Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na madiwani na wakuu wa idara wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakati wa Baraza Maalumu la kujadili hoja za
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Baadhi ya madiwani wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakifuatilia hoja wakati wa Baraza Maalumu la
kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt Angelina M Lutambi (wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Iramba
Emmanuel Luhahula wakiandika baadhi ya maoni na maelekezo katika Baraza Maalumu
la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Madiwani wametakiwa
kuacha mzaha wa kuwachekea na kuwaendekeza watumishi ambao wamesababisha Halmashauri
ya Wilaya ya Iramba kupata hati chafu ya Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za
Serikali katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi ameyasema hayo jana wakati wa baraza maalum la
madiwani la kujadili hoja 122 za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali katika
halmashauri hiyo.
Dkt Nchimbi
amewaambia madiwani kuwa wao ndio wazawa na ndio wawakilishi wa wananchi hivyo
wanapozembea kuwasimamia na kuwabana watumishi ili wafuate kanuni, sheria na
miongozo, watakaoumia ni wananchi wao pamoja na halmashauri yao kukosa ruzuku
ya serikali.
“Madiwani acheni
mzaha wa kuwachekea hawa watumishi, unapoona hoja ujue kiwanda ni watumishi,
lakini mmepata hati chafu miaka mitatu mfululizo hamshtuki tu kuna watu wana wanawahujumu?
Au mnaweza kujiendesha bila ya ruzuku ya serikali? Semeni leo? Wananchi
wamewaamini hebu watumikieni ipasavyo,” amesema Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa
halmashauri inapoendelea kupata hati chafu hiyo ni sifa mbaya kwao na hata kwa
mkoa mzima kwakuwa watendaji wa ngazi za mkoani mpaka halmashauri wanaonekana
wameshindwa kutekeleza wajibu wao vema.
Dkt Nchimbi amesema
madiwani waweke utaratibu ili wakuu wa idara waliothibitishwa wabaki katika
halmashauri hiyo kwa kipindi kirefu kwakuwa wamekuwa wakithibitishwa kisha
wanahama jambo linalowafanya wakose wakuu wa idara wa kutosha na kubaki na
wanaokaimu.
“Kuna baadhi ya
watumishi wanaharibu tu kwakuwa wanajua watahama hapo, lakini ninyi madiwani na
wananachi hamtaweza kuhama hapo ndio kwenu hivyo basi wekeni utaratibu tu, mkuu
wa idara akithibitishwa abaki hapo kwa muda awatumikie wananchi au akitaka
kuhama basi atafute wa kubadilishana naye”, amesisitiza.
Aidha Dkt Nchimbi
amewataka watumishi kuacha uzembe, watumie fursa zilizopo katika kujiongezea
kipato lakini wasifanye biashara na halmashauri huku akiwashauri kuwasikiliza
viongozi wa dini ambao wanawahimiza uadilifu na uchapa kazi.
Naye Mkaguzi wa Nje
wa Hesabu za Serikali Annamary Kakunguru amesema baadhi ya watumishi wa
halmashauri hiyo wamekuwa wazito katika kujibu hoja, kufuta hoja pamoja na
kufuata maoni ya mkaguzi wa Nje hivyo kuisababishia halmashauri kuwa na hoja
nyingi zinazodumu kwa muda mrefu.
Kakunguru amesema
watumishi wanapaswa kubadilika na kuwa na utendaji mzuri pamoja na kupeana
ushirikiano ili kwa pamoja waweze kufuta hoja na kuweka mikakati mizuri ya kuzuia
hoja.
Pia Katibu Tawala
Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi amewaasa watumishi kufanya kazi kwa
kufuata miongozo, sheria na kanuni ili kuepuka kutengeza hoja huku wakuu wa
idara wanaokaimu wakitakiwa kufanya kazi kwa bidii ili utendaji wao uonekane.
Lutambi ameongeza
kuwa utendaji wa ushirikiano ndio utaifanya halmashaur hiyo kusonga mbele huku
akiwaeleza kuwa hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali zinawakumbusha kuongeza
uadilifu na usimamizi wa fedha na shughuli za serikali.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba Linno Mwageni amemshukuru Dkt Nchimbi kwa
kuwakumbusha kuwajibika ili waendane na kasi ya awamu ya tano ya hapa kazi tu.
Mwageni amemweleza
Mkuu huyo kuwa siku nyingine asisite kuwaonya pale wanapoenda tofauti huku
akiahidi kwa niaba ya watumishi kubadilika na kuongeza bidii katika utendaji na
usimamizi wao.
Wakati huo huo Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amekabidhi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli vitanda vya kuzalia vitatu, vya
kawaida 20, mashuka hamsini na magodoro hamsini
vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa hospitali na vituo vya kutolea
huduma za afya Wilayani humo.
Dkt Nchimbi amesema
Rais Magufuli ameonyesha upendo wake kwa wana Iramba hivyo wasiogope kutumia huduma
za afya katika vituo vya serikali kwa kuwa sasa huduma zimeboreshwa, huku
akiwaasa wakunga wa jadi wawaache wajawazito wakajifungulie hospitali na vituo
vya afya.
Ameongeza kuwa watoa
huduma na madaktari sasa wameboreshewa mazingira ya kufanyia kazi hiyo
wanapaswa kutoa huduma kwa uadilifu mkubwa na kwa bidii.
Mganga Mkuu wa Wilaya
ya Iramba Boniphace Richard amemshukuru Rais Magufuli kwakuwa walikuwa na
upungufu wa mashuka 400, ambapo jitihada za Rais zimewapatia mashuka 150 huku
wakipanga kununua mashuka 200 kwa mapato ya ndani.
Jitihada za Rais
Magufuli zimeungwa mkono na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa
Mkoa, Mwenyekiti wa halmashauri na madiwani, Mkurugenzi wa halmashauri na
watumishi ambao kwa pamoja wamechangia mashuka 96, magodoro matano na pesa
shilingi elfu hamsini.
Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Iramba Linno Mwageni akimshukuru Dkt Nchimbi kwa kuwakumbusha kuwajibika katika
Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Iramba Simioni Tiyosera baadhi ya mashuka yaliyotolewa na Rais Magufuli kwa
ajili ya halmashauri yake.
Mganga Mkuu wa Wilaya
ya Iramba Boniphace Richard akimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia mashuka,
vitanda na magodoro ambayo yamesaidia kupunguza uhaba wa vifaa hivyo na
kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment