Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza katika mkutano wa uelimishaji juu ya
mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya mda mrefu
uliofanyika Mkoani Singida.
Wajumbe wa mkutano wa
uelimishaji juu ya mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya
mda mrefu uliofanyika Mkoani Singida, wa kwanza ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Itigi Pius Shija Luhende pembeni yake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Singida Bravo Lyampembile.
Serikali imerudisha
utaratibu wa kugawa vyandarua vyenye viuatilifu kwa akina mama wajawazito na
watoto ambao wanapatiwa chanjo ya surua kupitia vituo vya kutolea huduma za
afya ya uzazi na mtoto ambapo utaratibu huo utaanza rasmi mwezi Agosti mwaka
huu.
Afisa Muuguzi kutoka
Wizara ya Afya Epifania Malingumu amewaambia wajumbe wa mkutano wa uelimishaji
juu ya mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya mda mrefu
kuwa kwa sasa vyandarua hivyo havitapatikana katika maduka kama ilivyokuwa
kwenye utaratibu wa ‘hati punguzo’ ya zamani.
Malingumu amesema
hapo awali vyandarua vyenye viuatilifu vilikuwa vikitolewa kwa mfumo wa hati
punguzo ambapo mama mjamzito alikuwa anatakiwa kutafuta maduka ya mawakala wa
vyandarua hivyo mara baada ya kupatiwa hati hiyo katika vituo vya kutolea
huduma ya afya ya uzazi.
“Utaratibu wa hati
punguzo wa zamani ulikwisha muda wake mwaka 2014, akina mama walikuwa wanapata
changamoto katika kutafuta mawakala wa vyandarua lakini utaratibu mpya ni
kwamba mama mjamzito au mwenye mtoto mchanga atapewa chandarua chenye viuatilifu
palepale atakapokuwa katika vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi” amesema.
Ameongeza kuwa mama
atapewa chandarua katika hudhurio la kwanza la kliniki ambapo takwimu
zinaonyesha kuwa asilimia 98 ya wajawazito huhudhuria kliniki angalau mara moja
pia vyandarua hivyo vitatolewa kwa idadi ya watoto ambao mama atakua amejifungua
kwa wakati huo.
Kwa upande wake
Mratibu wa zoezi la ugawaji vyandarua nchini Yusufu Mwita amesema vyandarua
vyenye viuatilifu ni nyenzo mojawapo ya kupambana na ugonjwa wa maralia endapo
kila mwananchi atazingatia kuvitumia kwa ufanisi.
Mwita amesema kwa
mkoa wa Singida kumekua na ongezeko la maambukizi ya Ugonjwa wa maralia kutoka asilimia
0.2 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 5.5 kwa mwaka 2016 licha ya vyandarua
954,644 kugawiwa mkoani hapa kwa mwaka 2016.
Ameongeza kuwa
mkakati wa ugawaji vyandarua umelenga kuwafikia asilimia 85 ya watanzania wote
ifikapo 2025 na kuutokomeza ugonjwa wa maralia kwa kushirikisha mbinu
mbalimbali ikiwemo kupulizia dawa ya ukoka ili kuthibiti mazalia ya mbu pamoja
na kuhakikisha matibabu sahihi ya ugonjwa wa maralia yanatolewa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema Maralia inakuwepo kutokana na kwamba Mkoa wa
Singida sio kame una maji ya kutosha hivyo kusababisha mbu kuzaliana kwa wingi.
Dkt. Nchimbi amesema
mikakati iliyopo ni mizuri ila inatakiwa iende sambamba na mikakati mingine ya
kupambana na ugonjwa wa maralia kwa kuwa ni ugonjwa ambao hupoteza nguvu kazi
ya taifa.
Maafisa kutoka wizara
ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto wakiutambulisha mkoani
Singida mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya mda mrefu.
Mratibu wa ugawaji
Vyandarua kutoka Mkoa wa Njombe Mwamaka Assey akieleza uzoefu wake na mbinu
bora katika ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu.
No comments:
Post a Comment