Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt. Rehema Nchimbi akimkabidhi afisa wa usalama kutoka shirika la TANESCO Mkoa
wa Singida Juma Mauba zawadi ya cheti na TV flat screen baada ya kuchaguliwa
kuwa mfanyakazi bora mwaka 2017.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa
ameshikama na Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi TUCTA Mkoa wa
Singida Aaran Jumbe (kulia kwake) na Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo
(kushoto kwake) wakiimba wimbo maalumu wa wafanyakazi wa Mshikamano daima
pamoja na wimbo wa taifa.
Waajiri
wote Mkoani Singida hususani wakurugenzi wa halmashauri ambao ndio wenye
watumishi wengi wameelekezwa kujenga mahusiano mazuri baina yao ili kuboresha
utumishi wao.
Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa maelekezo hayo wakati wa maadhimisho
ya siku ya wafanyakazi mkoani hapa yaliyofanyika katika uwanja wa Peolpe’s
mjini Singida.
Dkt.
Nchimbi amesema mwajiri na mtumishi sio maadui bali wanapaswa kujenga mahusiani
mazuri hasa kwa mwajiri kujenga mazoea ya kufahamu sifa za watumishi wake,
shida na matatizo yao.
Ameongeza
kuwa waajiri wamekuwa wakisubiria watumishi wakosee ndio wawape adhabu lakini
haipaswi kuwa hivyo kwani mwajiri anatakiwa ahakikishe anaweka mazingira mazuri
na kumuelimisha mtumishi asifanye makosa.
“Ukiona
mtumishi anafanya mambo yanayokinzana na sheria, kanuni na utaratibu, usimkaripie
wala kumtega, mtafutie afisa ustawi wa jamii. Kwa vyo vyote afisa ustawi wa
jamii atamrejesha kwenye mstari stahiki na mambo yatakwenda vizuri”.
Aidha Dkt
Nchimbi amewataka wakurugenzi kutofanya ziara nyingi nje ya halmashauri zao
bali wajikite katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi na watumishi wao
ambazo watazibaini endapo watafanya ziara za kutosha katika halmashauri zao.
Amesema
ili kuboresha maslahi ya watumishi, waajiri wanapaswa kuandaa mafunzo kwa
watumishi juu ya matumizi bora ya fedha ili waweze kutunza fedha zao, kila
halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya watumishi kupewa viwanja vya makazi
pamoja na kila halmashauri kuwa na afisa ustawi wa jamii atayehusika na
watumishi kwa ajila ya masuala ya ushauri.
Pia Dkt.
Nchimbi amekemea tabia mbaya ya baadhi ya wakuu wa idara/vitengo ya kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na wafanyakazi wa kike walio chini yao.
“Wakuu
hawa wa idara/vitengo wanakiuka sheria kanuni na taratibu kwa kuanzisha mahusiano
ya kimapenzi humo humo kazini. Wakati mwingine wanafanya mapenzi na wake za
watu. Tabia hii haikubaliki na haivumiliki hata kidogo. Viongozi au wakuu wa
idara/vitengo wenye tabia ya aina hii, waiache mara moja”, amesema Dk.Nchimbi.
Kwa
upande wao wananchi na watumishi Mkoani Singida wamempongeza rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zake utumishi wa umma
ambapo kwa sasa amerejesha nidhamu na uadilifu kwa kiwango cha kuridhisha.
Wananchi
hao wamesema chini ya serikali ya awamu ya tano watumishi wa umma wamebadilika
sana na sasa wanatoa huduma kwa ukarimu mkubwa, wepesi na uharaka zaidi tofauti
na ilivyokuwa awali.
“Huko
nyuma watumishi wa umma wengi walikuwa wana urasimu wa hali ya juu. Walikuwa
wakitoa huduma huku macho na akili zao zikiwa kwenye ‘whatsapp’. Mbaya zaidi
mwananchi ukipeleka kero zako, wanakuona ni msumbufu. Hivi sasa mambo ni
tofauti kero za wananchi zinatafutiwa majibu na majawabu kwa wakati,” ameongeza
Dkt. Nchimbi akiunga mkono maoni ya wananchi.
Mmoja wa
wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo Sombi Hangida amekiri kwamba ni kweli
watumishi wa umma wamebadilika mno na sasa wanatoa huduma bila kuomba rushwa na
wamekuwa na lugha rafiki kwa wananchi.
Awali
mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi TUCTA Mkoani Singida Aaran
Jumbe amehimiza kuhusu mabaraza ya wafanyakazi kufanyika katika maeneo ya kazi kwa
mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na hasa kuwashirikisha vyama vya
wafanyakazi.
Jumbe
ameongeza kuwa halmashauri zimekuwa zikitoa ushirikiano kwa vyama vya
wafanyakazi na kuomba ushirikiano huo uendelee huku akisisitiza zawadi za
mfanyakazi hodari zinazo ahidiwa na taasisi na halmashauri zitolewe kwa wakati.
Watumishi wa Kutoka
Halmashauri ya Ikungi wakipita mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi na kuonyesha mazao ambayo huzalishwa kwa wingi wilayani humo ambayo ni
viazi vitamu na alizeti katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kwa Mkoa kwa
Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akitoa zawadi ya mpira kwa viongozi wa wafanyakazi wanawake kwa halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida ili waweze kuunda timu za wanawake katika halmashauri zao.
Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi wakati akihutubia
kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kwa Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akitoa zawadi ya mpira kwa viongozi wa wafanyakazi wanawake kwa halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida ili waweze kuunda timu za wanawake katika halmashauri zao.
No comments:
Post a Comment