Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akimpongeza Balozi Nicolous Kuhanga mara
baada ya kutunukiwa na Mhe Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, shahada ya
heshima ya uzamivu kutokana na mchango wake mkubwa hasa wakati wa kuanzishwa
kwa Chuo Kikuu Huria Tanzania.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa Kassim akimpongeza Mke wake Mama Mary Majaliwa mara baada
ya kutunukiwa shahada ya uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera
kutokana katika Chuo Kikuu Huria Tanzania mapema jana Mjini Singida.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa Kassim amesema
kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa elimu ya juu nchini ili kuuboresha uweze
kusaidia kutayarisha haraka rasilimali watu walioelimika zaidi,
watakaoliwezesha taifa kuwa na maendeleo na kufikia uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025.
Waziri Mkuu
Majaliwa ameyasema huyo jana wakati akizungumza kwenye kilele cha mahafali ya
33 ya Chuo Kikuu huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa
Katoliki mjini Singida.
“Kwa
kuzingatia malengo ya dira ya taifa ya maendeleo na mwelekeo wa serikali ya awamu
ya tano, napenda nisisitize kuwa dira ya utendaji wenu ijikite katika maeneo
yaliyoainishwa chini ya mwamvuli wa kauli mbiu ya chuo-elimu bora na nafuu kwa
wote”, amesema.
Amesisitiza
kwa kusema kwa uchumi wa kati na wa viwanda, hauwezi kufikiwa au kuwa endelevu
pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika elimu ya juu cha angalau asilimia 23.
“Hivi sasa
kiwango cha Tanzania cha udahili katika elimu ya juu ni aslimia nne (4). Kiwango
hiki ni kidogo hata kuliko nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao
licha ya hali ya vita nchini mwao kwa muda mrefu,wamefikia asilimia saba (7)”,amefafanua.
Waziri
Mkuu Majaliwa amefafanua zaidi kwa kusema kuwa takwimu zinaonyesha kwamba
karibu nchi zote washiriki katika jumuiya ya Afrika mashariki, ukiacha Burundi,
zina viwango vya juu zaidi vya udahili katika elimu ya juu ikilinganishwa na
kiwango cha Tanzania.
Amesema kwa mujibu
wa sera ya elimu ya mwaka 2014 mfumo wa elimu na mafunzo umetawaliwa na muundo
wa kitaaluma wenye dhana ya kuchuja wahitimu kwa kila ngazi ili kupata wachache
wenye uwezo mkubwa katika taaluma.
“Hali hii
inatokana na nafasi za elimu na mafunzo ngazi za juu kuwa chache kadri
wanafunzi wanavyohitimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na kuendelea. Kwa
uhaba wa nafasi za elimu ya juu na ufinyu wa bajeti ndio unaosababisha kutumia
muundo wa kuchuja badala ule wa kutoa fursa kulingana na uwezo, vipaji na
vipawa”, amesema na kuongeza;
“Huu
ndio mfumo ambao unahitaji kuhuishwa na mfumo wa elimu huria na masafa kama
alivyoeleza Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Profesa Joyce Ndalichako kwamba
mazingira, vigezo na masharti ya mchakato huu vimeainishwa katika sera ya elimu
na mafunzo 2014’.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali inaunga mkono azma ya Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuanzisha dawati maalum kwa ajili ya kuimarisha
mfumo wa elimu huria na masafa.
“Kupitia hafla
hii, ninaagiza dawati kama hili lianzishwe pia katika Tume ya vyuo vikuu (TCU)
na Baraza la elimu ya ufundi (NACTE), kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu
zao za ithibati zinazingatia na kukidhi matakwa ya viwango vya mfumo wa elimu
huria na masafa”, amesema.
Katika
Mahafali hayo Mkuu wa Chuo Kikuu Huria na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Peter
Pinda amemtunuku shahada ya heshima ya uzamivu Balozi Nicolous Kuhanga ambaye
mchango wake umetajwa kuwa mkubwa hasa wakati wa kuanzishwa kwa chuo hicho.
Zaidi
ya wahitimu 2200 wamehitimu katika Chuo Kikuu hicho na kutunikiwa shahada
mbalimbali ambapo mke wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Mama Mary Majaliwa, amekuwa miongoni mwa
wahitimu akitunukiwa shahada ya uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na
Sera.
No comments:
Post a Comment