Saturday, December 04, 2021

Wananchi mkoani Singida watakiwa kulima mazao ya muda mfupi ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa


Wananchi mkoani Singida wametakiwa kutumia vizuri chakula walichonacho na kulima mazao ya muda mfupi yanayohitaji mvua kidogo yakiwemo alizeti, mtama, dengu na mkonge kwa kuwa utabiri wa hali ya hewa umeonesha kwamba kutakuwa na mvua chini ya wastani.

Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge  Desemba 3, 2021 alipokuwa anafungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Singida (RCC) iliyokutana katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa huo na kuwasistiza wakulima kupanda mazao ya muda mfupi.

Amewataka wakulima kuandaa mashamba na mbegu mapema ili mvua za kwanza zitumike kikamilifu kwa kupandia mazao na kuwataka maafisa kilimo kuhakisha wanaendelea kusimamia na kuwasaidia wakulima kupata ushauri sahihi kuhusiana na mbegu, mbolea  pamoja na matumizi.

Dkt. Mahenge amesema taarifa iliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa TMA hivi karibuni kwamba kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa mvua za msimu huu zitachelewa na zitakaponyesha zitakuwa chini ya kiwango, kutokana na sababu hizo inabidi kuchukua tahadhari ya kupambana na hali hiyo kwa kulima mazao ya muda mfupi lakini pia kutunza mazingira.

Dkt. Mahenge akawakumbusha viongozi mbalimbali kuendeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa alizeti ili kupunguza uhaba wa mafuta ya kula nchini na kuwafanya wakulima wa Mkoa wa Singida kulima kibiashara.

Amesema  kutokana na uhaba wa mvua kwa mazao ya biashara mkoa wa Singida hautaathirika kwa sababu mazao kama alizeti, korosho na mkonge ni mazao ambayo hayahitaji mvua kubwa hivyo kama wakulima watakosa  mazao ya chakula lakini watafanya biashara kupitia mazao hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Singida vijijini Mhe. Elia Digha akafafanua kwamba kupitia Madiwani walihamasisha wakulima wengi kulima alizeti kama mkakati wa kuongeza uzalishaji wa alizeti na kupunguza uhaba wa mafuta na mwitikio ulikuwa mkubwa lakini changamoto mbegu haitoshi.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilipatiwa mahitaji ya mbegu tani 195 kwa wilaya ya Singida vijijini lakini walizoahidi kutoa ni tani 76 na mpaka sasa tumepokea tani 12.8 jambo ambalo litawakwamisha wakulima.

Mwenyekiti Digha akaiomba wizara ya kilimo kupeleka mbegu hizo kwa wakulima ili mvua zikianza waweze kulima zao hilo ambalo limetajwa kuhitaji mvua kidogo.

Hata hivyo wakati wa kuzindua msimu wa kilimo katika wilaya ya Singida vijijini tuliwaahidi wananchi kwamba watakopeshwa mbegu halafu watalipa mwisho wa msimu baada ya mavuno kauli ambayo ndiyo ilikuwa ikizungumzwa na Serikali kupitia Wizara ya kilimo jambo ambao hatulioni likifanyika kwa wakulima wetu. Alibainisha Elia Digha.

Akitoa ufafanuzi katika changamoto ya mbegu ya alizeti Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Singida Beatus Choaji amesema mahitaji ya mbegu kwa mkoa mzima yalikuwa tani 1194 ambazo zilitakiwa kupandwa katika ekari 586,909 kwa mkoa mzima.

Choaji akabainisha kwamba mpaka kufikia Desemba 1, 2021 wilaya ya Singida vijijini ilipelekewa kiasi cha kilo 76.016 ambazo utaratibu wa kuzifikisha kwa wakulima umeendelea kutekelezwa.

Amesema kuhusiana na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kwa wakulima kutunza vyakula na kulima mazao yanayokomaa haraka na yanayotumia maji kidogo amesema wataalamu wa kilimo na viongozi mbalimbali watahakikisha wanafikisha taarifa hizo kwa wakulima ili wachukue hatua.

Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Singida Beatus Choaji akisisitiza jambo kuhusu mkakati wa Kilimo wakati wa kikao hicho.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akisisitiza jambo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. (Kulia kwake ) Katibu Tawala Mkoa Dorothy Mwaluko.

No comments:

Post a Comment