Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza katika baraza maalumu la madiwani wa
halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji
Jumanne Mtaturu na Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ikungi Ally Mwanga.
Watumishi wa halmashauri
ya Wilaya ya Ikungi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi
katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu
wa Hesabu za Serikali.
Watendaji wa halmashauri
za wilaya na manispaa wamekuwa ni kiwanda cha kutengeneza hoja za mkaguzi na
Mthibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kwa kukosa umakini, uaminifu, uwajibikaji
na kutokuzingata sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema ameyasema hayo mapema leo katika baraza maalumu la madiwani
wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa kujadili hoja 80 za Mkaguzi na
Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2015/16 licha ya halmashauri hiyo
kupata hati safi.
Dkt Nchimbi amesema
wamekuwa ndio wazalishaji wakubwa wa hoja tena hoja zenyewe zikionyesha udhaifu
wao wa kutotimiza wajibu wao huku akiwaeleza kuwa hoja hizo zinaonyesha kuwa
kuna udhaifu katika utendaji wao.
“Hoja hazitengenezwi
na madiwani, ni nyinyi watendaji kwa uvivu, mnashindwa kufuata taratibu hadi
mnazalisha hoja, mmekuwa ni kiwanda na kiwanda chenyewe kibaya cha kuzalisha
hoja, badilikeni”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha amewataka
madiwani kuwa wasimamizi wa miradi na shughuli za serikali pamoja utendaji wa
watumishi ili wasiendelee kuzalisha hoja kwakuwa utendaji ukilega lega unawaathiri
wananchi ambao ndio wamewaamini ili wawakilishe.
Dkt amewasisitiza
kuwa watumishi wengine huja na kuondoka lakini madiwani ndio wazawa hivyo
maendeleo yao wanapaswa kuyasimamia kwa nguvu zote wakishirikiana na watumishi
pamoja na kuwashauri viongozi wa halmashauri katika kuboresha utendaji.
Amewataka madiwani pia
kuwasimamia watumishi wasijiingize kwenye ushabiki wa kisiasa na kupandikiza
chuki kwa wananchi bali wao wajikite kwenye kuhudumia wananchi na kuwaachia
siasa madiwani na wanasiasa wengine.
Naye Katibu Tawala
Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi ameishauri halmashauri hiyo kuhakikisha
wanafunga hoja hizo ili halmashauri hiyo iendelee kupata hati safi.
Dkt Lutambi amesema
watumishi wasijisahau na kufanya kazi kwa mazoea bali wachape kazi kwa bidii,
kwa ubunifu na kwa kufuata taratibu ili kutoa huduma nzuri kwa wananchi na kuepuka kuzalisha hoja.
Ameongeza kuwa taifa
na halmashauri ya Ikungi inazo rasilimali za kutosha, jukumu la watumishi ni
kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi wote bila upendeleo au
kuzifuja.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka amesema yeye na
watendaji wake wote watahakikisha wanazingatia ushauri na maelekezo
yaliyotolewa katika baraza hilo ili hoja zifutwe.
Turuka ameongeza kuwa
atahakikisha halmashauri ya Ikungi haipati hoja nyingi na itaendelea kupata
hati safi kama ambavyo imekuwa ikipata kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Amesema kuwa atashirikiana
na madiwani katika kuhakikisha halmashauri inakusanya mapato yake vizuri na kuongeza
vyanzo vingine vya mapato ili waweze kutoa huduma kwa wananchi kwa ajili ya
maendeleo ya Ikungi na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka akizungumza katika baraza
maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali.
Madiwani wa
halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika baraza maalumu la madiwani la kujadili
hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
No comments:
Post a Comment