Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa uhuru Amour Hamad Amour akikagua ujenzi wa daraja la Mto Mtoa na
makaravati katika barabara ya shelui-Mtoa-Urughu Wilayani Iramba.
Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa uhuru Amour Hamad Amour akiweka jiwe la msingi ujenzi wa daraja la
Mto Mtoa na makaravati katika barabara ya shelui-Mtoa-Urughu, pembeni yake ni
Mratibu wa mwenge Mkoa Mkoa wa Singida Yusufu Makulo.
Serikali imedhamiria
kuwaunganisha wakulima wakubwa wa mazao ya chakula wa kata tano za Wilaya ya
Iramba kwa kujenga daraja na makaravati manne katika barabara yenye urefu wa
kilomita 38.6 yatakayo gharimu shilingi bilioni 4.1.
Akiweka jiwe la
msingi la ujenzi wa daraja la Mto Mtoa na makaravati katika barabara ya shelui-Mtoa-Urughu
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Amour Hamad Amour amesema serikali
imedhamiria kuwaunganisha wananchi ili wazalishe mazao, waanzishe viwanda kisha
kusafirisha bidhaa.
Amour amesema kwakuwa
barabara hiyo inahudumia wananchi wa kata
za Shelui, Mtoa, Mtekente, Urughu na Ndago wananchi wa maeneo hayo watumie fursa
ya kuwa na barabara nzuri kwa kutengeneza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa
na kisha kusafirisha bidhaa na sio mazao kama mali ghafi.
Amesema kwa kufanya
hivyo wakulima wa mazao wataweza kujiongeza kipato chao kwa kuwa hawatapunjwa
kwa kuuzwa mali ghafi ambayo hupelekwa kwenye viwanda vya nchi nyingine hivyo
barabara hiyo iwe hamasa kwao kuzalisha kwa wingi pamoja na kuanzisha
viwanda kwa wingi.
Mradi huo wa barabara
na makaravati unatekelezwa kupitia mpango wa kuondoa vikwazo kwenye barabara za
vijijini, mpango unaofadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa kushirkiana na
serikali za Uingereza na Ireland Kaskazini.
Kukamilika kwa ujenzi
wa daraja na makaravati hayo kutawezesha barabara hiyo kupitika kwa kipindi cha
mwaka mzima na hivyo kuwanufaisha wakazi elfu 79 wa kata hizo pamoja na
kuwezesha utoaji wa huduma za kijamii katika eneo hilo lenye shule za msingi
29, shule za sekondari 6, zahanati 7 na kituo cha afya kimoja.
Wakati huo huo Kiongozi
wa mbio za mwenge wa Uhuru Amour Hamad Amour amezindua mradi wa ghala la
kuhifadhia chakula katika kijiji cha Nselembwe ambalo litakuwa likihudumia
jamii ya kata za Ulemo,Mgongo, Ntwike, Shelui na Mtoa.
Akifungua ghala hilo
Amour amesema kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka huu ni shiriki kukuza uchumi
wa viwanda kwa maendeleo ya taifa hivyo ujenzi wa ghala ili kuhifadhi mazao unasaidia
wananchi kutoyauza ovyo mazao na kuyahifadhi mahali salama kabla ya kuyachakata
kuwa bidhaa.
Amesema mradi huo
wenye thamani ya shilingi milioni 350 utaweza kuwasaidia wananchi kuhifadhi
mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuwa na kauli moja juu ya bei ya mazao
pia watakua na uhakika wa mazao.
Amour amewasisitiza wananchi
wa kata hizo kuzalisha kwa wingi kwa kuwa sasa wana uhakika wa sehemu salama ya
kutunzia mazao yao ili wasishawishike kuyauza kwa bei ndogo.
Mwenge wa Uhuru ukiwa
Wilayani Iramba umetembelea miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 huku
ukipitia miradi 6 na kuona shughuli 5 katika vijiji 10 na tarafa 4 katika umbali wa km 119.1.
Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa uhuru Amour Hamad Amour akikagua ghala la kuhifadhia mazao katika
kijiji cha Nselembwe Wilayani Iramba Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba
Emmanuel Luhahula.
Mkimbiza mwenge Kitaifa
Fredrick Ndahani akikagua ghala la kuhifadhia mazao katika kijiji cha Nselembwe
Wilayani Iramba wakati Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru Amour Hamad Amour
akizindua ghala hilo, nyuma yake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel Luhahula.
Mwanafunzi
akiwa ameushika kiukakamavu mwenge wa uhuru wakati risala ya utii ya wananchi
wa Iramba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikisomwa, mbele ya mwanafunzi
ni Mkimbiza mwenge kitaifa Fredrick Ndahani na Nyuma ya Mwanafunzi ni Mkimbiza
Mwenge Kitaifa Salome Obadia Mwakitalima.
No comments:
Post a Comment