Monday, August 02, 2021

Wanaume zaidi ya milioni tatu kutahiriwa ifikapo 2024 - Katibu Tawala Singida

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu akizungumza kwaniaba ya Katibu Tawala wa Singida

Serikali imeweka  malengo ya kutahiri wanaume wapatao 3,801,860 katika mikoa 17 ifikapoa mwaka 2024 lengo likiwa ni kuendeleza  jitihada za kupunguza maambukizi ya  ugonjwa wa VVU/UKIMWI.

Akiongea Kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida wakati wa kufungua kikao kazi  cha Uraghabishi wa  Mpango Endelevu wa Huduma za tohara kinga kwa mwanaume  kilichofanyika leo 02.08.2021 katika ukumbi wa Chuo  cha ufundi VETA Singida Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu amesema,  Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na wadau wengine, imeandaa Mpango Endelevu wa Huduma ya Tohara kwa Wanaume nchini .

Aidha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida kwaniaba ya Katibu Tawala amebainisha kwamba Mpango huo umejikita katika maeneo makuu manne ambayo ni uongozi, rasilimali watu, utoaji huduma na usimamizi wa ugavi ambapo  unabainisha malengo ya nchi na mikoa katika kutahiri wanaume.

Hata hivyo ameeleza kuwa huduma ya tohara kwa mwanaume inatolewa katika mikoa 17 ya kipaumbele ambayo ni  Geita, Iringa, Kagera, Katavi, Kigoma, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Songwe na Tabora.

Tanzania tulianza kutekeleza afua ya tohara kinga katika mikoa mitatu Kagera, Iringa na Mbeya kama majaribio  mwaka 2009. mwaka 2010 tulianza kutekeleza afua hii ya tohara kwa kujumuisha mikoa mingine yenye viwango vya juu vya maambukizi. Hivi sasa huduma ya tohara kwa mwanaume inatolewa katika mikoa 17” Alisema, Kiaratu.

Kwa upande mwingine Kiaratu amefafanua kwamba kutokana na jitihada za Serikali za kupunguza  maambukizi ya VVU nchini kiwango cha tohara kwa wanaume kimeongezeka kutoka asilimia 67.0 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 77.4 mwaka 2017, ambapo takwimu za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, unaonesha  zaidi ya wanaume milioni sita mpaka sasa wametahiriwa katika mikoa ya kipaumbele.

Hata hivyo Mstahiki Meya huyo kwaniaba ya Katibu Tawala Mkoa amewashukuru  wadau mbalimbali waliowezesha zoezi hili kufanikiwa wakiwemo Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria (Global Fund) na  Mashirika ya Umoja wa Mataifa hususan WHO, UNICEF na UNAIDS.

Kwa upande Dkt. Susan Mmbando Mratibu wa huduma endelevu ya tohara  kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika mpango wa taifa wa kudhibiti ukimwi amesema matokea ya tafiti yalithaibitisha kuwa tohara inapunguza uwezekano wa mwanaume kupata maambukizi ya VVU toka kwa mwanamke kwa asilimia sitini (60%).

Aidha Dkt. Susan amebainisha kwamba matumizi ya rasilimali watu, fedha na miundombinu iliyopo itumike ipasavyo ili kuwezesha utoaji wa huduma endelevu za Tohara kinga ya kitabibu.

Dkt. Susan ametoa wito  kujumuishwa kwa huduma za tohara kinga kwenye huduma nyingine zinazotolewa katika vituo vya huduma za afya na kuhakikisha miongozo inapatikana na  kutekelezwa ili kuhakikisha huduma za tohara zinaingizwa katika mpangokazi wa  kila Halmashauri.

Amesma ili kuongeza wigo ni muhimu kuongeza vituo vya kutolea huduma kutoka 339 – 4,900 ambapo kila Mkoa unatakiwa kuongeza asilimia 10 -20 ya vituo vyake.

No comments:

Post a Comment