Wednesday, December 01, 2021

Mikataba 26 ya ujenzi wa barabara Singida yasainiwa

Mkuu wa Mkoa wa Singida  Dkt. Binilith Mahenge leo Desemba 1, 2021 ameshiriki utiaji wa saini katika mikataba 26 ya awamu ya pili baina ya Wakandarasi na Wakala wa barabara za vijijini  na mijini TARURA wa  mkoani hapo zenye thamani  ya Sh. Bilioni 12.6  ambazo zimetokana na makusanyo ya tozo za miamala ya simu.

Utiaji saini huo umefanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa pamoja na taasisi za kifedha zikiwemo benk ya CRDB, NMB na makampuni ya bima kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kuwakopesha Makandarasi hao.

Akiongea katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa akawataka Makandarasi waliopata kazi hizo za utengenezaji wa barabara katika Halmashauri saba (7) za Mkoa wa Singida akawataka kuhakikisha kwamba zinajengwa kwa viwango ili kulingana  na thamani ya fedha zinazotolewa.

Aidha RC Mahenge akawakumbusha Wakandarasi hao kutumia ratiba ya kazi vizuri na kukamilisha kazi kwa wakati huku akiwataka kutumia muda huu ambapo mvua sio nyingi kuanza na utekelezaji wa miradi kwa sababu hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Kwa kuwa fedha zinazotumika ni kodi za wananchi zinazotokana na makato kweye simu ni vizuri kila mmoja wenu afanye kazi kwa uzalendo kwa kuwa miradi yote inatekelezwa na makandarasi wazawa, tuhakikishe fedha zinatumika kulinga na kazi zinazofanyika”. alifafanua Dkt. Mahenge.

“Kupata mradi ni jambo moja na kutekeleza mradi ni jambo la pili, nafahamu wapo watu watatumia zaidi ya siku 14 walizopewa za kukusanya vitendea kazi kwa mambo mengine hivyo kusababisha ucheleweshaji wa kazi, hatutakuwa na msamaha kwa mkandarasi yeyote atakaye fanya kazi mbaya na atakayechelewesha kazi”. Aliendelea kusisitiza  Dkt. Mahenge.

Hata hivyo Dkt. Mahenge akatumia muda huo kuishukuru Serikali kwa kutoa Bilioni 12.6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini katika wilaya zote mkoani Singida na kukiri kwamba kwa kipindi kifupi kilichopita walipata Sh. Bilioni 27 za UVIKO 19 ambazo zililenga kwenye miradi ya maendeleo hivyo kwa kipindi kifupi Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali mkoani hapa.

Akimaliza hotuba yake RC Mahenge akawashukuru TARURA kwa jitihada zao za kufanikisha mchakato wa kuwapata Wakandarasi wenye sifa zinazukubalika hivyo kuwataka  wakala hao wa barabara za vijijini na mijini kuwasimamia ili waweze kukamilisha kazi kwa wakati na kwa kiwango kinacho stahili.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa Jumanne Kilimba akisisitiza jambo wakati wa hafla ya utiaji wa saini katika mikataba 26 ya awamu ya pili baina ya Wakandarasi na Wakala wa barabara za vijijini  na mijini TARURA iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa Jumanne Kilimba  amesema kupitia kamati ya siasa  watahakikisha wanakagua miradi hiyo kwa umakinifu mkubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata kile kilicho tarajiwa kufikishwa  na Serikali kwa lengo la  kuwanufaisha wakazi wa Mkoa wa Singida.

Hata hivyo amebainisha kwamba Wakandarasi hao wana uwezo mkubwa kwa kuwa wengi wao wameshafanya kazi mkoani hapo na kuwahakikishia kwamba wanaendelea kupata kazi mkoani hapo endapo watafanya vizuri na kuwakumbusha kwamba atakaye haribu Mkoa wa Singida asitegemee kupata kazi mkoa wowote.

Awali akieleza malengo ya hafla hiyo Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Tembo D.R amesema mikataba hiyo itatekelezwa katika Wilaya ya Iramba, Itigi, Singida DC, Manyoni Mkalama, Ikungi na Manispaa ya Singida.

Amesema makampuni yaliyopata kazi hizo ni M/S Kangwa General Supply Ltd, M/s J.P Trader Ltd, Chase Investment, Brand Mark, Kumba Quality, Sumaco Eng., Coyesa company, Gornad company na nyinginezo nyingi ambazo kwa mujibu wa mkataba wanatakiwa kumaliza kazi ndani ya miezi 6. Alifafanua Mhandisi Tembo.  

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akiwasisitiza Wakandarasi kuhusu kuzingatia ratiba na muda, viwango bora vya ujenzi wa barabara pamoja na uzaleondo katika ufanikishaji wa miradi hiyo mkoni Singida. 

 Zoezi la utiaji wa saini katika mikataba 26 ya awamu ya pili baina ya Wakandarasi na Wakala wa barabara za vijijini  na mijini TARURA mkoani Singida ukiendelea.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko wakati wa hafla fupi ya utiaji wa saini katika mikataba 26 ya awamu ya pili baina ya Wakandarasi na Wakala wa barabara za vijijini  na mijini TARURA iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida.

Baadhi ya Wakandarasi walioshiriki katika utiaji wa saini wakimsikilia Mkuu wa Mkoa wa Singida (hayupo picha) wakati wa hotuba yake.

No comments:

Post a Comment