Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akishirikiana na wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) na Askari wa Magereza kushusha madawati yalitolewa na Bunge.
Madawati hayo 2579 yanapelekwa katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Askari wa Magereza
wakipanda moja ya magari ya JWTZ na kusaidia kushusha sehemu ya madawati 2579
yaliyopokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa niaba ya mikoa ya Arusha, Manyara
na Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi leo ampokea madawati 2579 kutoka kwa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Akipokea madawati
hayo yaliyosafirishwa katika magari 19 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
Dkt Nchimbi amelipongeza jeshi hilo kwa uzalendo huo wa kuhakikisha mali za
umma zinafika Singida kwa ajili ya kuanza kusambazwa katika halmashauri husika
zikiwa salama na katika hali nzuri.
Dkt Nchimbi amelipongeza
Bunge kwa uzalendo wa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt John Pombe Magufuli katika kuhakikisha sekta ya elimu inaboreka nchini ili kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati na
wa viwanda.
Amesema madawati hayo
yataongeza motisha kwa wanafunzi kujisomea kwakuwa mazingira yatawawezesha
kuandika na kusoma kwa ufanisi zaidi.
Aidha Dkt Nchimbi
amezitaka halmashauri zitakazopokea madawati hayo kuhakikisha wanayatunza ili
yadumu na kuwanufaisha wanafunzi kwa muda unaistahili.
“Madawati na yenyewe
yanahitaji ukarabati, sio kwakuwa mmepewa basi muyaache tu, hapana, ukiona ubao
unalegea kidogo basi hakikisha unarekebisha na sio kuanza kusubiri waliotupatia
ndo waturekebishie”, amesema na kuongeza kuwa
“Ili madawati haya
yadumu waalimu na wanafunzi kwa pamoja wahakikishe wanayatunza vizuri, hasa
walimu wasimamieni wanafunzi na muaelekeze namna ya kuyatunza kwakuwa hii ni
mali yetu sote”, Amesisitiza.
Aidha Dkt Nchimbi
ameongeza kuwa mkoa wa Singida uko tayari kupokea vifaa na mambo mbalimbali ya
kitaifa kutokana na kuwa katikati mwa Tanzania hivyo kuwezesha usambazaji kwa
mikoa mingine kuwa rahisi.
“Tunakaribisha taasisi,
mashirika, na hata serikali kuu kama kuna vifaa vingine leteni Singida ni
katikati na usambazaji utakuwa ni rahisi, lakini pia hata shughuli zozote za
kitaifa mkoa wa Singida uko tayari kabisa kuzipokea” amesema Dkt Nchimbi.
Kwa upande wake Afisa
Elimu Vifaa na Takwimu wa halmashauri ya
Wilaya ya Meru Frank Paul Mwambachi amelishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano
kwa kuwapatia madawati ambapo halmashauri yake imepata madawati 400.
Mwambachi amelishukuru
JWTZ kwa kuyasogeza madawati jirani na
halmashauri yake hivyo itakuwa rahisi na salama zaidi kwake kuyasafirisha na
kuyafikisha yakiwa katika hali nzuri na kwa uharaka zaidi.
“Madawati 400 wakikaa
wanafunzi watatu watatu ina maana ni wanafunzi 1200 wamenufaika, kwakweli
tunalishukuru sana bunge kwa uzalendo wao, pia jeshi limetusaidia sana kuyaleta
madawati yetu Singida ambapo ni jirani” amesema Mwambachi.
Aidha ameongeza kuwa
madawati hayo yataboresha mazingira ya ufundishaji na ya kujifunzia hivyo
halmashauri itahakikisha wanayatunza ili wanafunzi wanufaike kwa kipindi kirefu.
Afisa Elimu Vifaa na
Takwimu wa halmashauri ya Wilaya ya Meru
Frank Paul Mwambachi akisaidiana na askari wengine kubeba madawati waliyopatiwa
na Bunge ambapo halmashauri yake imepewa madawati 400.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimpongeza kwa furaha mmoja wa mwanajeshi
aliyehusika kusafirisha Madawati 2579 yaliyotolewa na bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro. Madawati hayo
yamefikishwa Singida kwa ajili ya urahisi wa kuyasambaza katika mikoa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akipokea kwa furaha moja ya magari ya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyokuwa yamebeba Madawati hayo 2579 yanapelekwa
katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro. Madawati hayo yametolewa na
bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment