Tuesday, August 03, 2021

Programu ya Mazingira kwa njia ya Kisiki hai yatua Singida- Dkt. Mahenge awataka viongozi wa Mkoa kutooneana aibu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewataka wananchi wa Mkoa huo kupanda na kutunza miti ili kulinda mazingira na kuyarejesha yaliyoharibika. Pia amewataka viongozi wote mkoani humo kutooneana aibua wakati wa kutekeleza majukumu hayo.

Dkt. Mahenge  amesema hayo leo 03.08.2021 wakati akifungua warsha ya siku nne ya mafunzo  kwa wawezeshaji wa programu ya ukombozi wa mazingira kwa njia ya kisiki hai  iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha ualimu mkoani Singida.

Mkuu wa Mkoa huyo amewataka  viongozi wa ngazi zote Mkoani hapo  kuhakikisha shughuli za Programu hii ya kutunza mazingira kupitia njia ya Kisiki Hai zinafanyika kikamilifu kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Aidha ameawakumbusha viongozi hao kusimamia  utungaji na utekelezaji wa sheria ndogo ambazo zitatumika kuwabana wale wote watakaokwenda kinyume na kampeni  ya kuboresha mazingira  kwa ujumla wake.

”Viongozi katika ngazi zote tusioneane aibu tunapotekeleza majukumu ya kiserikali. Tuwawajibishe kwa mujibu wa kanuni wale wote watakaokuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yetu tuliyokabidhiwa tuyasimamie. “ alisema Dkt Mahenge

Hata hivyo amesema  mradi huo umekuja wakti muafaka ambapo utasaidia kuokoa baadhi ya maeneo ambayo bado hayajaharibika kutokana na desturi ya kukata miti kwa ajili ya kuandaa mashamba, kupata miti ya kujengea nyumba au maboma ya mifugo, kupata nishati za kuni na mkaa, na kupata malisho ya mifugo.

Dkt. Mahenge anabainisha kwamba uharibifu huo wa mazingira unasababisha  maeneo mengi ya ardhi ya kilimo na malisho kuwa tupu na kukosa rutuba na kuathiri upatikanaji wa mvua na mavuno ya kutosha hivyo kuwataka maafisa kilimo wa ngazi zote, kusimamia mradi huo ili kuwasaidia  wakulima na wafugaji.

“Kwa kuwa mradi huu unawagusa wakulima moja kwa moja naomba ofisi zote za kilimo kuanzia ya Mkoa, za halamashauri za wilaya pamoja na maafisa ugani wa ngazi zote mkausimamie huu mradi kwa karibu ili ukawe na tija kwa wakulima wetu.” Alienedelea kusema Mkuu wa Mkoa.

Awali Dkt. Mahenge amelipongeza shirika la LEAD Foundation, kwa kuanzisha programu hiyo ya kutaka kuirejesha hali ya Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla kuwa ya kijani, na kuunga mkono jitihada za Serikali za kutunza mazingira.

Mkuu wa mkoa amefafanua  kwamba Serikali  kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imetilia mkazo suala la kutunza mazingira kwa kupanda miti ambapo tayari ilizindua  kampeni kubwa ya Kupanda miti mwanzoni mwa mwezi Juni 2021 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani.

Akimalizia hotuba yake Dkt Mahenge amesisitiza  Watanzania wote kushirikiana na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa juhudi zinafanyika  za kuboresha rutuba ya ardhi na kurudisha uoto wa asili kwenye mashamba na misitu ya hifadhi.

Naye Mkurugenzi wa miradi Bwana Njamasi Chiwanga  kutoka Shirika hilo amesema lengo ni kuhifadhi mazingira  kwa njia ya asili ambayo haitakuwa na changamoto kubwa kwenye utunzanji wa miti.

Mkurugenzi wa Programu ya Lead Foundation Njamasi Chiwanga wakati akiwasilisha mada

Amefafanua kwamba zimekuwepo changamoto za upandaji miti hasa katika maeneo makame hivyo shirika hilo limeamua kubuni njia ya uhifadhi wa mazingira kwa kuotesha uoto wa asili kwa njia ya kisiki hai.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akizungumza na Askofu Mstaafu, Dkt. Saimon Chiwanga, Mwanzilishi wa Lead Foundation

Picha ya pamoja katikati waliokaa ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge 


Imeandaliwa na

Afisa Habari

Ofisi ya Mkuu Mkuu wa Mkoa Singida.

No comments:

Post a Comment