Friday, July 23, 2021

IKUNGI YADHAMIRIA KUTOKOMEZA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA NA UDUMAVU

Wilaya ya Ikungi imedhamiria kutokomeza magonjwa ya kuambukiza pamoja na vifo vya mama wajawazito pamoja na changamoto ya utapiamlo kwa watoto wa umri chini ya miaka 5.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Gerry Muro amebainisha hayo wakati wa uzinduzi wa miradi iliyozinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2021 uliopokelewa wilayani hapo leo Julai 23, 2021 katika Viwanja vya Utaho.

Mhe. Gerry Muro amesema Wilaya ya Ikungi imedhamiria kuondoa magonjwa kama Malaria, VVU/UKIMWI, Udumavu na vifo kwa mama wajawazito  kwa kusambaza elimu ya kujikinga na magonjwa hayo kupitia Elimu mashuleni.

Aidha Bi.  Agnes John  mratibu wa lishe katika mradi wa lishe uliopo eneo la soko la viazi  Kata ya Puma  wilayani hapo amesema wanazalisha mazao yenye virutubisho  yakiwemo viazi lishe, mahindi lishe na Mboga ili kusambaza elimu lengo likiwa ni kujenga jamii yenye afya imara kwa kuzingatia lishe bora.

Kufuatia mapambano dhidi ya magonjwa hayo, Halmashauri ya Ikungi imegawa vitamin A kwa watoto chini ya miaka mitano (5) na vidonge vya kuongeza wekundu wa damu.

Akielezea umuhimu wa mradi wa lishe na chimbuko la mapambano dhidi ya magonjwa hayo Bi. Agnes John  amefafanua kwamba  Watoto chini ya miaka mitano (5) wapatao 58,364  walifanyiwa vipimo mbalimbali vya ki afya.

Matokeo ya vipimo hivyo vilibainisha kwamba watoto 2,918 sawa na 5% wana udumavu, watoto 350 sawa na 0.6% wana ukondefu na watoto 9 sawa  na 0.07% wana upungufu wa vitamini zote, wakati  watoto 1,167  sawa na 0.2% wana uzito pungufu. Alisema Bi Agnes John mratibu wa lishe.

Kwa upande wake Dkt. Philip E. Kitundu mratibu wa mradi wa Malaria wilayani hapo amebainisha juhudi za kuondoa ugonjwa huo ikiwemo ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu kwa watu mbalimbali.

Amesema kwamba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali jumla ya kaya 59,608 ziligawiwa vyandarua bure ambapo kwa jamii ya watu wa Wilaya ya Ikungi walipata vyandarua 203,087 lengo likiwa ni kupambana na Malaria.

 Hata hivyo Lucina kimaro mratibu wa mradi wa VVU/UKIMWI anasema umekuwepo mradi wa VVU/UKIMWI  ambapo Wilaya imeanziasha vituo  46 vya kutolea huduma za VVU/UKIMWI ambapo  23 vinatoa huduma za tiba na maangalizi (CTC) kama sehemu ya mapambano ya ugonjwa huo.

Mradi mwingine uliyozinduliwa ni wa kuzuia matumizi ya madawa ya kulevya ambapo BW. SSP.Fortunatus Biyacca mkuu wa Polisi katika taarifa yake anasema elimu hiyo itasaida kuwa na vijana wakakamavu na wachapakazi ambao watakuwa na afya bora.

Kwa mujibu wa Bw. SSP. Fortunatus uchunguzi umebaini kwamba vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 30 ni wahanga katika matumizi ya madawa ya kulevya.

Amesema kuwa walishakamata kilo 450.5 za bangi na kilo 50.3 za mirungi ambapo mashtaka 222 yameripotiwa polisi na kati ya hayo  mashauri 20 yalifikishwa Mahakamani.

Aidha  watuhumiwa 8 katika mashauri hayo wametiwa hatiani na mashauri 12 yanaendelea  na upelelezi. Alisema SSP. Fortunatus.

http://www.singida.go.tz/new/ikungi-yadhamiria-kutokomeza-magonjwa-ya-kuambukiza-na-udumavu

No comments:

Post a Comment