Mzee maarufu na
mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi akichangia hoja katika semina ya
kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
Mratibu wa Mradi wa
Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman akizungumza na washiriki wa semina ya
kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
Elimu sahihi juu ya
madhara ya ukeketaji ya muda mfupi na mrefu inatakiwa itolewe kwa jamii kabla
ya kuwachukulia hatua baadhi yao wanaoendelea kufanya vitendo vya ukeketaji
licha ya uwepo wa sheria kali.
Rai hiyo imetolewa
mapema leo na Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman
katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani
Singida, kwa ushirikiano wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida na mradi
huo kwa ufadhili wa shirika la WAAF-Japan.
Mratibu huyo amesema
nguvu ya sheria itasaidia kuondoa ukeketaji endapo wananchi wengi watakuwa na
uelewa wa kutosha juu ya madhara ya ukeketaji na kuamua kwa hiyari kuachana na
mila hiyo.
“Sheria isiwe nguvu
pekee ya kupambana na ukeketaji, tukifanya hivyo itafikia kipindi tutakwama kwa
kiasi kikubwa kwa kuwa watu wataendelea kukeketa kwa kificho ili wasikamatwe,
lakini kila mwana jamii akiwa na elimu ya kutosha ya madhara hayo, nguvu ya
sheria itatumika tu kwa wachache watao kaidi”, amesisitiza Nasra.
Ameongeza kuwa
Watendaji wa kata na vijiji wana uwezo mkubwa wa kubadilisha mtazamo na mila ya
ukeketaji kwa kuelimisha wananchi wao hasa baada ya semina zinazoandaliwa na
miradi au mashirika Fulani kwakuwa zinawajengea uwezo ili waweze kutoa elimu
sahihi na mbinu za kuelimisha.
Nasra amesisitiza kuwa
jukumu la elimu lisiachwe kwa sekta binafsi kama mradi wake wa WOWAP pekee bali
liwe jukumu la jamii nzima huku akifafanua kuwa elimu inayotakiwa kutolewa ni
ile inayoelezea madhara ya ukeketaji na sio kuwakataza kwa kigezo cha kutii
sheria pekee.
Naye Afisa Maendeleo ya
Jamii kata ya Msange Magni Oisso amesema katika kata hiyo ukeketaji
umekufanyika kwa siri sana kwa kuogopa mkono wa sheria huku wahanga wakiwa
watoto wachanga na wale waliomaliza kliniki.
Oisso amesema kumekuwa
na usiri mkubwa huku wakeketaji wakibadili mbinu namna za kujificha
wasigundulike kwa jamii ambayo elimu imeanza kuwafikia baadhi yao.
Aidha amependekeza kuwa
ili kukomesha ukeketaji moja ya njia ni kutoa elimu katika vituo vya kutolea
huduma za uzazi na mtoto ili mtoto aweze kunusurika pia elimu itolewe shuleni
kwa ngazi zote kuanzia darasa la awali hadi la saba.
Akichangia mada katika
semina hiyo mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi amesema
elimu ni bora zaidi kuliko kuwaogopesha wanajamii kwa kutumia sheria kwakuwa
watatafuta namna ya kutekeleza azma yao kwa usiri ili kukwepa mkono wa sheria
na sio kuacha.
Greta ameongeza kuwa
kwa sasa kutokana na kuwa wakeketaji wamebainika kuwa wanakeketa watoto
wachanga na hugundulika wakienda kliniki baadhi yao wanabadili mbinu na
kusubiri mtoto amalize kliniki ndipo anakeketwa.
Naye Mzee wa Kimila
Hosea Mnyambi amesema yeye amekulia katika familia ya wakeketaji na wamekuwa
wakirithishwa mbinu za ukeketaji kizazi hadi kizazi ila kutokana na kuwepo kwa
sheria, dini kuhubiri madhara ya ukeketaji, mila hiyo wameiacha.
Amesema wachache
wanaoendelea kufanya vitendo hivy o ha wanawake wamekuwa wakifanya kwa usiri
mkubwa huku akina baba wakiwa hawana taarifa ya kinachoendelea na endapo mtoto
anafariki hudanganywa ugonjwa uliopelekea kifo cha mtoto.
Mzee Mnyambi amesema
elimu iendelee kutolewa hasa kwa kutumia vyombo vinavyoaminika mfano vyama vya
siasa, dini na vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kuiweka agenda ya
ukeketaji kwa vikao vya Kata na vijiji.
Semina ya kupinga
ukeketaji Kata ya Msange imefanywa na mradi wa WOWAP kwa ushirikiano wa maafisa
ustawi wa jamii mkoa wa Singia kwa watendaji wa kata na vijiji, watoa huduma za
afya, polisi, waalimu, wawakilishi wa viongozi wa dini, maafisa ustawi wa jamii
na maendeleo ya jamii, wazee maarufu na wa kimila ili wawe mabalozi wa
kusambaza elimu hiyo kwa jamii inayo wazunguka.
Afisa Maendeleo ya
Jamii kata ya Msange Magni Oisso akichangia hoja katika semina ya kupinga
Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
Washiriki wa semiana ya
kupinga ukeketaji iliyoandaliwa na Mradi wa WOWAP wakifuatilia kwa umakini
filamu fupi ya Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi
akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya
Msange Wilayani Singida.
No comments:
Post a Comment