Tuesday, August 10, 2021

Dkt. Mahenge awataka wakandarasi kumaliza miradi ya madaraja kabla msimu wa mvua haujafika.

Mkuu wa Mkoa Singida Mhe. Dkt. Binilith Mahenge akitoa maelekezo kwa meneja wa TANROAD Mhandisi Deus Masige  mkoa Singida baada ya kutembelea ujenzi wa daraja, pembeni ni Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Mfaume Kizigo

Mkuu wa Mkoa Singida Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amewataka TANROAD kumaliza haraka ujenzi wa daraja unaoendelea katika Kata ya Msingi Wilayani Mkalama mkoani hapa ili kurahisisha mawasiliano  katika maeneo mbalimbali  kabla msimu wa mvua haujaanza.

Dkt. Binilith Mahenge ametoa maelekezo hayo leo tarehe 10.08.2021 alipotembelea mradi wa ujenzi wa daraja lililopo   Kata ya Msingi wilaya ya Mkalama ambapo amesema daraja hilo likikamilika litaweza kuhudumia mikoa ya Mwanza, Simiyu na Manyara.

Aidha amewapongeza viongozi wa TANROAD mkoani hapo kwa usimamizi mzuri wa ujenzi huo na kuwataka kuhakikisha kwamba daraja linakamilika kwa ubora na muda uliopangwa.

Hata hivyo RC amebainisha kwamba kumalizika kwa ujenzi wa daraja hilo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 10.9 na linatakiwa kukamilika ifikapo tarehe 30.10.2021.

Aidha Mhe. Dkt. Mahenge amewapongeza Viongozi wa TANROAD  kwa usimamizi mzuri pamoja na changamoto za mvua kwa msimu uliopita lakini kazi imeendelea kuwa nzuri.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo kutahamasisha  kwa kiasi kikukbwa ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na  taifa kwa ujumla.

“Nimefahamishwa kwamba daraja hili linaunganisha mikoa ya Simyu, Mwanza, Manyara na kwa mkoa wa Singida linaunganisha Wilaya ya Mkalama na Iramba, ni matumaini yangu kwamba shughuli za uchumi zitaimarika sana kwa mtu mmoja na Taifa kwa ujumla wake” Alisema Dkt. Mahenge.

Awali akimkaribisha RC, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe.  Sophia Mfaume Kizigo amesema daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu cha wilaya ya Mkalama na Iramba litawasidia wananchi wa maeneo hayo kuendesha shughuli za kila siku kwa ufasaha kutoka eneo moja kwenda jingine.

Aidha ufanikishwaji wa daraja hilo utasababisha barabara nyingine zinazounga wilaya na mikoa mbalimbali kujengwa kwa kiwango cha lami alisistiza Mhe.  Sophia

Naye Diwani wa Kata ya Msingi wilayani hapo Mhe. Amri Juma  ameishukuru Serikali kwa jitihada za kufanikisha ujenzi wa daraja hilo na mengine madogo yanayojengwa na TARURA katika Kata hiyo kwamba ni ishara ya mabadiliko makubwa ya kiutendaji unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita.

Naye Mhandisi Deus Masige Meneja wa TANROAD mkoani Singida amesema daraja linaurefu wa mita 100 na midomo ya kupitisha maji  mnne (4)  ambapo limefikia asilimia 67 na linatumia fedha za ndani.

Ujenzi wa daraja hilo ulitegemewa kumalizika   tarehe 11/12/2020 lakini kutokana na changamoto za mvua kwa msimu uliopita halikuweza kumalizika kwa wakati.

Mwisho Mhandisi Masige amemhakikishia Mkuu wa mkoa kwamba pamoja na changamoto zilizojitokeza lakini ujenzi wa daraja hilo utakamilika ifikapo 30/10/2021.

Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amewataka wananchi wa Mkalama na maeneo mengine kujikinga na ungojwa wa Covid 19 na kuendelea kupata chanjo ambazo Serikali imeshazisambaza maeneo mbalimbali mkoani hapo.

Amesema Mkoa umepokea chacho Zaidi ya 30,000 ili wananchi waweze kupata  chanjo hizo ambazo Serikali imejiridhisha kwamba ni salama kwa afya ya watu wake.

Aidha Mhe. Dkt. Mahenge amewaagiza wakuu wa wilaya zote mkoani hapo kuendelea kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya korona kama sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Amewataka madiwani kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu misongamono ambayo sio ya lazima ili kuepuka usambazaji wa ugonjwa huo endapo mtu mmoja atakuwa ameathirika.

Naye Mzee Aroni Msindye Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapo ameiomba Serikali kusogeza karibu vituo vya kupatia chanjo ili wazee waweze kufika kwa urahisi.

Mzee Aroni amebainisha kwamba wazee kwa sasa wanapata changamoto ya umbali hivyo wengi kushindwa kupata chanjo hiyo.

Imeandaliwa na 

Afisa Habari

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida

http://singidars.blogspot.com/

 Matukio katika picha

Mkuu wa Mkoa Singida Mhe. Dkt. Binilith Mahenge akizungumza (kushoto) ni Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Mfaume Kizigo

Mkuu wa Mkoa Singida Mhe. Dkt. Binilith Mahenge akiwa na viongozi mbalimbali na waandishi wa habari  wakati wa ukaguzi wa  ujenzi wa daraja katika kata ya Msingi wilayani Mkalama mkoani Singida leo 10.8. 2021

Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Mfaume Kizigo (kulia) akizungumza wakati wa ukaguzi wa  ujenzi wa daraja katika kata ya Msingi wilayani Mkalama mkoani Singida leo 10.8. 2021


Muonekano wa ujenzi wa daraja katika kata ya Msingi 

Diwani wa Kata ya  msingi Mhe. Amri Juma akitoa shukrani kwa Serikali kwa niaba ya wananchi kutokana na ujenzi wa daraja hilo.

Imeandaliwa na 

Afisa Habari

Mkuu wa Mkoa Singida

www.singida.go.tz/new

No comments:

Post a Comment