Tuesday, November 16, 2021

Tumejipanga kuimarisha usalama wa chakula ndani ya mkoa – Dkt Binilith Mahenge.

Mkoa wa Singida unatarajia kuvuna  jumla ya tani 1,166,464.7 za mazao mbalimbali ya chakula yanayotarajiwa kulimwa kwenye hekta 585,744.9 katika msimu wa kilimo wa 2021/22 ndani ya  maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Singida.

Kauli hii imetolewa leo 16.05.2021 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge katika kikao kazi cha uzinduzi wa ugawaji wa mbegu kupitia mradi unaofadhiliwa na mfuko wa kimataifa  wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwenye Sekta ya Kilimo uliofanyika katika ukumbi wa Socia Holl uliopo mjini Singida,  ambapo amebainisha kwamba wakulima wamejiandaa ipasavyo katika msimu huu wa kilimo.


Akiwa katika uzinduzi huo Dkt. Mahenge amebainisha kwamba Mkoa unatarajia kupanda zao la mahindi katika eneo lenye ukubwa wa hekta 269, 175.6  ambapo matarajio ni kuvuna  tani 501,526.3 wakati mpunga ukilimwa katika eneo la hekta 23,584.4 na kuvunwa tani 70,187


Aidha  mazao mengine ni mtama uwele ulezi ngano mihogo viazi  vitamu na viazi mviringo ambavyo kwa jumla ya mazao yote  kutatumika  eneo lenye ekari 585,744.9 ambalo litatoa mavuno kiasi cha tani 1,166,464.7 alifafanua RC Mahenge.


Dkt. Mahenge amefafanua kwamba katika msimu huu wa kilimo mkoa unatarajia kulima mazao mbalimbali ya biashara  yakiwemo pamba korosho vitunguu alizeti karanga choroko na dengu  ambapo eneo litakalolimwa mazao haya ni hekta 352,510.7


Hata hivyo RC Mahenge akaendelea kufafanua kwamba katika msimu huu wa kilimo kwa upande wa  mazao ya biashara Mkoa unatarajia kutoa mavuno yapatayo tani 955,200.5 ambapo  wakulima na wananchi wa Singida watapata faida na kuongeza vipato na kuboresha maisha yao.


Awali akitoa takwimu za chakula  Mkuu wa Mkoa  amesema kwamba msimu wa mwaka jana eneo la Kilimo lilikuwa hekta 525 za mazao ya chakula zilizozalisha  tani 821,881.7 ambayo ni ongezeko lililotokana na kuongezeka kwa tija katika kilimo iliyosababishwa na wakulima kutumia kanuni bora za kilimo.


Matumizi ya pembejeo na  kanuni bora za kilimo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kusaidia kuimarisha usalama wa chakula kwa wananchi wa mkoa wa Singida. Alimalizia Dkt. Binilith Mahenge


Kikao hicho kiliwahusisha  Wizara ya Kilimo, wakuu wa Wilaya zinazolima alizeti, Makatibu Tawala  wa mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Manyara  pamoja na Shirika la kimataifa la Kilimo (IFAD).


No comments:

Post a Comment