singida.

Muonekano wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Singida Vijijini ambalo limewekewa jiwe la msingi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Singida Agosti 6, 2022. 

No comments:

Post a Comment