Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi akizungumza na Wahadzabe waliokuwa wakijiandaa kupokea fedha kutoka
Mpango wa Tasaf katika kijiji cha Munguli Wilayani Mkalama, Dkt Nchimbi
amewatahadharisha kutofanya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Walengwa wa Tasaf wa kijiji cha Singa
Wilayani Mkalama wakimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi (hayupo
pichani) alipowatembelea kushuhudia ujenzi wa bwawa walilolijenga katika mpango
wa ajira za muda za Tasaf.
Bwawa lililopo katika kijiji cha Singa
Wilayani Mkalama lililojengwa na walengwa 246 wa Tasaf katika mpango wa ajira
za muda, bwawa hilo linaujazo wa mita 5777.6 ambalo litasaidia upatikanaji wa
maji na uanzishwaji wa kilimo cha umwagiliaji,
Dkt Nchimbi ameagiza halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuweka miundombinu
ya kunyweshea maji mifugo kutoka katika bwawa hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi ameshauri Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) uanzishe kazi za
ajira za muda kwa walengwa wa Mpango huo kutoka jamii ya Wahadzabe waliopo
Wilayani Mkalama ili uwasaidie kuinua uchumi wao.
Dkt Nchimbi ametoa ushauri huo mara
baada ya kutembela kijiji cha Singa Wilayani Mkalama na kuona bwawa
litakalotumika kuhifandhi maji ya mvua kwa ajili ya shughuli mbalimbali lililojengwa
na walengwa wa Tasaf Kijijini hapo kisha kutembelea kijiji cha Munguli Kata ya
Mwangeza Wilayani humo aliposhuhudia
malipo ya walengwa wa kihadzabe wa Mpango wa Tasaf.
Ameeleza kuwa jamii ya wahadzabe
hawana mradi unaohusisha kazi za ajira za muda ambazo zimekuwa zikisaidia
katika kuongeza kipato, kuwafundisha thamani ya kazi pamoja na kutekeleza
miradi ambayo imekuwa ikisaidia jamii nzima kama vile mabwawa na barabara.
“Nashauri TASAF kabla ya msimu huu wa
mvua kuisha muwaletee na hawa wahadzabe mradi wa ajira za muda kama ambavyo
walengwa wa vijiji vingine wamekuwa wakifanya kazi hizo na zimekuwa zikichangia
maendeleo kwa vijiji vyao”, ameeleza na kuongeza kuwa,
“Miradi ya ajira za muda zitawafundisha
Wahadzabe kujituma kufanya kazi ambazo zinachangia maendeleo ya jamii huku kazi
hizi zikiwa kama darasa la wao kujifunza kwa vitendo kuwa kama anaweza kwa
mfano kushiriki kujenga bwawa basi anaweza kufanya jambo kubwa katika familia
au maisha yake”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha ametoa tahadhari kwa walengwa
hao wa kihadzabe kuwa wasitumie pesa wanayopewa kwa kunywa pombe badala yake
pesa hiyo itumike sawasawa na maelekezo ya mpango huo na hatua zichukuliwe kwa
wale watakaokaidi.
Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji
Kutoka Tasaf Makao Makuu Anna Njau ambaye aliambatana na Mkuu wa Mkoa Dkt
Nchimbi katika ziara yake ameeleza kuwa ushauri huo ni mzuri na una lengo la
kuwasaidia wananchi kama ambavyo Tasaf imekuwa na lengo la kuinua jamii hasa
kaya masikini hivyo wazo hilo ataliwasilisha makao makuu kwa ajili ya
utekelezaji.
Baadhi ya wahadzabe waliofika kupokea
fedha za Mpango wa Tasaf wameeleza kuwa fedha hizo zimewasaidia kuwainua
kiuchumi kwa kuhakikisha wana chakula cha kutosha, watoto wameenda shule,
watoto wadogo wamepelekwa kliniki huku wakijiendeleza zaidi kiuchumi kwa
ufugaji mdogo wa kuku na mbuzi pamoja na kuboresha makazi yao.
Jamii ya Wahadzabe waliopo Kijiji cha
Munguli na hasa kitongoji cha Kipamba Wilayani Mkalama wamekuwa wakiishi kwa
kutegemea uwindaji wa wanyama pori, kula asali, ubuyu, matunda na mizizi
mbalimbali ambapo juhudi za Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf)
umesaidia jamii hiyo kuanza kupeleka watoto shule, kuanzisha shughuli za
uzalishaji mali kama vile kilimo na ufugaji.
No comments:
Post a Comment