Kiongozi wa Mbio za Mwenge
wa uhuru Amour Hamad Amour akifungua maji katika bomba wakati wa uzinduzi wa
mradi huo katika kijiji cha Merya Wilayani Singida, pembeni yake Mkimbiza
Mwenge Kitaifa Fredrick Ndahani.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge
wa uhuru Amour Hamad Amour akimtwisha ndoo ya maji moja ya akina mama
waliojitokeza kushuhudia uzinduzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Merya
Wilayani Singida.
Wanawake wa Vijiji
vya Merya na Ikugha katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida wameushukuru Mwenge
wa Uhuru kwa kuwafungulia mradi ambao umewaepusha kutembea umbali mrefu
kutafuta maji ya kutumia ambayo si safi wala salama huku wakiyachangia na
mifugo yao.
Wanawake hao wametoa
pongezi hizo mara baada ya kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Amour Hamad
Amour kufungua mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 49 utakaohudumia
vijiji hivyo ambao umegharimiwa na shirika la saving International, halmashauri
ya Singida pamoja na michango ya wananchi.
Wamesema kabla ya
kupatikana mradi huo wanawake wa vijiji hivyo wamekuwa wakifuata maji umbali
mrefu sana kiasi cha kushindwa kutekeleza shughuli nyingine za kuzalisha mali.
“Tulikua tunatembea
mpaka tunachoka, tunaamua kupumzika njiani kwanza ndio tuendelee na safari ya
kuleta maji nyumbani, yani tunashukuru sana kwakweli”, ameongea Bi Greta Senge
Mkazi wa kijiji cha Ikugha.
Aidha wameongeza kuwa
mradi huo utawapatia maji safi na salama kwakuwa maji waliyokuwa wakiyafuata
umbali mrefu hapo awali yalikuwa machafu na si salama.
“Yani tulikuwa
tunachota maji ambayo unakuta ng’ombe anakunywa hapohapo, wakati mwingine
anajisaidia na inabidi uchote hivyo hivyo, kwakweli tunaushukuru sana mwenge
kutufungulia mradi huu, tulikua tunaumwa matumbo kila mara”, ameongeza Rehema
Lazaro.
Wameongeza kuwa mradi
huo utapunguza magonjwa ya tumbo na macho ambayo yamekuwa yakiwasumbua mara kwa
mara hukua wakiridhia kulipia kiasi cha shilingi 50 kwa lita 20 za maji ili
kupata fedha za kutunza mradi huo.
Kwa upande wake
kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru Amour Hamad Amour ameitaka jumuiya ya
watumia maji ya mradi huo kuutunza mradi huo ili utoe maji kwa wingi na muda
huo kutokanana kuonekana ni hitaji la muhimu.
“Nimefika hapa na
kushuhudia akina mama wengi mnamiminika na ndoo ili mpate maji, hii ni ishara
kuwa mradi huu ni muhimu hivyo basi jumuiya ya watumia maji hakikisheni mda
wote maji yanatoka na sio kupanga masaa ya kutoa maji au mvua ikinyesha tu
mnayafunga, hapana” amesisitiza Amour.
Amesema mradi huo
usimamiwe vizuri kusiwe na upendeleo au ubaguzi wowote kwakuwa maendeleo hayo
hayana ubaguzi wa rangi, dini, itikadi za kichama au makabila.
Amour amesema jumuiya
hiyo ihakikishe miundombinu ya mradi huo inatunzwa ili kuepusha kuwarudisha
akina mama hao katika shida waliyokuwa wakiipata awali huku akiwashauri
kuangalia namna ya kuipatia mifugo maji pamoja na kuweka taratibu nzuri za
mapato na matumizi ya mradi huo.
Wakati huo huo
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amezindua mradi wa umwagiliaji mbogamboga kwa
njia matone wa ekari 25 wenye thamani ya shilingi milioni 326 katika kijiji cha
Msange.
Akisoma taarifa ya
mradi huo Afisa Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Singida Adam Mngale amesema
mradi huo ulianzishwa mwaka 2012 na hadi sasa una wanachama 32 ambao
wananufaika kwa kujiongezea kipato kutokana na kulima misimu miwili yani
kiangazi na masika.
Mngale amesema
malengo ya mradi huo ni kuongeza eneo la uzalishaji hadi kufikia ekari 1400, kupanua
miundombinu ili waweze kutumia kutumia bwawa la suke na lililoko eneo jirani
katika umwagiliaji na kutumia kiwanda cha kusindika mbogamboga kilichoko Msange
kusindika mazao yao.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge
wa uhuru Amour Hamad Amour akitazama vitunguu katika shamba la mboga mboga la
umwagiliaji kwa njia ya matone wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika kijiji
cha Msange Wilayani Singida.
Sehemu ya shamba la
mbogamboga lenye kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone ambapo vitunguu
vinaonekana vimestawi vizuri, shamba hilo lina ukubwa wa ekari 25.
No comments:
Post a Comment