Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na uongozi na wanachuo kilichopo katika
Masjid ya Shafii wakati akitangaza kukifunga mapema leo katika eneo la Mwaja
Manispaa ya Singida.
Wanachuo kilichopo katika msikiti wa Shafii eneo
la Mwaja manispaa ya Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida dkt Rehema
Nchimbi na kamati yote ya ulinzi na usalama ya Mkoa (hawapo pichani)
wakitangaza uamuzi wa kukifungia chuo hicho.
Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa wa Singida imekifungia chuo kilichopo chini ya Masjid Shafii
katika eneo la Mwaja Manispaa ya Singida kutokana na Shughuli zake
kutofahamika, kukosa usajili na miundombinu yake kutoridisha.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulizi na Usalama ya Mkoa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi amekifungia chuo hicho leo asubuhi kutokana na kutokuwa na usajili na
hivyo kutumia usajili wa msikiti namba 4834 pia kujiendesha bila ya kuwa na
mtaala wowote unaoonyesha mafunzo yanayotolewa na hatma ya wanaosoma hapo.
Akiwa ameambatana na
Wajumbe wote wa Kamati hiyo Dkt Nchimbi amesema baada ya kukifunga, wahusika
wafuatilie usajili wa chuo hicho na kuhakikisha wanafunzi 80 ambao wametoka
ndani na nje ya Mkoa wa Singida wanarudi makwao mara moja.
Ameongeza kuwa
waalimu wawili wa chuoni hapo ambao ni raia wa kigeni kutoka Marekani na Yemen warudi
katika makao makuu ya taasisi yao kwakuwa walikuja Singida kwa ajili ya chuo na
sasa kimefungwa, huku akimuagiza Afisa Uhamiaji wa Mkoa kutoa usaidizi ili raia
hao wafike salama wanakostahili kwenda.
“Chuo hiki kifungwe
mara moja, fuatilieni usajili kwanza kwakuwa sheria za nchi zinataka chuo
chochote kile lazima kiwe na usajili, pia wanafunzi wote warudi makwao, Kamanda
wa Polisi Mkoa hakikisha unasimamia watoto hawa wanafika makwao salama”,
ameagiza Dkt. Nchimbi.
Amesema pamoja na
chuo hicho kutokuwa na usajili, bado wana changamoto nyingine ambazo wanatakiwa
kuzishughulikia kabla hawajafuguliwa ikiwemo miundombinu ya mabweni na vyoo vya
kujitosheleza.
“Tungependa kujua
aina ya mafunzo mnayotoa na yatamuwezesha vipi atakayehitimu kujikimu kimaisha
pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa, pia Afisa Afya amekagua na kuona mapungufu,
hakikisheni mnakuwa na vyoo pamoja na mabweni ya kutosha, mtakapokuwa tayari
hata kama ni ndani ya wiki moja au mwezi hata mwaka ndipo nitakifungua tena
chuo hiki”, amesisitiza.
Dkt Nchimbi ameongeza
kuwa Serikali inapenda na kuthamini taasisi za kidini kwakuwa zinatoa malezi ya
kimaadili ya kuwajenga wananchi kuwa waadilifu na wachapakazi hivyo
wanachotakiwa kufanya ni kufuata taratibu na sheria katika kuanzisha chuo chao.
Amesema nia yake ni
kuona chuo hicho kinakamilisha taratibu za kisheria ndipo kifunguliwe huku
akiamini kuwa kitaweza kuwa chuo bora na cha mfano wa kuigwa kwa kuzalisha wana
taaluma waadilifu na wachapa kazi huku akisisitiza kuwa Msikiti wa Masjid
Shufaa haujafungwa, uko halali hivyo waumini wake waendelee kuswali.
Imam wa Msikiti huo
Mohamed Said ambaye amekubaliana na uamuzi wa Mkuu wa Mkoa Dkt Nchimbi amesema
chuo hicho kinakabiliwa pia na changamoto ya kukosa umeme, maji na Chakula.
Said amesema
anaishukuru kamati ya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wanaopewa hadi kufikia
hapo walipo na kusisitiza kuwa ushirikiano huo umeletwa na uongozi mzuri wa
Mkoa wa Singida.
Jengo la Mbele ni
masjid Shafii na jengo la nyuma ndilo lililokuwa likitumika kama chuo ambacho
mafunzo yanayotolewa hayakufahamika kutokana na kutokuwa na mtaala pia
kutosajiliwa.
Baadhi ya wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa wa Singida wakiwa katika kikao kifupi
kilichotangaza uamuzi wa kukifungia chuo kilichopo katika Masjid Shafii eneo la
Mwaja Singida mapema leo.
Imam wa Masjid Shafii
ulioko Mwaja Singida Mohamed Said akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt Rehema Nchimbi kabla ya chuo
kilichopo chini ya msikiti huo kufungwa.
No comments:
Post a Comment