Katibu Tawala
Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida Beatus Chowaji akisoma bango mara
baaa ya kuzindua mradi wa Faida Mali unaoshirikiana na shirika la AMDT katika
kuwasaidia wakulima wa Alizeti Singida.
Mkurugenzi wa Shirika
la AMDT Michael Kayombo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Faida Mali wenye
lengo la kuwasaidia wakulima wa Alizeti Singida kulima kibiashara.
Wauzaji wa pembejeo
ambao sio waaminifu wamepewa onyo kali na endapo atabainika yeyote
anayewalaghai wakulima na kuwauzia pembejeo ambazo sio hali hatua kali dhidi
yake zitachukuliwa.
Katibu Tawala
Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida Beatus Chowaji ametoa onyo hilo
wakati akizindua mradi wa Faida Mali unaoshirikiana na shirika la AMDT katika
kuwasaidia wakulima wa alizeti Mkoani Singida ili kulima zao hilo kibiashara
zaidi.
Chowaji amesema
kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya wakulima ambao hukumbana na wauzaji wa
pembejeo ambao sio waaminifu na kuwalaghai kwakuwa wakulima hao hawana elimu na
uelewa hasa wa viuatilifu au mbegu ambazo ni halisi.
Ameongeza kuwa mkono
wa serikali ni merfu na utawabaini popote walipo hivyo waache mara moja kwani
kwa kufanya hivyo wanakirudisha nyuma kilimo cha alizeti ambacho ni tegemeo kwa
ajili ya uchumi wa viwanda Mkoani Singida.
“Singida tuna Viwanda
vya kuamua mafuta ya alizeti vikubwa viwili, vya kati vitatu na vidogo 115 na
kufanya jumla ya viwanda vya alizeti kuwa 120, vyote hivyo vinategemea alizeti
ya mkulima, lakini pia mkulima anakuwa na matarajioa makubwa, hao wauzaji
pembejeo wasio waaminifu hatutawavumilia, tena waache mara moja”, amesisitiza
Chowaji.
Aidha amelipongeza
shirika la AMDT kupitia mradi wa Faida mali kwa kuuchagua Mkoa wa Singida ili
kuboresha kilimo cha alizeti hasa kwa ajili ya mkulima mdogo.
Chowaji amesema
viwanda vya alizeti Mkoani Singida hufanya kazi kwa miezi minane kwa mwaka
badala ya mwaka mzima kutokana na kuwa alizeti inayozalisha bado haitosheleshi
viwanda hivyo kufanya kazi mwaka mzima.
Amesema matumaini
makubwa ya serikali mkoani hapa ni kuwa mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji
wa zao hilo ili kuifanya Singida ya Viwanda kuwa bora zaidi pamoja na
kuliboresha zao lenyewe la alizeti kwa kutumia pembejeo za kisasa zaidi.
Chowaji amewataka
wakulima wote wa alizeti kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga katika vikundi
ili waweze kufikiwa kwa urahisi na kunufaika, pia waache kilimo cha mazoea
kwakuwa alizeti ni biashara kubwa ambayo itawakomboa kiuchumi na kukupa pato la
mkoa wa Singida.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Shirika la AMDT Michael Kayombo amesema shirika hilo kupitia
Mradi wa Faida mali utahakikisha unasaidia upatikanaji wa mikopo kwa wakulima
wadogo wa alizeti Mkoani singida.
Kayombo ameongeza
kuwa mradi utaboresha huduma za ugani kwa kutoa taarifa sahihi na mapema juu ya
kilimo cha alizeti kwa wakulima na taarifa hizo zitatolewa kwa njia ya ujumbe
mfupi wa maneno hivyo kuwafikia mapema.
Amreongeza kuwa
watahakikisha wakulima wanapata soko la uhakika la zao hilo ndani na nje ya
mkoa wa singida pamoja na kuhakikisha bei ya zao hilo ni yenye kumnufaisha
mkulima na sio kumdidimiza zaidi.
Naye Mtendaji Mkuu wa
Chama cha wasindikaji wa Mbegu za alizeti Tanzania Daud Musa Mwasantaja amesema
viwanda vya alizeti bado vina uhitaji mkubwa wa alizeti kwa kuwa viwanda vyao
vimekuwa vikiendeshwa chini ya malengo kutokana na mbegu hizo kuwa chache.
Mwasantaja amesema
wana imani kuwa mraadi wa Faida Mali utasaidia kuongeza uzalishaji wa alizeti
hivyo kuwasaidia kuongeza pia uzalishaji katika viwanda vyao.
Ameongeza kuwa
watatoa ushirikiano wa kutosha na hivyo wakulima wasiwe na wasiwasi walime zao
hilo kwa wingi watapata wateja na kwa bei ambayo ni nzuri.
Nao wakulima
walioshiriki uzinduzi wa maradi huo wamesema mradi huo umekuja muda muafaka
kwakuwa na wao wanatamani kupata faida kutokana na kilimo hicho kwakuwa baadhi
bado wanalima kwa mazoea na kwa kutumia mbegu ambazo hazizalishi kwa wingi.
Baadhi ya wadau
waliohudhuruia uzinduzi wa mradi wa Faida Mali wenye lengo la kuwasaidia
wakulima wa Alizeti Singida kulima kibiashara.
Mkurugenzi wa mradi
wa Faida Mali mkoa wa Singida Tom Silayo akisoma taarifa ya mradi huo kwa
wajumbe waliohudhuria uzinduzi wa mradi utakaowasaidia wakulima kulima alizeti
kibiashara.
Mtendaji Mkuu wa
Chama cha wasindikaji wa Mbegu za alizeti Tanzania Daud Musa Mwasantaja
akiwahakikishia wakulima wa alizeti upatikanaji wa soko katika uzinduzi wa
Mradi wa Faida Mali.
No comments:
Post a Comment