Mkoa wa Singida umetajwa kuwa na fursa kubwa ya kukuza uchumi wa viwanda, lakini bado unakabiliwa na changamoto ya uhaba wa malighafi unaosababisha baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji. Kauli hiyo imetolewa na Brigedia Jenerali Charles Ndiege wakati wa ziara ya mafunzo kwa vitendo ya washiriki wa kozi ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi waliotembelea viwanda mbalimbali mkoani humo.

Akizungumza baada ya kutembelea viwanda vya kuchakata alizeti na pamba, leo Januari 22,2025 Brigedia Jenerali Ndiege amesema changamoto kubwa iliyojitokeza ni viwanda kushindwa kufanya kazi kwa msimu mzima kutokana na utegemezi wa malighafi zinazotokana na kilimo cha mvua. Amesema hali hiyo huathiri mnyororo mzima wa maendeleo ya kiuchumi, kuanzia wakulima hadi wafanyakazi wa viwandani.
Amefafanua kuwa viwanda vinaposimama, ajira hupungua na mapato ya wananchi hushuka, hali inayodhoofisha mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa. Kwa mtazamo wake, uzalishaji wa viwanda hauwezi kuwa endelevu bila sera madhubuti zitakazohakikisha upatikanaji wa malighafi kwa uhakika na kwa wingi.

Brigedia Jenerali Ndiege amesisitiza kuwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya viwandani ni ajenda ya kimkakati kwa taifa, akibainisha kuwa masuala ya chakula na viwanda yanagusa moja kwa moja usalama wa taifa. Ameshauri kuimarishwa kwa kilimo cha tija, matumizi ya teknolojia na ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wakulima na wawekezaji wa viwanda.

Kwa upande wa washiriki wa kozi hiyo, Hawa Adam kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema ziara hiyo imewapa uelewa wa kina kuhusu mchango wa viwanda vya Singida katika kukuza uchumi wa taifa. Amesema viwanda hivyo vinatoa soko la uhakika kwa wakulima na hivyo kuboresha maisha yao kupitia kipato na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Ameongeza kuwa changamoto ya uzalishaji mdogo inaweza kutatuliwa kwa kutoa elimu zaidi kwa wakulima juu ya mbinu bora za kilimo ili kuongeza mavuno ya mazao yanayotumika kama malighafi viwandani, hatua itakayosaidia viwanda kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Aidha, Wawakilishi wa viwanda vya Biosustain Tanzania Limited na Mount Meru Millers Limited wameeleza kuwa uzalishaji mdogo wa pamba na alizeti bado ni changamoto kubwa, wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji. Wamesema kupitia elimu, motisha na ushirikiano na serikali, uzalishaji unaweza kuongezeka na kuwezesha viwanda kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi.

Ziara ya washiriki wa kozi ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi mkoani Singida ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo yanayolenga kuoanisha nadharia za darasani na utekelezaji wa sera, mipango na mikakati ya serikali katika mazingira halisi. Kupitia ziara hiyo, washiriki wanapata fursa ya kutathmini maendeleo ya viwanda, kilimo na uchumi kwa ujumla, pamoja na kubaini changamoto na fursa zilizopo kwa maendeleo endelevu ya taifa.
No comments:
Post a Comment