WAUMINI wa madhehebu ya Dini mbalimbali na wasio waumini mkoani
Singida wamehimizwa kuitumia siku kuu ya Pasaka kumaliza tofauti zilizopo
kwenye ndoa, familia zao ili amani na utulivu iendelee kudumu kuanzia ngazi ya
familia, mkoa na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa umoja wa madhehebu ya
dini manispaa ya Singida, Sheikh Hamisi Kisuke, wakati akizungumza kwenye hafla
ya kuwatakia kheri waumini wa dhehebu ya dini ya Kikristo, waumini
wengine na wale wasiokuwa na dini.
Akifafanua amesema, amani na utulivu ndio mambo pekee ambayo
yanatoa fursa kwa binadamu kujiletea maendeleo endelevu, kwa uhuru
mkubwa.
Aidha, amewataka waumini hao kutumia siku kuu ya Pasaka
kuimarisha upendo bila kujali itikadi ya dini yoyote kwa madai Mungu
kwenye amri zake, ameagiza binadamu kupendana.
“Kwa kifupi katika umoja wetu wa madhehebu ya dini, tunapenda
kuona mume na mke wa dini yoyote kama kuna sitofahamu yoyote waitatue kipindi
hiki cha Pasaka. Pasaka ikimalizika waanze maisha mapya na mema” amesema Sheikh
Kisuke ambaye pia ni diwani kata ya Misuna.
Pia Sheikh Kisuke, ametumia nafasi hiyo kumpongeza na kumshukru
mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, kwa juhudi zake za kusimamia vema
maendeleo ya mkoa wa Singida kwa ufanisi.
“Mkuu wetu wa mkoa Dkt. Rehema Nchimbi ni muasisi wa umoja wetu
wa madhehebu ya dini mbalimbali katika mkoa huu. Umoja huu umesaidia kwa kiasi
kikubwa waumini wa madhehebu ya dini kuheshimiana, kuaminiana na
kushikamana kama ndugu. Nampongeza sana Dkt. Nchimbi kwa hili” amesema mwenyekiti
huyo.
Kwa upande wake Askofu msataafu Kanisa la Pentekoste (FPCT) la
mjini kati, Dkt. Paulo Samwel, amesema, Umoja huo sio wa kisiasa. Umoja huo ni
wa kweli na unatekeleza yote yale yanayompendeza Mungu na raia wote wema.
“Ndugu zangu, mvua msimu huu haijakidhi mahitaji, nawaomba
waumini wa madhehebu ya dini mbalimbali na wasio na dini waondoe hofu ya aina
yoyote. Mungu wetu hatatutupa kamwe, ataleta neema zake kwa namna nyingine”
amesema Dkt. Paulo.
Wakati huo huo, Jaji mstaafu, Fatuma Masengi, amesema, wakazi wa
mkoa wa Singida wawe na amani kipindi hiki cha Pasaka kwa kuwa Mungu ataendelea
kuwalinda wao na viongozi wao.
No comments:
Post a Comment