Wednesday, January 21, 2026

DKT.MGANGA AWAPIGA MSASA MAAFISA ELIMU KATA NAMNA YA KUBORESHA UFAULU MASHULENI

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewaagiza Maafisa Elimu Kata kuimarisha uwajibikaji, ubunifu na ufuatiliaji wa karibu katika usimamizi wa elimu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa. Ameyasema hayo wakati wa kikao kazi cha Maafisa Elimu Kata wa Mkoa wa Singida kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.


Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mganga amesema takwimu za ufaulu kwa miaka ya karibuni zimekuwa zikionesha mabadiliko ya kupanda na kushuka, hali inayoashiria changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji. Ameeleza kuwa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi yameendelea kuonesha ufaulu wa chini, jambo linalohitaji mikakati madhubuti, mbinu bunifu za ufundishaji na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika shule.

Ameeleza kuwa lengo la Mkoa wa Singida ni kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 81.21 mwaka 2025 hadi kufikia asilimia 95, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yanategemea kwa kiasi kikubwa uwajibikaji wa Maafisa Elimu Kata. Amesema viongozi hao wako karibu zaidi na shule, hivyo wana nafasi ya kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua stahiki kabla hazijaathiri matokeo ya wanafunzi.

Dkt. Mganga ameongeza kuwa jukumu la Maafisa Elimu Kata si kufundisha moja kwa moja, bali ni kuhakikisha walimu wanafundisha kwa ufanisi, wanazingatia mitaala, wanapata stahili zao kwa wakati na wanahamasishwa kufanya kazi kwa nidhamu na ari. Amesisitiza pia utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho kwa vitendo na kuendeleza utamaduni wa tathmini ya mara kwa mara ili kuleta maboresho endelevu katika shule za msingi na sekondari.

Aidha, Afisa Elimu mstaafu, Ndg. Hamisi Maulidi, amesema kikao kazi hicho kinalenga kuwajengea uwezo Maafisa Elimu Kata ili kuimarisha usimamizi wa elimu mkoani Singida. Amebainisha kuwa mafanikio ya Mkoa katika mitihani ya kitaifa yanategemea moja kwa moja weledi na ufanisi wa usimamizi wao katika ngazi ya kata.

Nao Maafisa hawakusita kueleza furaha yao kutokana na kikao kazi hicho, Bw. Benjamini Nikodemas, Afisa Elimu Kata ya Miganga amesema maelekezo yaliyotolewa yameongeza hamasa ya kufanya kazi kwa weledi zaidi, huku Afisa Elimu Kata ya Muhalala, Mwl. Fatina Rajabu, akieleza kuwa kikao hicho kimewapa motisha ya kuimarisha mbinu za usimamizi na kujifunza uzoefu bora ili kuongeza ufaulu mwaka 2026.

Kwa ujumla, kikao kazi hicho kimefanyika katika kipindi muhimu kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya mitihani ya Darasa la Nne, Darasa la Saba na Kidato cha Pili pamoja na tathmini ya Mtihani wa Kidato cha Nne, kikitoa fursa ya kufanya tathmini ya kina ya mafanikio na changamoto katika sekta ya elimu. Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mkoa wa Singida wa kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufaulu wa mitihani ya kitaifa kwa kuweka mkazo katika usimamizi wa karibu na utendaji unaozingatia matokeo.







KWA KUTAZAMA VIDEO YA KIKAO, TAZAMA VIDEO HAPA CHINI:




 



No comments:

Post a Comment