Thursday, December 02, 2021

Mtandao wa Barabara waboresha maisha ya wananchi Singida

Uwepo wa mitandao ya barabara kuu na za viunganishi mkoani Singida zimeongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi na kukuza uchumi wa mtu mmoja moja kutokana na biashara zinazofanyika baina ya wilaya na halmashauri mbalimbali.

Mkoa huo umetajwa kuwa na  mtandao wa barabara wenye urefu wa jumla ya  kilometa 1716.12  ambapo lami ni   Km 488.73 na changarawe ni  km  1,227.39

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akifungua kikao kazi cha 44 kilichohusu Bodi ya barabara ya Mkoa  ambacho kimefanyika leo Desemba 3, 2021 katika ukumbi wa mkoa huo  na kuhusisha wakala wa barabara (TANROAD), Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wabunge wa mkoa huo, Viongozi wa CCM mkoa, wenyeviti wa Halmashauri, wakurungezi watendaji, na wataalamu mbalimbali wa Serikali.

Akiongea katika kikao hicho RC. Mahenge amesema mifumo ya barabara iliyopo katika Mkoa huo umefungua fursa mbalimbali  za kiuchumi kwa kuwa imeendelea kuunganisha Mkoa na Mikoa mingine, miji na  maeneo ya kitalii pamoja na migodi ya madini.

“Mifumo ya barabara imekuwa kama mishipa ya damu ambayo ikisimama kila kitu kina simama, nawashukuru sana TANROAD na TARURA kwa kusaidia kuboresha barabara za lami na zile zenye kiwango cha changarawe” alisema RC. Mahenge.

Aidha akawaomba viongozi waliohudhuria kikao hicho kuhakikisha wanasaidia kusimamia ujenzi wa barabara zote zinazoendelea  katika maeneo mbalimbali mkoani hapo kwa kuwa fedha nyingi za barabara zinaendelea kuja.

Aidha Mkuu wa Mkoa akaendelea kuwakumbusha wakandarasi wote wanaoshughulika ujenzi wa barabara  kuhakikisha wanatekeleza kazi zao kwa muda walipewa kwa kuwa hatapenda kusikia sababu zozote zitakazosimamisha ujenzi huo.

Akiwakilisha taaraifa yake Meneja wa TANROAD Mkoa Mhandshi Erick Ng’walali amesema hali ya barabara  katika Mkoa wa Singida  inaridhisha  kwa kuwa  asilimia 63.1 ni barabara zenye hali nzuri, asilimia 27.6 ni hali ya wastani wakati asilimia 9.3 tu zina hali  mbaya.

Aidha Mhandisi Erick akafafanua kwamba bado wameendelea kufanya matengenezo katika baadhi ya barabara mkoani hapo  ambapo asilimia 32.7 zimekamilika  na asilimia 14.4 za fedha zimekwisha tumika.

Hata hivyo Mhandisi Erick akazitaja baadhi ya changamoto zikiwemo wizi wa vyuma na alama za barabarani ambapo amesema elimu na uhamasishaji vinahitajika katika maeneo mbalimbali ili kutunza alama hizo ambazo ni muhimu kwa watumiaji wa barabara.

Aidha akatumia muda huo kuwaonya baadhi ya watu wanaotumia vibaya hifadhi ya barabara ikiwemo kupasua mifereji ya maji, kujenga na kupitisha mifugo katika sehemu ambazo hazistahili.

Akitoa maadhimio ya kikao hicho Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko amesema ahadi zote zilizotolewa na viongozi wa juu kuhusiana na ukarabati na utengenezwaji wa barabara utaingizwa kwenye mpango na kuhakikisha  unatekelezwa na wananchi wanafaidika.

Aidha amewataka TANROAD na TARURA kuboresha barabara na madaraja yote yenye uhitaji huo ndani ya mkoa mzima ili kuondoa athari zinazoweza kutokea wakati wa mvua.

MATUKIO KATIKA PICHA



Mkuu wa Wilaya ya Singida  DC Mhandisi Pasikas Muragili akichangia mada kuhusu Ujenzi wa Barabara kutoka TRA mpaka Kinyeto wilayani humo wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika Disemba 2, 2021 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Murro akichangia mada wakati wa kikao hicho.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Juma Kilimba akichangia hoja mbalimbali wakati wa kikao hicho.

Wajumbe wa Bodi ya Barabara wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa na TANROAD na TARURA wakati wa Kikao hicho


Meneja wa TANROAD Mkoa wa Singida Mhandshi Erick Ng’walali akiwakilisha taaraifa  wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika Disemba 2, 2021 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa.

No comments:

Post a Comment