Friday, December 03, 2021

Singida yapokea mbegu 20,000 za Mkonge

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kulia) akipokea mbegu ya Mkonge kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Saddy Kambona kwa niaba ya wakulima wa mkoa huo.

Mkoa wa Singida umepokea  mbegu za mkonge miche 20,000 itakayogawiwa kwa wakulima wa wilaya ya Singida Vijijini ikiwa ni mpango wa kuongeza chanzo cha mapato kwa mkoa huo na wananchi kwa ujumla.

Akipokea mbegu hizo leo Desemba 3.2021 kutoka Bodi ya Mkonge Tanzania Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge amesema zao la mkonge ni utajiri mwingine ambao umeingia mkoani Singida na wataalamu wamekiri ardhi ya mkoa huo kustawisha mkonge ambao ni mrefu na haushambuliwi na magonjwa.

Amewataka wakulima mkoani hapo kulima mazao yanayovumilia ukame kama alizeti, mtama, mkonge na dengu kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa mvua kunyesha chini ya kiwango kwa mwaka huu.

Awali akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) Dkt. Mahenge akatumia muda huo  kuwaasa wananchi wote wa Singida kulima mazao yanayovumilia ukame na ya muda mfupi ili kukabiliana na hali ya hewa ya sasa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Mjini Mhanddisi Pasikas Muragili akabaniisha kwamba uzalishaji wa mkonge unafanyika  katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na unafanyika katika mapalio (mipaka ya mashamba) iliyopandwa mkonge na kuuchakata.

Amesema wakulima wilayani humo wameanzisha AMCOS inayofahamika kwa jina la Mpipiti katika kijiji cha Mpipiti ambao wana mashine 16 za kuchakata mkonge na kati ya hizo mashine 10 ni za wanachama  na sita ni za watu binafsi.

Aidha wilaya imeandaa mashamba yenye ukubwa wa ekari 100 ambapo ekari 50 ni kwa ajili ya waanzilishi wa zao hilo na 50 kwa ajili ya wakulima wengine wa wilaya hiyo alibainisha DC Muragili.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu  Bodi ya Mkonge  Saady Kambona wakati akikabizi  mbegu hizo amesema kuanzia sasa Singida inaingia kwenye mikoa mitatu ya uzalishaji wa mkonge ambayo ni Tanga, Morogoro na Singida.

Amesema zao la mkonge halina msimu  maalum muda wote linastawi hivyo  kuwaomba wakulima wa mkoa huo kutumia fursa hiyo hasa wakati huu ambapo mbegu zinagawiwa bure na serikali.

Kambona  amesema matumizi ya zao hilo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka  ambapo kwa sasa unatumika kutengeneza mbao kwa ajili ya kutengeneza thamani, sukari, nyuzi, kamba na kwenye magari.

Hata hivyo ameahidi  kuleta mbegu 165,000 za mkonge ambazo zitatosheleza katika mashamba yenye ukubwa wa ekari 100 zilizitengwa wilayani Singida Vijijini.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA



Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akiwapitisha wajumbe kwenye muhtasari wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) -Singida


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo (kushoto) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili, wakifuatilia taarifa mbalimbali wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) -Singida

Sekretarieti ya Mkoa wa Singida wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) -Singida

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Murro, akizungumza wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) -Singida

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba akizungumza wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) -Singida

Mbunge wa Singida Mashariki Mheshimiwa Miraji Mtaturu , akizungumza wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) -Singida

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) -Singida (Kulia kwake ) Katibu Tawala Mkoa Dorothy Mwaluko.

No comments:

Post a Comment