Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na fundi anayejenga mnara wa kuweka
tanki la maji la lita elfu 10 katika kijiji cha Ghalunyangu, Wilayani Singida.
Mhandisi wa Maji Mkoa
wa Singida Mhandisi Lydia Joseph (aliyeinama) akikagua mabomba yatakayotumika kupeleka
maji kwenye vituo vitatu vya kuchotea maji katika kijiji cha Ghalunyangu,
Wilayani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amewapongeza wana kijiji cha Ghalunyangu kilichopo kata
ya Makuro Wilayani Singida kwa uzalendo wa kujitolea nguvu kazi ya kuchimba
mtaro wenye urefu wa mita 670 katika mradi wa maji kijijini hapo.
Dkt Nchimbi ametoa
pongezi hizo mara baada ya kushuhudia mtaro huo utakaopitisha maji kutoka katika
chanzo cha maji hadi katika tenki la ukubwa wa lita elfu 10 na kuelekea katika vituo
vitatu vya kuchotea maji ikiwa ni jitihada za kufanikisha ukarabati wa mradi wa
maji kijijini hapo.
Amesema “nguvu ya
kuchimba mtaro huu haitaenda bure, tuna uhakika maji yatafika katika vituo
hivyo vitatu kwa kuanzia ili kuwaepusha kuendelea kuchota maji katika bomba
moja lililopo eneo la chanzo cha maji”.
Dkt Nchimbi ameongeza
kuwa, “uzalendo huu usiishie kwenye kuchimba mtaro tu, nawaomba mtoe ushauri na
mapendekezo ili ukarabati wa mradi huu uwe wa ufanisi mkubwa, na hata mkiona
mambo yanaenda ndivyo sivyo toeni taarifa mapema, lakini nina imani na
halmashauri ya Singida, itatekeleza kwa ufanisi mradi huu kwa manufaa yenu wana
Ghalunyangu”.
Aidha amewataka wana
kijiji hao kuwa walinzi wa miundo mbinu ya mradi huo pamoja na kutunza chanzo
cha maji hasa kwa kuongeza eneo la hifadhi ya chanzo cha maji kutoka mita 60
mpaka mita 100 na kupanda miti ya kutosha katika chanzo hicho.
Kwa upande wake
Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Edward Kisalu amesema
ukarabati wa mradi huo wa maji unatokana na fedha za malipo kwa matokeo jumla
ya shilingi milioni 37 walizopatiwa kutokana na kutekeleza vizuri miradi ya
maji Wilayani humo.
Kisalu amesema
halmashauri iliamua kutumia fedha hizo kukarabati mradi wa maji katika kijiji
hicho kwa kuwa ni mradi pekee ambao unahudumia wakazi zaidi ya elfu mbili huku ukiwa
umechakaa kutokana na mashine ya kusukuma maji ya mradi huo kuwa na zaidi ya
miaka kumi toka inunuliwe.
Amesema fedha hizo
zitatumika kununua mashine mpya ya kusukuma maji, kununua tenki la kuhifadhia
maji lenye ujazo wa lita elfu 10, ujenzi wa mnara wa kuhifadhia tenki, mabomba
ya kupitishia maji pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji.
Kisalu amefafanua
kuwa kutokana na fedha hizo kutotosheleza kukamilisha kazi zote ikiwemo
uchimbaji wa mitaro wanakijiji waliamua kwa pamoja wajitolee nguvu kazi zao
kuchimba mtaro huo bila malipo yoyote ili ukarabati wa mradi ufanikiwe kwa
uharaka zaidi.
Ameongeza kuwa licha
ya kuwepo kwa tanki lenye ujazo wa lita elfu 90 kijijini hapo, mabomba ya
kupeleka maji katika tanki hilo yamekatika hivyo halmashauri kwenye bajeti ya
mwaka 2017/2018 imetenga shilingi milioni 300 za ukarabati mkubwa wa kupeleka
maji katika tenki hilo na kuongeza vituo vya kuchotea maji hivyo kufuta kabisa
kero ya maji kijijini hapo.
Kwa upande wao
wanakijiji cha Ghalunyangu wamempongeza Dkt Rehema Nchimbi kwani amekuwa Mkuu
wa Mkoa wa Kwanza kufika kijijini hapo hali iliyowapa faraja kubwa na ari zaidi
ya kujitolea katika miradi ya maendeleo.
Wanakijiji hao licha
ya kuwa na itikadi tofauti za kichama kwa kauli moja wamesema wana imani kubwa
sana na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli
kwakuwa matokeo chanya yanaonekana na sio maneno tu.
Wamesema wana imani na
Rais Magufuli sio tu kwenye miradi ya maji kuwa itatekelezwa vizuri bali hata
miradi mingine ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara ambayo tayari
mkandarasi ameanza kazi ya ukarabati wa barabara kijijini hapo.
Naye Mhandisi wa Maji
Mkoa wa Singida Mhandisi Lydia Joseph amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha
2016/17 halmashauri tatu kati ya saba Mkoani Singida zimepokea fedha za malipo
kwa matokeo ambapo halmashauri hizo ni Mkalama, Manyoni na Halmashauri ya
Wilaya ya Singida.
Mhandisi Lydia
amesema halmashauri hizo zimepata fedha hizo kutokana na kazi nzuri ya kuwasilisha
taarifa za miradi ya maji kwa wakati na mfululizo hivyo Serikali kupitia Wizara
ya Maji na Umwagiliaji imezipatia fedha hizo kama motisha.
Ameongeza kuwa
halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imepatiwa shilingi milioni 16.6, halmashauri
ya wilaya ya Mkalama shilingi milioni 20.1 na halmashauri ya wilaya ya Singida
shilingi milioni 37.8.
Aidha Mhandisi Lydia
amezisisitizia halmashauri zilizopokea fedha hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa
ambayo ni kukarabati miradi ya maji iliyopo vijijini, kuanzisha na kuimarisha
jumuiya za watumia maji pamoja na kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.
Wanakijiji cha
Ghalunyangu wakichota maji katika bomba pekee lililopo katika chanzo cha maji
na maradi wa maji kijijini hapo. Fedha za malipo kwa matokeo zimeelekezwa
kijijini hapo ili kujenga vituo vitatu vya kuchotea maji kwa kuanzia ikiwa
vituo vingine vitajengwa hapo baadaye.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na wana kijiji cha Ghalunyangu, Wilayani
Singida waliokusanyika katika chanzo cha maji na eneo ulipo mradi wa maji
kijjini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza wanakijiji cha Ghalunyangu, Wilayani
Singida (hawapo pichani) katika mkutano wa kijiji.
No comments:
Post a Comment