Wednesday, March 18, 2015

JAMII YATAKIWA KUVUNJA UKIMYA NA KUZUNGUMZA NA VIJANA.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone, ameiagiza jamii kuvunja ukimya kwa kuanzisha utamaduni wa kuwapatia vijana elimu ya afya ya uzazi na ujinsia ili kuwapatia mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maisha yao.

Dokta Kone ametoa wito huo juzi wakati akizungumza kwenye hitimisho la utekelezaji mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia (TMEP) Mkoani Singida.

Amesema jamii inalo jukumu la kuhakikisha inatenga muda wa kuzungumza au kujadiliana mara kwa mara na vijana kwa lengo la kuwapa mbinu bora zitakazowawezesha kutimiza ndoto za kimaisha kama vijana.

Katibu Tawala Miundo mbinu Tiluganilwa Mayunga akizungmza juzi kwenye ufungaji wa hitimisho la mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na ujinsia (TMEP), Mradi huo wa miaka minne uliohitimishwa juzi na kukabidhiwa kwa Halmashauri za wilaya ya Manyoni, Singida na manispaa ya Singida. Kushoto ni Meneja wa TMEP, Cuthbert Maendaenda na kulia ni meneja wa HAPA, David Mnkaje.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Miundo mbinu Tiluganilwa Mayunga, Dokta Kone ameitumia fursa hiyo kuyashukuru mashirika ya Health Actions Promotions Association (HAPA) na Youth Movement For Change (YMC) kwa kutekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa.


"Nimepewa taarifa kwamba hivi sasa wanaume wengi wamebadilika na kuwa chachu katika masuala ya afya ya uzazi na ujinsia.Nimeambiwa kuwa kwa sasa wanaume wanawasindikiza wenza wao kliniki, wanajadili pamoja uzazi wa mpango na wanafanya kazi zote za nyumbani isipokuwa zile za kibailojia. Kabla ya ujio wa TMEP wanaume wote walikuwa wanawaachia kazi nyingi wake zao basi", amefafanua.

Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la Health Actions Promotions Association (HAPA) David Mnkaje akitoa taarifa yake juu ya kumalizika kwa mradi wa ushiriki sawa kwa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na ujinsia (TMEP) mbele ya wadau waliofanikisha mradi huo wa miaka mine uliomalizika mwaka jana. Wa pili kushoto ni Katibu Tawala Miundo mbinu Tiluganilwa Mayunga na wa kwanza kushoto ni Meneja wa mradi wa TMEP Cuthirbert Maendaenda.


Kwa upande wake Meneja wa HAPA David Mnkaje amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne cha mradi huo wamehamasisha jamii na kutoa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa njia mbalimbali ikiwemo ya majadiliano na matumizi ya vikaragosi.

"Pamoja na changamoto za hapa na pale leo wafanyakazi wa HAPA kwa ujumla wetu tunayofuraha kubwa kwa kuwa tumefikia kwa kiasi kikubwa lengo la mradi. Kwa sababu hakuna awamu ya pili ya mradi huu tunaangalia uwezekano wa kuanzisha mradi wa aina hii kati ya Mkoa wa Manyara na Tabora", alisema  meneja huyo.

Naye meneja TMEP Makao makuu Cuthrbet Maendaenda amesema madhumuni kuu la TMEP ni kila mtu katika jamii awe huru kutumia haki yake ya afya ya uzazi na ujinsia wakati madhumuni mahususi ni wanaume wawe chachu ya mabadiliko juu ya mtazamo wao dhidi ya wanawake.

Maendaenda ametaja baadhi ya mikakati ya kuendeleza mradi huo kuwa, ni pamoja na kutoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali na kuwahimiza masuala ya afya ya uzazi na ujinsia yawe ni ajenda ya kudumu katika mikutano ya WDC, kamati za afya, VEO, WEO, waelimisha rika, wahudumu wa afya vijijini.







Katibu Tawala Miundo mbinu Tiluganilwa Mayunga Tiluganilwa Mayunga (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa mradi wa ushiriki wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na ujinsia baada ya wadau hao kukabidhiwa vyeti kwa ushiriki wao katika kutekeleza mradi huo wa miaka minne. Kulia ni Daktari bingwa wa maradhi ya wanawake Mkoani Singida Dokta Suleimani Muttani na kulia ni Meneja wa shirika la HAPA David Mnkeje.


Habari na Gasper Andrew,  Picha na Nathaniel Limu.

No comments:

Post a Comment