Saturday, April 18, 2015

WORLD VISION TANZANIA YATUMIA ZAIDI YA BILIONI 5.3 KUBORESHA MIRADI YA AFYA SINGIDA.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida, Saidi Alli Amanzi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, akifungua hafla ya makabidhiano wa mradi wa afya ya mama na mtoto (SUSTAIN-MNCH). Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Gishuli Charles na anayefuatia ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa shirika la World vision Tanzania, Mary Lema.Shirika lisilo la kiserikali World Vision Tanzania, limetumia zaidi ya shilingi 5.3 bilioni kugharamia mradi wa kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto Mkoani Singida.
Hayo yamesemwa na Mwakilishi  Mkurugenzi wa Miradi ya World Vision Tanzania  Mary Lema, wakati akitoa taarifa yake kwenye hafla ya makabidhiano ya mradi wa afya na lishe ya mama na mtoto (Sustain-MNCH).
Amesema mradi huo umetekelezwa katika wilaya za Iramba, Mkalama, Ikungi na Singida Vijijini na umedumu kwa miaka mitatu kuanzia januari 2012 hadi mwezi Machi 2015.
Akifafanua, amesema mradi ulijikita zaidi katika kuimarisha mfumo wa afya katika ngazi ya mbalimbali za utoaji wa huduma za afya na lishe ya mama na watoto.
“Mradi umetoa mafunzo kwa watendaji 325 na wasimamizi wa huduma za afya ya mama na mtoto ngazi mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya upangaji na matumizi ya rasilimali zilizopo. Pia mradi umeimarisha mafunzo ya utoaji taarifa za afya (MTUHA) kwa wakati”,amesema Lema.
 
Baadhi ya wadau wa afya waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya mradi wa afya ya mama na mtoto (SUSTAIN -MNCH) iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aque Vitae Resort mjini Singida.

Aidha Mwakilishi huyo  amesema malengo ya mradi huo yamefikiwa kwa kiwango kizuri ambapo idadi ya wanawake wajawazito waliohudhuria kliniki mara 4 wakati wa ujauzito imeongezeka kutoka asilimia 43 wakati mradi unaanza, hadi asilimia 50 wakati tathimini ya mwisho inafanywa.

“Pia idadi ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka asilimia 62 wakati mradi unaanza hadi asilimia 71 kwa sasa”,amesema.
Lema amesema shirika la World Vision lilifikia uamuzi wa kutekeleza mradi huo Mkoani Singida ikiwa ni njia moja wapo ya kuunga mkono juhudi za serikali kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto nchini iliyoridhiwa na umoja wa mataifa.


Afisa afya Mkoa wa Singida, Joseline Ishengoma, akiwasha gari aina ya Land cruiser lililotolewa msaada na shirika la World vision Tanzania kwa hospitali ya mkoa mjini hapa.Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone  ametumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Canada kupitia shirika lake la maendeleo la Department of Foreign Affairs and Trade Development (DFDAT) kwa kuufadhili mradi huo.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Singida Saidi Amanzi amesema, mradi huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya akina mama na watoto katika wilaya za Iramba, Mkalama, Singida Vijijini na Ikungi.
“Kwa kipindi cha mwaka 2011-2013, vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi vilipungua kutoka vifo 52 hadi kufikia vifo 49, na vifo vya watoto wachanga wenye umri kuanzia siku ya kuzaliwa hadi siku ya 28, vimepungua kutoka 182 hadi 178”,amesema.
Dkt. Kone amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa mifumo ya utoaji wa huduma ambapo watoa huduma 101 walipata mafunzo ya utoaji huduma za dharura.
Twakwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazochangia katika asilimia 61 ya vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na asilimia 66 ya vifo vya watoto wachanga.
Kwa mujibu wa takwimu za Tanzania Demographic and Health Survey (TDHS 2010), akina mama wapatao 454 hupoteza maisha kati ya vizazi hai 100,000 ikionesha mafanikio kidogo ukilinganisha na (TDHS 2004/2005 ya vifo 578 kwa kutoa kizazi hai 100,000.
Kasi hii ni ndogo sana ukilinganisha na lengo la kitaifa la kufikia vifo 193 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo desemba 2015.
Kwa upande wa vifo vya watoto wachanga wenye umri wa kuanzia siku ya kuzaliwa hadi siku 28, wapatao 26 kati ya vizazi hai 1,000 hupoteza maisha ambayo ni sawa na watoto 42,343 kwa mwaka. Nusu ya vifo hivyo hutokea ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye n Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Alli Amanzi (wa tatu kulia) akiwa pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya mkoani hapa waliohudhuria hafla ya makabidhiano wa mradi wa afya na lishe kwa mama na watoto.Na Nathaniel Limu, Singida

No comments:

Post a Comment