Thursday, July 20, 2017

SITAVUMILIA HATI CHAFU KATIKA HALMASHAURI YOYOTE MKOANI KWANGU-DKT NCHIMBI.



Mkuu wa Mkoa wa Singia Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na Meya wa Manispaa ya Singida Gwae Chima Mbua kabla ya kuanza kwa baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Kizito Lyampembile akifungua baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Singia Dkt Rehema Nchimbi amesema hatavumilia kuona halmashauri inafanya uzembe na kupata hati chafu ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali kwakuwa itamchafua yeye na taswira ya uongozi wote wa Mkoa wa Singida.

Dkt Nchimbi ametoa kauli hiyo mapema jana wakati wa baraza maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali ambazo amesema hoja nyingi zimetokana na uzembe.

Amesema licha ya kuipongeza Manispaa ya Singida kwa kupata hati safi, uwepo wa hoja umedhihirisha kuwa kuna baadhi ya watendaji wanafanya kazi kwa uzembe na kutofuata taratibu na sheria hivyo wajirekebishe haraka.

Dkt Nchimbi ameongeza kuwa hoja nyingi zinajitokeza kwa kukosa umakini na watendaji kufanya kazi kwa mazoea hali ambayo ikiendelea inaweza kuipelekea manispaa kupata hati isiyoridhisha hivyo kupata hati safi kuwaongezee nguzu ya kuboresha utendaji kazi wao.

Aidha amewashauri wakuu wa idara na watumishi wengine kuitendea haki manispaa yao kwa kuchapa kazi kuwa wadilifu na kufuata sheria kwani wakifanya hivyo wataepuka hoja zisizo za lazima na kuharakisha maendeleo.

Dkt Nchimbi amewasisitizia matumizi ya muda kuwa yenye tija ambapo amelaani kitendo cha kutumia muda mwingi kwenye vikao ambavyo havina tija bali watumie muda kidogo kwenye vikao na muda mwingi kutatua kero za wananchi, huku akiahidi kufuatilia matumizi ya muda unaotumika kwenye vikao.

Ameongeza kuwa watendaji wote wanapaswa kubadilika na kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Hapa kazi tu ili waweze kupunguza hoja na kufuta zile zisizo za lazima.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Lutambi amewaasa watendaji kuitumia vema dhamana ya utumishi wa umma kwa kuhakikisha wanaleta mabadiliko ya kimaendeleo.

Dkt Lutambi ameongeza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kufahamu kuwa jutendaji wao ukilega lega athari yake inamkumba mwananchi kwakuwa atachelewa kupata maendeleo, hivyo bidii katika utumishi umma ni muhimu.

Amewasisitizia kuwa mikakati na malengo ya maendeleo ya kimkoa na kitaifa haitaweza kufikia endapo watendaji hawatakuwa waadilifu na wakiendekeza uzembe hivyo wajitume kwa bidii kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Naye Diwani Viti maalumu Magreth Malecela amemshukuru Mkuu wa Mkoa Dkt Nchimbi kwa kuwapa vyeti ambavyo vilitolewa kwa madiwani wote waliopata mafunzo ya usimamizi wa ruzuku na miradi ya serikali.

Malecela ameongeza kuwa ushirikiano na ushauri wanoaupata kutoka kwa Dkt Nchimbi utaisaidia manispaa kuwa na maendeleo huku akiahidi kwa niaba ya madiwani wenzake kuwa watafuata maelekezo na ushauri kwa manufaa ya manispaa ya Singida.

Baadhi ya Viongozi wa Manispaa ya Singida wakifuatilia baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.
Madiwani wa manispaa ya Singida wakifuatilia baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.


Madiwani wa manispaa ya Singida wakiwa wamesimama kuridhia hoja katika baraza Maalumu la madiwani wa Manispaa ya Singida kujadili hoja za Mkaguzi wa Fedha za Serikali.



No comments:

Post a Comment