Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi akizungumza na wakazi wa Singida waliojitokeza katika maadhimisho ya
wiki ya nenda kwa usalama yaliyofanyika juzi katika viwanja vya stendi ya
Singida Mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP
Debora Magiligimba akizungumza na wakazi wa Singida waliojitokeza katika
maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama yaliyofanyika juzi katika viwanja vya
stendi ya Singida Mjini.
Kikundi cha burudani wakionyesha
ukakamavu katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama yaliyofanyika juzi katika
viwanja vya stendi ya Singida Mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP
Debora Magiligimba akiimba na kikundi cha burudani huku Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt Rehema Nchimbi akicheza katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama
yaliyofanyika juzi katika viwanja vya stendi ya Singida Mjini.
Madereva wa vyomo vya moto hasa bajaji
na bodaboda wamewahimizwa kujiunga na chuo kikuu huria ili waweze kujiendeleza
kielimu na kuboresha huduma zao, ambapo kwa kufanya hivyo watasaidia kupunguza
kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi ametoa wito huo juzi wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho
ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yaliyofanyika kwenye kituo cha zamani
cha mabasi cha Mjini Singida.
Amesema masomo ya chuo kikuu huria
humwezesha mtu kujiendelea kwa kupata elimu bora bila kuathiri shughuli zake za
kila siku hasa za kujipatia kipato.
“Dereva wa bodaboda, bajaji au mkazi
yeyote mkoani kwetu, tusiridhike na elimu tuliyonayo, kumbukeni elimu haina
mwisho. Hivyo tutumie chuo chetu hiki cha huria kujiendeleza kielimu. Tukiwa na
wasomi wengi mkoa wetu kwa vyovyote
lengo la kuwa na uchumi wa kati na chini ya viwanda utalifikia kwa
haraka”, amesema.
Dkt Nchimbi amwataka madereva wa vyombo
vya moto kutii na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na
sio tu kuendeshwa na kamera za barabarani.
“Baadhi ya madereva wa vyombo vya moto, hawaheshimu
kabisa sheria za usalama barabarani, wanaendeshwa na kamera. Siku moja yupo dereva mmoja wa
bodaboda alikuwa mbele yangu, huku akiandika ujumbe kwenye simu yake. Utamaduni
huu haufai kwa sababu ni chanzo cha ajali”,amesema Dkt.Nchimbi.
Aidha amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Singida ACP Debora Magiligimba kusimamia zoezi la madereva wa bajaji na
bodaboda kujiunga na Chuo kikuu Huria.
“Hebu angalia uwezekano wa kuanzisha
mfuko maalumu kwa ajili ya madereva hawa kujiendeleza kielimu. Tunataka ifike
siku tuwe na madereva hawa wana diploma au digrii, kwa hili nina imani na wewe
utaweza kuwasaidia vizuri”, amesema.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt Rehema Nchimbi amesema atagharamia safari ya viongozi wa madhehebu ya dini
kwa kutoa kiasi cha shilingi laki tano, kwenda kufanya sala maalum kwenye
maeneo yaliyokidhiri kwa vitendo vya
ajali.
“Karibu kila wilaya ina eneo ambalo
ajali haziishi kutokea mara kwa mara. Nina imani Mungu hajanipa mkoa wenye
maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajali. Nimekubaliana na viongozi wangu wa madhehebu ya dini wataenda katika
maeneo hayo, na kuomba Mungu atuondolee balaa la ajali za barabarani kwenye
maeneo hayo”, amesema.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Singida ACP Debora Magiligimba amewaagiza viongozi wa madereva wa bodaboda
na bajaji, kusimamia vema madereva hao ili wapunguze ajali za barabarani.
Mmoja kati ya wakazi wa Manispaa ya
Singida, Njolo Kidimanda, amesema kuwa kuna haja serikali kuongeza kiwango cha faini kwa madai
kiwango kilichopo, hakiwaogopeshi kabisa
baadhi ya madereva.
Aidha, Kidimanda ameshauri madereva
kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu salama, ili kusaidia majeruhi wa
ajali barabarani wenye hitaji la damu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Singida, jumla ya watu 68 wamefariki kutokana na ajali za
barabarani kati ya Januari hadi Oktoba mwaka huu. Idadi hiyo imeonyesha
kupungua kwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani kwa kuwa katika kipindi hicho hicho
mwaka jana, watu 152 walifariki.
No comments:
Post a Comment