Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi (wa pili kulia) akishiriki kuvua samaki aina ya kambare kwenye bwawa
lililopo kwenye shamba la samaki la Mikumbi mjini hapa ikiwa ni sehemu ya
uzinduzi uvuvi kwenye shamba hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi ameziagiza halmshauri zote za Mkoa wa Singida kuanzisha mabwawa ya
ufugaji wa samaki ili kutunza mazingira, kuongeza kipato na kuwa darasa la
kufundishia vikundi na wananchi wengine.
Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo mapema
asubuhi ya leo katika shamba ya ufugaji wa samaki la Mikumbi lililopo manispaa
ya Singida linalomilikiwa na Bwana Charles Kidua wakati wa uzinduzi wa mavuno
ya kwanza ya samaki aina ya kambare katika mabwawa matatu kati ya sita yaliyopo
katika shamba hilo.
Amesema halmashauri zionyeshe mfano
kwa kuiga mbinu ya ufugaji wa samaki katika kutunza mazingira kwakuwa itaongeza
kipato cha halmashauri pia halmashauri iangalie namna ya kufundisha ufugaji wa
samaki vikundi vya vijana kuliko kuwapa mikopo ya pesa ambayo huishia kutumika
vibaya.
Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa uwepo wa
mabwawa hayo ya ufugaji wa samaki unaonyesha kuwa Mkoa wa Singida sio kame na
wala sio mkoa masikini na uko tayari kuandaa chakula kulisha mikoa ya jirani
hasa makao makuu ya nchi ambayo ni Dodoma.
“Tumejipanga na tuko vizuri
kuhakikisha Dodoma inapata chakula kizuri na cha uhakika, Singida sio kame wala
masikini, samaki hawafugwi kwenye ukame, Singida sio kame hata kidogo”
amesisitiza Dkt. Nchimbi.
Ameongeza kuwa watendaji wote
wanapaswa kuziishi taaluma zao kama ambavyo mmiliki wa mabwawa hayo ambaye ni
afisa maliasili ambaye ameweza kuanzisha bwawa la samaki na hivyo kuwataka
watendaji wengine mfano maafisa kilimo, mifugo kuwa mifano kwa jamii kwa
kuonyesha manufaa ya taaluma hizo.
Naye mmiliki wa mabwawa hayo Bw.
Charles Kidua amesema amekuwa na wazo la kuanzisha mabwawa ya ufugaji wa samaki
kwa muda mrefu lakini amefanikiwa kuanzisha mradi huo mwaka 2016 kwa gharama ya
shilingi milioni 12.
Kidua amesema kuanzishwa kwa mabwawa
hayo kumewafaidisha baadhi ya wananchi amabo tayari wamejifunza kutka kwake na
kuchukua vifaranga vya samaki kwake.
“Ukiwa na eneo zuri lenye maji uanzishaji
wa ufugaji wa samaki kwa bwawa moja unaweza kukugharimu shilingi laki tatu tu,
jirani yangu hapa yeye ameanzisha bwawa lake na kuchukua vifaranga hapa kwangu,
kuna wananchi wengine pia wameanzisha mabwawa yao kupitia elimu wanayojifunza
kutoka hapa” amesema Kidua.
Ameongeza kuwa changamoto aliyokumbana
nayo katika kuanzisha mradi huo ni pamoja na ukosefu wa vifaranga wa samaki
katika mikoa jirani na hivyo kumlazimu kuvifuata Mwanza hali ambayo inaongeza
gharama.
Baadhi ya maofisa wa serikali na
wananchi walioshuhudia uvunaji wa samaki hao wamekiri kuhamasika na wao kuanzisha
ufugaji wa samaki. Mavuno ya samaki aina ya kambare katika shamba hilo yatafuatiwa
na uvunaji wa samaki wengine aina ya sato ambao pia wapo katika mabwawa ya
shamba hilohilo.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa mmiliki wa shamba la ufugaji
samaki la Mikumbi Bw. Charles Kidua (wa pili kulia) wakati akikagua shamba hilo
lenye mabwawa sita yaliyofungwa samaki aina ya sato na kambare.
Mmiliki wa shamba la samaki Mikumbi
mjini Singida na afisa maliasili Mkoa wa Singida Charles Kidua (aliyenyoosha
mkono) akimweleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza
kulia) muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa uvuvi kwenye shamba hilo asubuhi ya
leo.
Baadhi ya samaki aina ya kambare
waliovuliwa mapema leo kwenye uzinduzi wa uvuvi shamba la samaki la Mikumbi
lililopo mjini hapa.
No comments:
Post a Comment