Monday, June 18, 2018

RC SINGIDA AMEWAAGIZA MADIWANI WOTE MKOANI SINGIDA KUONGOZA OPARESHENI YA KUWAKAMATA WATU WANAOSABABISHA MIMBA KWA WANAFUNZI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewaagiza Madiwani wote wa Mkoa wa Singida kuongoza oparesheni ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria watu wote watakaobainika kuwatia mimba wanafunzi mkoani Singida.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoadhimishwa katika kijiji cha Doromoni, Kata ya Tulya Tarafa ya Kisiriri, wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Dkt. Nchimbi amesema, vitendo vya kuwapa mimba wanafunzi ni jambo baya na linapaswa kulaaniwa na jamii nzima.

Amesema Serikali kamwe haiwezi kuvumilia vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi kimasomo hivyo watu watakaobainika kufanya vitendo hivyo ni lazima wachukuliwe hatua kali za kisheria kuondoa kabisa tatizo hilo mkoani Singida.

Dkt. Nchimbi, amewataka viongozi katika ngazi zote washirikikiane na Madiwani wote kufanikisha kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo katika jamii.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mkuu wa mkoa wa Singida ametoa muda wa miezi 4 kwa Wakurugenzi na Wakuu wa wilaya mkoani Singida kukamilisha jengo moja la Maabara katika kila shule ya Sekondari mkoani Singida.

Dkt. Nchimbi amesema hadi kufikia mwezi wa 9 mwaka huu 2018 anataka kupata taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa Maabara hizo.

Amesema ujenzi wa majengo ya Maabara katika shule za Serikali itasaidia na kuhamasisha wanafunzi kujifunza masomo ya Sayansi ili kuongeza wataalamu wa fani mbalimbali nchini.

Kuhusu vitendo vya uvuvi haramu katika ziwa kitangiri wilayani Iramba, Dkt. Nchimbi ameonya vikali kuhusu vitendo hivyo ambavyo vinaharibu mazalia ya Samaki na kutaka wananchi wanaofanya vitendo hivyo kuchukuliwa hatua stahiki.

Amesema vitendo hivyo vya uvuvi haramu vikiachwa viendelee katika ziwa hilo vitasababisha Samaki na viumbe vingine kupotea na kuleta athari za kiuchumi kwa wananchi kwasababu samaki hao huuzwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.

Katika maadhimisho hayo ya Siku ya Mtoto wa Afrika mkoani Singida umeonyesha kuwa na matukio machache ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya Watoto ambapo kati ya Julai 2017 hadi Mei mwaka 2018, Jumla ya matukio 8 na unyanyasaji wa ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa mkoani Singida.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Mtoto wa Afrika yamefanyika katika kijiji cha Doromoni wilayani Iramba yameambatana na zoezi la utoaji wa chanjo ya minyoo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 pamoja na upimaji wa macho na kutoa tiba kwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani Iramba, mkoa wa Singida.

 Matukio mbalimbali katika picha:
















  
 




 

 


 
 



 



 Imetolewa na;
Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Singida

No comments:

Post a Comment