Monday, August 19, 2019

MWENGE WA UHURU 2019 WAPOKELEWA KWA KISHINDO MKOANI SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akipokea Mwenge wa Uhuru 2019 kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge

Serikali ya mkoa wa Singida inayoongozwa na mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi, kwa kushirikiana na wananchi wa Singida, mapema leo 19/08/2019 wameupokewa Mwenge wa Uhuru ukitokea mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema, Mwenge wa Uhuru 2019, Katika Mkoa wa Singida utakimbizwa kwa muda wa siku 7 katika Halmashauri 7 kwa kuanzia na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni leo tarehe 19 Agosti, 2019 na utahitimisha mbio zake mnamo tarehe 25 Agosti, 2019 na tarehe 26 Agosti, 2019 utakabidhiwa mkoani Tabora.

Dkt. Nchimbi amesema kuwa, katika Mkoa wa Singida Mwenge wa Uhuru utakimbizwa jumla ya Kilometa 804.8, utapitia jumla ya miradi 46 inayohusu Sekta za Elimu, Afya, Mazingira, Maji, Utawala Bora, Kilimo, Ushirika, Biashara, na Programu za mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya, Malaria, Rushwa, Elimu ya Mpiga kura na UKIMWI.

Amesema, Miradi 12 itazinduliwa ambapo miradi 2 itafanyiwa ufunguzi, miradi 10 itawekwa jiwe la msingi na miradi 22 itakaguliwa na kutembelewa. Miradi yote itakayopitiwa itakuwa na thamani ya Shilingi za Kitanzania 9,462,470,874/=.

Aidha, Dkt. Nchimbi amemhakikishia mkimbiza Mwenge wa Uhuru 2019 Kitaifa Ndugu Mzee Mkongea Ali, kuwa Serikali ya Mkoa wa Singida imejipanga vema katika kuhakikisha inatokomeza na kumaliza kabisa mizizi ya Rushwa, Madawa ya Kulevya, UKIMWI na Malaria kwa kutambua na kupokea Ujumbe mwambatano wa Mapambano dhidi ya Rushwa, chini ya kaulimbiu, “Kataa Rushwa Jenga Tanzania”.

Pia, Mapambano dhidi ya Dawa za kulevya, chini ya kaulimbiu “Shiriki kutokomeza Malaria kwa manufaa ya jamii”. Mapambano dhidi ya UKIMWI chini ya kaulimbiu “Mwananchi Jitambue, Pima afya yako sasa”.

“ Napenda kuwakaribisha rasmi Mkoani Singida vijana wetu wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2019 Kitaifa” Dkt. Nchimbi

Awali, Dkt. Nchimbi, kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Singida pamoja na wananchi wote, alianza kwa kutoa salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  na Serikali ya Awamu ya Tano kwa moyo wa upendo, kusimamia rasilimali za nchi, kudhibiti wizi na ubadirifu, kuongoza vema, kusimamia utekelezaji wa Agenda kubwa za Kitaifa zikiwemo; Ununuzi wa Ndege, Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Mwendokasi, Elimu Bure, kutuimarisha katika undugu na Nchi za SADC, Afrika Mashariki, Afrika na Dunia.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida ametoa fedha kiasi cha Shilingi za Kitanzania Laki moja na shilingi 40 elfu kwa ajili ya kuboresha vyoo vya shule ya msingi Sanza. Fedha hizo zilipatikana wakati mkuu huyo wa Mkoa akiimba wimbo wa kuiburudisha jamii na kuielimisha juu ya Mwenge wa Uhuru 2019, wimbo uliopelekea jamii kuguswa na kuweza kumtunza Mkuu huyo wa Mkoa.
Wimbo
“Mwenge wa Uhuru … unaleta Amani”
“Mwenge wa Uhuru … unalea Upendo”...

MATUKIO KATIKA PICHA





















Mapokezi haya yamefanyika katika Kijiji cha Sanza, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kupambwa na wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019

1. Ndugu Mzee Mkongea Ali - Kutoka Mjini Magharibi (Kiongozi)
2. Ndugu Latifa Khamisi Juwakali - Kutoka Kusini Unguja
3. Ndugu Haji Abdulla Hamad - Kutoka Kaskazini Pemba
4. Ndugu Kenani Laban Kihongosi - Kutoka Iringa
5. Ndugu Malugu Benard Mwanganya - Kutoka Lindi
6. Ndugu Nkwimba Madirisha Nyangogo - Kutoka Songwe

Imetolewa Na;
Kitengo cha Habari na Mawasiliano 
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
SINGIDA

No comments:

Post a Comment