Wednesday, November 29, 2017

NAIBU WAZIRI TAMISEMI AZIAGIZA HALMASHAURI KUTUMIA ‘MAFUNDI WAZAWA’ KATIKA MIRADI MIDOGO; AFURAHISHWA NA MIRADI YA WILAYANI MKALAMA.



Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akipima kiasi cha saruji kilichowekwa kwenye mchanga katika ujenzi shule ya Sekondari Iguguni Wilayani Mkalama katika ziara yake ya Siku moja kufuatilia utoaji huduma mbalimbali kwa jamii.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisisitiza jambo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jakson Masaka (kulia kwake) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga (kushoto kwake).
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisalimiana na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jaksoni Masaka mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya Ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya elimu na maji.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisalimiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama Elizabeth Rwegasira mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya Ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya elimu na maji.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda ameziagiza halmashauri zote nchini kutumia mafundi wa kawaida wazawa waliopo katika maeneo yao katika miradi yote midogo kupitia utaratibu unaojulika kama ‘force account’.

Naibu Waziri Kakunda ametoa agizo hilo jana mara baada ya kufanya ziara Wilayani Mkalama kufuatilia utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii huku akijikita zaidi katika sekta ya Maji na Elimu, ambapo ametembelea mradi wa maji Iguguno na Shule ya Sekondari Iguguno.

“Matumizi ya Wakandarasi yabaki katika miradi mikubwa tu lakini miradi yote midogo tuwatumie mafundi waliopo katika maeneo yetu, mafundi hawa wazawa wanatekeleza kazi kwa ubora kama huu ambao nimeuona leo na kwa gharama ambazo ni nzuri,” amesisitiza mara baada ya kutoa agizo hilo.

Ameeleza kuwa gharama na ubora wa mradi wa Shule ya Sekondari ya Iguguno ambao unajumuisha ujenzi na ukarabati wa madarasa 8, mabweni mawili, vyoo vyenye matundu 11, bwalo la chakula na maabara ambapo vyote hivyo vimegharimu milioni 416, unatosha kudhirihisha kuwa mafundi wa kawaida wazawa wanaweza kufanya kazi nzuri.

“Huu mradi endapo tungetumia utaratibu wa wakandarasi na wazabuni hiyo gharama ya milioni 416 ingekuwa kama robo ya gharama, nasisitiza wakandarasi na wazabuni watumike katika miradi mikubwa tu”, Naibu Waziri Kakunda amesisitiza.

Ameongeza kwa kuipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambao umewezesha usambazaji wa maji katika kata yote ya Iguguno na kuwasaidia wananchi wasihangaike kupata maji.
Aidha Naibu Waziri Kakunda ameonekana kutofurahishwa na taarifa kuhusu wanafunzi 12 waliokatishwa masomo tangu mwezi Januari Mwaka huu kutokana na sababu ya kupewa ujauzito, ambapo ametoa rai kwa wazazi na walezi wote nchini kuwa mstari wa mbele kukomesha tatizo hilo.

Ameeleza kuwa wazazi wengi wamekuwa wakifanya makubaliano ambapo mwanafunzi aliyepewa ujauzito anamkana mhalifu aliyempa ujauzito ili kumuepusha na kifungo cha miaka 30 jela, jambo linalofanya kesi nyingi kukosa ushahidi huku tatizo la mimba kwa wanafunzi likiendelea kuwepo.

Naibu Waziri Kakunda amesema ili kukomesha hilo serikali kupitia Wizara yake ina dhamira ya kupeleka hati ya dharula bungeni ili itungwe sheria itakayofuta dhamana ya mtuhumiwa atakayempa ujauzito mwanafunzi huku uchunguzi wa Vinasaba (DNA) utatakiwa kufanyika ili kuthibisha kama mtuhumiwa ndiye baba wa mtoto ama la.

Awali, Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Alan Kiula amewasilisha changamoto mbalimbali za Wilaya hiyo kwa Naibu Waziri Kakunda kwa kumueleza changamoto kubwa ni kutokuwa na hospitali ya Wilaya.

Mhe. Kiula ameongeza kuwa upungufu wa watumishi katika Wilaya hiyo hasa wa Sekta ya Elimu na Afya umekuwa ukikwamisha baadhi ya shughuli kufanyika kwa kasi inayotakiwa.

Aidha amemshukuru Naibu Waziri Kakunda kwa ahadi yake ya kuitazama Wilaya hiyo kwa jicho la pekee katika mgao ujao wa watumishi kwa Mwezi Disemba na Januari huku akimuhakikishia kuwa Halmashauri itafanya kwa haraka taratibu za awali za upatikanaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya.

No comments:

Post a Comment