Monday, July 24, 2017

RAIS MAGUFULI KUFANYA ZIARA MKOANI SINGIDA KESHO, ATAZINDUA BARABARA YA ITIGI.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (Picha ya Maktaba).


Sehemu ya Barabara ya Manyoni- Itigi-Chaya itakayozinduliwa kesho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Pius Luhende wakati wa maandalizi ya mapokezi ya Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi Mkoani Singida kesho Julai 25 ambapo atazindua barabaraya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa Kilomita 89.3.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema Rais Magufuli anatarajiwa kufanya uzinduzi wa barabara hiyo katika eneo la NjiaPanda, Itigi na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.

“Napenda kuwataarifu wananchi wote kuwa rais wetu Mpendwa atatuzindulia barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, hivyo basi tujitokeze tukamshukuru kwakutuletea maendeleo wana Singida, ametufanyia jambo kubwa sana, shukrani zetu hiyo kesho pale njiapanda zitaendelea kumpa hamasa ya kutuletea maendeleo zaidi” amesema Dkt Nchimbi.

Dkt Nchimbi ameongeza kuwa wananchi wajitokeze kumlaki na kutoa pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuokoa rasilimali za nchi hasa katika sekta ya madini ambayo Mkoani Singida pia yanapatikana kwa wingi na kwakuwa jitihada hizo zimelenga kuwanufaisha wana Singida na watanzania wote.

“Rais Magufuli ameokoa rasilimali nyingi za taifa na anapambana usiku na mchana kuzilinda ili watanzania hasa wanyonge wafaidike, wengi tumekuwa tukifurahishwa sana na jitihata hizo, hivyo basi kesho tuonyeshe upendo wetu na shukrani zetu kwake”, ameongeza Dkt Nchimbi.

Aidha amesema barabara itakayozinduliwa kesho na Rais Magufuli ni kiunganishi muhimu kati ya Mkoa wa Singida na Tabora na hivyo kurahisha usafirishaji tofauti na ilivyokuwa kabla ya kujengwa, pia itarahisisha kwa wasafirishaji wa mikoa ya Singida na maeneo ya jirani kuelekea Mkoa wa Tabora mpaka Kigoma.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya ugeni wa Rais Magufuli Mkoani Singida siku ya kesho.

No comments:

Post a Comment