Afya ya mtoto Mwenge aliyenusurika kifo baada ya kutumbukizwa chooni na kukaa humo kwa zaidi ya saa 14 kabla ya kuokolewa akiwa hai, inaendelea kuimarika huku akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Kiomboi Wilayani Iramba.
Mtoto Mwenge alitupwa
chooni na mama yake mzazi Winfrida Lori (23) mwanafunzi katika Chuo cha Uuguzi
cha Kiomboi Wilayani Iramba ambapo mama
huyo amekiri kujifungua mtoto huyo wa
kiume katika Kijiji cha Luono Julai 3, saa mbili usiku kisha kumfunga vitambaa
mdomoni na kumtumbukiza chooni.
Muuguzi Mkuu wa
Hospitali ya Kiomboi Regina Alex amesema afya ya Mtoto Mwenge inaendelea
kuimarika pamoja na hali ya mama mzazi wa mtoto huyo pia inaimarika tofauti na
hapo awali ambapo alikuwa dhaifu na kushindwa kumnyonyesha mtoto.
“Winifrida alikuwa
hawezi kumyonyesha mtoto Mwenge hapo mwanzoni lakini sasa hivi anamnyonyesha
vizuri na maziwa yanatoka ya kutosha, Mtoto mwenge ana hali nzuri na sasa
amefikisha uzito wa kilogramu 2.9 hali ambayo inaridhisha kwakweli”, ameeleza
muuguzi huyo.
Muuguzi Regina ameongeza
kuwa licha ya mama wa mtoto Mwenge kuwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi,
ameendelea kumhudumia mtoto wake vizuri na kwa upendo hali inayosababisha mtoto
Mwenge kupata nafuu kwa uharaka.
Kwa upande wake Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amempa jina mtoto huyo la Mwenge
amesema kuwa jina hilo litamfutia mtoto huyo majeraha ya kutupwa chooni na kuwa
ishara ya kujiamini, kujipenda, kujithamini na kumpa matumaini kama ambavyo
mwenge wa huru umekuwa ukifanya.
Dkt Nchimbi amesema
mwenge wa uhuru umekuwa ishara ya kuleta matumaini kwa waliokata tamaa, upendo
penye chuki na heshima penye dharau na hivyo kitendo cha mama kumtupa mtoto ni
kukosekana kwa amani, upendo na heshima katika maisha ya mama huyo.
Ameongeza kuwa anamtakia
kila la heri mtoto Mwenge ili atakapokuwa alete heshima, upendo na amani katika
maisha yake na ya wazazi wake huku akifuta kumbukumbu mbaya ya maisha yake
wakati wa kuzaliwa.
Wakati huo huo Dkt
Nchimbi amewaasa wazazi na walezi kuwapa majina mazuri watoto wao kwakuwa
majina huwa ni sehemu muhimu ya maisha ya watoto wao na hutafsiri maisha ya
baadaye.
Dkt. Nchimbi amesema jina
linapaswa liwe na maono mazuri kwakuwa ndio hayo yataambatana katika maisha
yake lakini jina lenye baya huleta mambo mabaya katika maisha ya mtoto.
No comments:
Post a Comment