Wednesday, July 21, 2021

WANANCHI MKALAMA WATAKIWA KUTUNZA MIRADI YA MAENDELEO

 

Kiongozi maalum wa Mbio za Mwenge  wa Uhuru kitaifa Lt. Josephine  Paul Mwambashi akizindua  Klabu ya kupinga Rushwa ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Jorma wilayani Mkalama.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe.  Sophia Mfaume Kizigo amewataka wananchi wa Wilaya ya Mkalama iliyopo mkoani Singida kutunza  miradi waliyoianzisha ili iweze kuwaongezea tija na kipato kwao na taifa kwa ujumla.

Akiongea baada ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi katika miradi mbalimbali  iliyokaguliwa na Mwenge wa Uhuru leo Julai 21, 2021 katika Wilaya hiyo amewataka wananchi kuhakikisha miradi inatunzwa ili kufikia malengo yaliyotarajiwa.

Amesema, miradi Zaidi ya nane ikiwemo ujenzi wa visima vya maji katika maeneo tofauti, ujenzi wa barabara, programu za kupambana na madawa ya kulevya pamoja na matumizi ya mifumo mbalimbali ni moja ya miradi iliyozinduliwa  na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2021  wilayani hapo.

 kuzinduliwa na uwekaji wa mawe ya msingi kwa miradi yetu ni ishara ya usimamizi mzuri wa miradi, hivyo  ni jukumu letu sote kuhakikisha kwamba tunaitunza miradi yetu ili iweze kutuletea mafanikio” alisema Mhe. Sophia.

Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mkoa wa Singida Fredrick Ndahani  (kulia) akizungumza na wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa  2021 kuhusu lishe bora.

Pia amewataka wana Mkalama  kuhakikisha wanapata lishe bora  ili kuendelea kupunguza udumavu kwa watoto na kwa wakina mama wajawazito.

Kwa upande wake Kiongozi maalum wa Mbio za Mwenge  wa Uhuru kitaifa Lt. Josephine  Paul Mwambashi ametoa wito kwa wanamkalama kuongeza ujuzi katika matumizi ya TEHAMA kwa kuwa  huko ndipo ajira zinapopatikana.

LT. Mwambashi amebainisha kwamba  masoko ya mazao na malipo mbalimbali ya huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na mashirika mbalimbali yanapatikana katika mifumo ya TEHAMA.

Aidha LT. Mwambashi amebainisha kwamba matumizi  sahihi ya mifumo mbalimbali ya kieletroniki yameonesha kusaidia nyanja ya usafirishaji, Afya pamoja na upatikanaji wa taarifa kwa wakati  hivyo kuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya uchumi nchini.

Hata hivyo kiongozi huyo wa Mwenge kitaifa amewataka vijana kuepuka ngono zembe pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya  ambayo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikikatisha ndoto za vijana  wengi nchini.

Amesema mbio za Mwenge mwaka huu  zitumike kupambana na magonjwa mbalimbali yakiwemo malaria na VVU/UKIMWI.

Tufanye usafi wa mazingira pamoja na kufukia madimbwi ili kupambana na mazalia ya mbu wanaosababisha malaria, lakini pia tuhakikishe tunaepuka ngono zembe ili kuepuka ugonjwa wa VVU/UKIMWI” Alisema LT. Mwambashi

Hata hivyo amewakumbusha wananchi wa  Mkalama kutumia vyandarua vyenye viuatilifu lengo likiwa ni kuhakikisha malaria inakwisha. Alisisitiza Lt. Josephine Paul Mwambashi.

www.singida.go.tz

No comments:

Post a Comment