Tuesday, August 17, 2021

CCM SINGIDA YATAKA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO KUIMARIKA.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Mhe.  Juma Kilimba amewataka viongozi wa miradi mbalimbali mkoani hapo kuongeza juhudi katika usimamizi  wa miradi wanayoitekeleza ili kulinda thamani ya fedha za Serikali  zinazotumika kukamilisha  miradi hiyo.

Akiongea leo tarehe 16/8/2021 wakati wa kuhitimisha ziara yake  kwa wilaya ya Iramba katika ukumbi wa Halmashauri hiyo  Mhe. Kilimba  amewapongeza viongozi hao kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi na  kuwataka kushughulikia baadhi ya changamoto ndogo ndogo walizozibaini  katika  miradi sita waliyoitembelea.

Miradi iliyotembelewa na Mwenyekiti wa CCM mkoa ni ile inayohusiana na ukarabati na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Tumaini, ujenzi wa darasa moja  katika shule ya msingi  Ulyang’ombe,  ujenzi wa zahanati moja (OPD),  Matengenezo ya barabara  kutoka Shelui  kupita  Mtoa hadi Ndago, mradi mwingine ni ule wa  umeme wa ujazilizi  katika vitongoji vya Pangani na Kintende pamoja na mradi wa miche ya miti katika eneo la Lulumba.

Ujenzi wa Hospitali kata ya Mkunda  iliyogharimu shilingi milioni 50, umaliziaji wa chumba cha darasa katika shule ya msingi Ulyango’ombe, ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 30.74 inayogharimu kiasi cha milioni 199.9, mradi wa umeme na ujenzi wa mabweni  katika shule ya sekondari Tumaini na mradi wa huduma za misitu ni miradi ambayo imekuwa na faida kubwa kwa wananchi wa Iramba, tuhakikishe inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyotarajiwa na Serikali.” Alisema Juma Kilimba

Amewataka viongozi wanaosimamia miradi hiyo  kuongeza umakinifu  katika usimamizi wa miradi pamoja matumizi sahihi ya fedha za Serikali  ili kufikia lengo la kuwasogezea huduma wananchi kwa ukaribu.

Aidha, Mhe, Juma amewapongeza wanachi wa wilaya ya Iramba kwa kujitokeza kwa hali na mali katika kuchangia ujenzi wa hospitali na shule mbalimbali wilayani hapo na kuwataka wananchi wa wilaya za jirani kuiga ushiriki wa shughuli za maendeleo badala ya kuiachia Serikali .

Mkandarasi wa kampuni ya M/S chase investment group ltd ya mkoani Mwanza inayosimamia ujenzi wa barabara hiyo,  amesema ujenzi umegharimu kiasi cha shilingi 199,917,000 ikihusisha kuchonga barabara km 30,74 Kuweka changarawe km 13, ukarabati  wa makalavati saba (7) na ujenzi wa makalavati mapya  mawili  (2) pamoja na kuchimba mifereji ya maji ya mvua  yenye urefu wa mita  2694.5.

Ziara hiyo wilayani Iramba imewahusisha baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa, RC ambaye aliwakilishwa na DC Mhe. Paskasi Muragili pamoja na DC wa  Iramba Mhe. Suleimani Mwenda na wakuu wa Idara mbalimbali.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Mhe.  Juma Kilimba (kulia) akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo



 Baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Singida wakiwa katika Mradi wa miche ya miti katika eneo la Lulumba

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Singida wakiwa katika Mradi wa ujenzi wa mabweni  katika shule ya sekondari Tumaini 

No comments:

Post a Comment