Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwenyekiti wa halmashauri ya itigi Ally
Minja cheti cha mafunzo ya usimamizi wa miradi ya serikali.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na watumishi, watendaji na madiwani wa
halmashauri ya wilaya ya Itigi (hawapo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amewataka watumishi kupunguza malalamiko na
kuelekeza nguvu zao katika kuhudumia wananchi kwa mambo yanayoonekana kwa
macho.
Dkt Nchimbi ameyasema
hayo katika baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya Itigi ambapo amewataka
watumishi na watendaji kupunguza muda wa vikao ili waende kuwatumikia wananchi.
Amesema kumekuwa na
tabia ya kulalamika ambayo pia inaambukiza kwa watumishi na watendaji wengine badala
ya kutoa suluhisho kwa changamoto ambazo zitawasaidia wananchi.
Dkt Nchimbi ameongeza
kuwa watendaji na madiwani wasitumie muda mwingi ofisini pamoja na kusubiria
taarifa za makaratsi ambazo hazina uhalisia wa matukio na hali halisi
inayoendelea kwa wananchi.
Ameongeza kuwa
utendaji wa mazoea na kulalamika ndiyo husababisha halmashauri kupata hoja za
mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali licha ya kuwa na wataalamu wa kutosha
ambao wana vyeti halisi.
Dkt Nchimbi amesema
watumishi, watendaji na madiwani wanapaswa kuzingatia kuwaheshimu, kuwatambua,
kuwathamini na kutowadanganya wananchi katika kuwatumikia kwakuwa wananchi wana
uelewa wa kutosha juu ya mambo mbalimbali.
Aidha katika baraza
hilo maalumu, madiwani wamepokea hoja 37 za mkaguzi na mthibiti wa hesabu za
serikali ambapo halmashauri ya itigio imepata hoja 37 na hatiu inayodhirisha.
Dkt Nchimbi
amewasisitiza watumishi, madiwani na viongozi wa halmashauri ya Itigi kufanya
kazi kwa kuzingatia uadilifu na uaminifu ili waweze kuepuka kutengeneza hoja.
Ameongeza kuwa madiwani
wasimamie kwa umakini miradi na shughuli za serikali ili thamani ya fedha iweze
kuonekana kwa miradi hiyo huku akiwashauri kumtumia mkaguzi wa ndani kama kioo
cha kuangalia dosari zao na kuzirekebisha mapema.
Kwa upande wake
Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Anna
Kakunguru ameishukuru halmashauri ya Itigi
kwa ushirikiano na kuwaasa wasiwe wataalamu wa kujibu hoja bali wawe
wataalamu wa kuzuia hoja.
Kakunguru amesema ofisi
ya Mkaguzi wa nje itaendelea kushirikiana na halmashauri kwakuwa kazi yake
kubwa ni kusimamia sheria zinafuatwa bila kupindishwa.
Naye Katibu Tawala wa
Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi amewasa watendaji kuendelea kufuata maadili
ya utumishi wa umma pamoja na maadili na maelekezo wanayopewa ili kuboresha
utendaji wao.
Lutambi ameongeza
kuwa kukiuka maadili na kutowahudumia wananchi ipasavyo ni kitengo cha
kurudisha nyuma jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania za
kuwakomboa wananchi kiuchumi.
Awali katika baraza
hilo Mkuu wa Mkoa wa Singida ametoa vyeti kwa madiwani wa halmashauri ya Itigi
baada ya kuhitimu mafunzo ya kuibua na kusimamia miradi na ruzuku za serikali.
Baadhi ya watumishi
wa halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi.
Mkaguzi wa Nje wa
Hesabu za Serikali Anna Kakunguru
akizungumza katika baraza maalumu la halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
No comments:
Post a Comment