Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akisisitiza jambo katika baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Mkurugenzi
wa halmashauri ya Wilaya ya Singida Rashid Mandoa ameagizwa kuhakikisha ofisi
za halmashauri hiyo zinahamia ndani ya eneo la halmashauri hiyo na kutoka
walipo sasa katika manispaa ya Singida.
Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo jana wakati akikabithi
vyeti kwa madiwani wa halmashauri ya Singida walipohitimu mafunzo kuhusu
jitihada za jamii kupitia mbinu shirikishi ya fursa na vikwazo kwa maendeleo
iliyoboreshwa na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Dkt.
Nchimbi amesema endapo mkurugenzi atahamishia ofisi na watendaji katika
halmashauri yake watapata ubunifu wa kutatua shida na kero za wananchi na hivyo
kuiendeleza halmashauri.
“Ukikaa kwenye
nyumba inayovuja ndipo utapata akili na ubunifu wa kutatua changamoto hiyo, ukiangaia
wanufaika wa Tasaf wameweza kufanya mambo mazuri kwa pesa kidog waliyonayo, mkurugenzi
uige mfano huo, mhamie katika halmasahuri yenu, wananchi hawafurahii kuwaona
ninyi na watendaji wengine mkiishi manispaa” amesisitiza Dkt. Nchimbi.
Ameongeza
kuwa kusitasita kwao kutohamia katika halmashauri yao kutasababisha halmasahuri
hiyo ikavunjwa na hivyo kukosa ajira kwa watumishi huku akiwaeleza madiwani
kuwa wataponzwa wa kukosa kura katika uchaguzi ujao kwani wananchi wangependa
kupata huduma kwa ukaribu.
Dkt.
Nchimbi amesema kuhusu makao makuu ya halmashauri hiyo baraza la madiwani litachagua
makao makuu yao huku akishauri wazingatie eneo ambalo litafaa kwakuwa
Halmashauri hiyo inapitiwa na miradi mbali mbali ya kitafa ikiwemo mradi wa
bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga na ujenzi wa kituo cha jeshi.
Akizungumzia
mafunzo waliyopea amesema ana imani kuwa sasa mafunzo hayo yataleta matokeo
mazuri ikiwa ni pamoja na kuwa na lugha nzuri ya kuwasiliana na wananchi na
kujisogea pamoja na wananchi, huku akiwaasa wasitumie kauli za kuwakatisha tama
wananchi.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo amesema mafunzo yatawasaidia madiwani
kusimamia miradi ikamilike na iwe na ubora unao takiwa huku akitarajia kuona
wananchi wakiibua na kukamilisha miradi ya maendeleo.
Tarimo
ameongeza kuwa madiwani wanapaswa kuhakikisha simu huu wa mavuno wananchi
wanavuna na kuhifadhi mazao yao vizuri pamoja na kuwaelimisha wayatumie vizuri
ili wapate fedha za kujiendeleza.
Kwa
upande wao madiwani hao wamesema mafunzo hayo yamekuwa msaada kwao kwa
kuwaelimisha majukumu yao na mipaka yao ili waweze kitekeleza kwa ufanisi
uwakilishi wao wa wananchi.
Wamesema
wengi walikuwa hawafahamu mipaka yao na hivyo kushindwa kutekeleza baadhi ya
majukumu huku wakieleza kuwa mafunzo yameimarisha ushirikiano baina yao na
watendaji tofauti na hapo awali.
Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Singida wakifuatilia kikao cha baraza hilo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Singida Rashid Mandoa (katikati) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (kulia kwake) na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Singida Eliya Digha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akitunuku cheti kwa mmoja wa madiwani waliohitimu mafunzo ya jitihada za jamii kupitia mbinu shirikishi ya fursa na vikwazo kwa maendeleo
iliyoboreshwa na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment