Kamati za maji za visima kumi vya maji katika
manispaa ya Singida zimekuwa sababu ya miradi hiyo iliyokamilika kwa asilimia
miamoja kutofanya kazi na kuwanufausha wananchi huku ikiwa imegharimu fedha
nyingi za serikali na wahisani hasa benki ya dunia.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi mwishoni mwa wiki hii mara baada ya kukagua miradi hiyo na
kujiridhisha kuwa miradi hiyo imekamilika licha ya kutofanya kazi.
Dkt. Nchimbi amesema sababu kubwa ya kutofanya kazi
miradi hiyo ni udhaifu wa kamati za maji na wanasiasa katika maeneo ya miradi
kutojali shida ya wananchi ya kukosa maji na hivyo kuitelekeza miradi hiyo
badala ya kuisimamia.
Amesema lengo la miradi hiyo ni wananchi wapate
maji safi na salama kwa umbali usiozidi kilometa nne kama ilivyoagizwa na
serikali.
“Katika ukaguzi wangu nimebaini mifumo katika
miradi hii ya maji ipo vizuri sana. Baadhi inaendeshwa kwa umeme na mingine kwa
mafuta ya dizel. Makubaliano yalikuwa baada ya kukamilika miradi hii iendeshwe
na kamati za maji kwa asilimia mia moja”, amesema.
Dkt. Nchimbi amesema wajibu wa kamati hizo ni
pamoja na kukusanya fedha zinazotokana na kuuza maji kwa wateja pamoja na
matengenezo ya miundombinu ya visima hivyo ili miradi hiyo iwe endelevu.
“Fedha zinazopatikana ndizo zitakazoendesha mradi
husika ikiwemo kugharamia matengenezo ya mashine, pampu, miundombinu, kununulia
dizel, umeme na kumlipa mhudumu wa mradi. Makubaliano ni miradi ikikamilika inabaki
mikononi mwa wananchi kupitia kamati zao za maji. Serikali na wafadhili hawatahusika
tena”, amesisitiza Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi amesema serikali na benki ya
dunia imegharamia fedha nyingi kwenye miradi hiyo hivyo haiwezi kuendelea kuona
miradi inabaki kuwa mapambo badala ya kuwaondolea wananchi kero ya maji.
“Naagiza wananchi wajipange upya chini ya kamati
zao wachague jumuiya za watumiaji maji. Kwenye jumuiya hizo za maji wanaweza
kuwepo pia wale waliokuwa kwenye kamati za awali za maji. Jumuiya hizi
ziwajibike kikamilifu zihakikishe zinapata fedha kutokana na mauzo ya maji ili
waendeleze miradi hiyo kwa ufanisi”, amesema Dkt. Nchimbi.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo amesema
kuanzia mei mwaka huu anataka kuona kila wananchi wa manispaa ya
Singida,anapata maji safi na salama kwa umbali mfupi.
“Rasilimali maji ni msingi kwa maisha ya viumbe hai
wakiwemo binadamu. Maji yakiwepo tena kwa umbali mfupi mambo yote yatakwenda
vizuri. Maji yanasaidia kuweka mazingira safi na afya za wananchi zinaboreka. Maji
yana mchango mkubwa kwa jamii inayoelekea kwenye Tanzania ya viwanda”, amesema.
Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa
wanatarajia baadhi ya miradi na hasa ile ya umeme kuibinafisha kwenye mamlaka
ya maji safi na maji taka (SUWASA) kwa ajili ya kuiendesha. Mingi itaendelea
kumilikiwa na wananchi wenyewe.
Awali mhandisi wa maji manispaa ya Singida Max
Hassan Kaaya amesema wanaendelea kuelimisha jamii kuwa miradi hiyo ya maji ni
mali yao hivyo jukumu la kuiendesha ni lao. Pia wanapaswa kuilinda na kuitunza
vizuri.
Naye mkazi wa kijiji cha Mtamaa Hongoa Bunka amesema
elimu zaidi itolewe ili kubadilisha fikiri potofu ya baadhi ya wananchi kuwa
jukumu la kuendesha miradi ya maji ni la serikali. Wabadilike na kutambua
kuwa ni mali yao na wao ndio watakaoiendesha.
No comments:
Post a Comment