WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia Watumishi wote katika Halmashauri za Mkoa wa Singida ambao walikusanya fedha za mapato lakini hawakuzipeleka benki wanazirudisha haraka.
Ametoa agizo
hilo leo kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkoani hapa
wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Singida, Ikungi na
Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Alisema kumekuwa
na tatizo kubwa kwenye Halmashauri nyingi nchini katika ukusanyaji wa mapato ya
ndani ambapo baadhi ya Watumishi wanapokusanya fedha haziingizwi kwenye mfumo
wa Serikali jambo ambalo limekuwa kero kubwa.
"Wakuu
wa Wilaya hakikisheni Watumishi wanaodaiwa fedha wazirudishe haraka, Iramba, Manyoni
na hata Ilongero (Halmashauri ya Wilaya ya Singida) nimepewa orodha ya Watumishi
ambao wanadaiwa fedha za makusanyo," alisema.
Majaliwa
alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza suala la ukusanyaji wa
mapato na hata majuzi wakati anawaapisha wakuu wa mikoa lakini cha kushangaza
baadhi ya Watumishi wa umma wamegeuka kuwa wabadhirifu.
Alisema ujanja
unaofanywa na baadhi ya Watumishi kufuja fedha za makusanyo ni kwamba
wanapokusanya fedha hasa wanapobaini ni nyingi wanazima mashine ili zisiingie
kwenye mfumo wa Serikali.
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka Watumishi kuacha urasimu katika utendaji wa kazi kwani
mambo hayo ndio yanakaribisha vitendo vya rushwa chini.
Kuhusu idara
za manunuzi, alisema limekuwa ni tatizo kubwa ambapo Idara hizo zimekuwa
zikiweka makadirio makubwa ya bei za manunuzi ya vifaa vya ujenzi kwenye miradi
hususani inayotumia 'force account'.
Aliongeza
kuwa kwenye Halmashauri kumekuwa na tatizo kubwa la usimamizi wa miradi
inayotekelezwa na kwamba kuna umuhimu kwa Watumishi kuhakikisha suala hili
linapewa umuhimu wa juu.
Alisisitiza
suala la mahusiano kwa Watumishi wa Umma mahali pa kazi kwani kufanya hivyo
kutaboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi mkubwa katika kuwatumikia wananchi.
Aidha,
alizitaka Halmashauri kuratibu vizuri suala la wafanyabiashara wadogo maarufu
wamachinga ili wapewe maeneo ya kufanyia biashara zao bila usumbufu.
Awali Waziri
Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Ofisi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Singida linalojengwa Ilongero katika kijiji cha Mwahango kwa thamani
ya Sh. 2.7 bilioni.
Akizungumza
na wananchi wa eneo hilo, alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Singida, Ester Chaula, kuisimamia idara ya manunuzi ili ujenzi wa jengo hilo
uweze kukamilika na kuanza kutumika.
"Nimeridhishwa
na ujenzi unavyoendelea, DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) isimamie idara ya
manunuzi, wasikuvuruge, mkandarasi alipwe fedha zake, " alisema.
Akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida inayojengwa kwa Sh. bilioni 19.5 Waziri Mkuu, alisema ujenzi wa hospitali hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa huu na mikoa jirani.
MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA ZIARA
No comments:
Post a Comment