Friday, July 28, 2017

IGP SIRRO ALIPONGEZA JESHI LA POLISI MKOA WA SINGIDA.Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro akipiga saluti wakati wa kukagua paredi ya jeshi la polisi iliyoandaliwa kwa ajili yake mapema leo kwenye viwanja vya kambi ya FFU mjini hapa.

Mkuu wa Jeshi la Polisi  Nchini IGP Simon Sirro akikagua baadhi ya askari wa jeshi la polisi  mjini  Singida leo wakati wa paredi ya polisi iliyoandaliwa kwa ajili yake.
 
Mkuu wa Jeshi la polisi nchini (IGP), Simon Sirro amelipongeza jeshi la polisi Mkoani Singida kwa juhudi zake za kupunguza matukio ya uhalifu yakiwemo ya utekeji wa magari kwa kiwango kikubwa.

IGP  Siro ametoa pongezi hizo  leo asubuhi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  kweye viwanja vya kambi  ya kikosi  cha kuzuia fujo (FFU) mjini  hapa.

Amesema matukio ya uhalifu mbalimbali Mkoani Singida yamepungua kwa kiwango kikubwa kwa  sasa, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Hatua hii  inachangia  uwepo  wa amani  na utulivu kwa  wananchi  wa  Mkoa wa Singida hivyo  kutoa fursa   kuweza  kujiletea maendeleo yao, ya mkoa na  taifa   kwa ujumla” amesema.

IGP Siro  amesema  mafanikio  hayo yamechangiwa   na wananchi kwa kiwango  kikubwa  kwa kutoa ushirikiano  kwa jeshi la polisi. 

Akifafanua amesema wananchi wamekuwa wakitoa  taarifa sahihi na kwa wakati kwa jeshi la polisi  pindi wanapobaini  dalili  ama  matukio ya kihalifu.

“Kwa sasa wananchi na hata ninyi waandishi  wa habari mnatupa  ushirikiano  mzuri sana. Ushirikiano huu unachangia  kazi zetu kuwa nyepesi na za mafanikio makubwa. Sasa  hivi  kule Kibiti mkoani Pwani, wananchi wanatusaidia mno taarifa  zinazohusu  mauaji ya watu  wasiokuwa  na hatia”, amefafanua zaidi.

IGP Sirro amesema Tanzania inaonewa wivu na nchi jirani kwa namna inavyodhibiti matukio ya kihalifu na kupelekea nchi kuendelea kudumisha amani na utulivu.

Aidha Mkuu huyo  wa jeshi la polisi ametumia fursa hiyo  kuwaomba wananchi  waendelee  kushirikiana na jeshi hilo kufichua  baadhi ya watu wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya kihalifu ili waweze kuchukuliwa  hatua stahiki.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada kukagua askari polisi waliokuwa kwenye paredi kwenye viwanja vya kambi ya  FFU mjini hapa.

Picha/Habari na Gasper Andrew.

No comments:

Post a Comment